Kiongozi wa Timu ya wataalamu wanaofanya maboresho ya mfumo wa kielektroniki wa PlanRep, Bi. Nseya Kipilyango akizungumza wakati wa mafunzo ...
Kiongozi wa Timu ya wataalamu wanaofanya maboresho ya mfumo wa kielektroniki wa PlanRep, Bi. Nseya Kipilyango akizungumza wakati wa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo yanayoendelea Mjini Kigoma.
Mmoja wa Wawezeshaji wa Mfumo wa mfumo wa kielektroniki wa PlanRep Kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bi Jacqueline Manyanga akiwasilisha mada kwa watumiaji wa mfumo huo yanayofanyika Mkoani Kigoma yakihusisha Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma.
Washiriki wa Mafunzo wakifuatilia mada wakati wa mafunzo hayo yanayoendelea mjini Kigoma.
Tanzania imetajwa kuwa nchi ya kwanza Kusini mwa Afrika kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa PlanRep ulioboreshwa ambao husaidia katika mipango, bajeti na kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini kote.
Akizungumza katika mahojiano maalum mjini Kigoma, Mkuu wa Timu ya Mifumo ya TEHAMA kutoka mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) Desderi Wengaa, amesema kuwa mfumo huo utasaidia Taifa kufikia maendeleo endelevu kwa wakati kwani utaunganishwa na mifumo mingine iliyopo sasa na utawashirikisha wananchi wote.
“Mfumo huu utawezesha kutolewa kwa taarifa za miradi ya maendeleo zinazohusu sekta zote zilizoainishwa katika mipango na bajeti kwa wakati katika kipindi chote cha mwaka” alisema Wengaa.
Aliendelea kusema kuwa PlanRep iliyoboreshwa inaunganisha sekta zote katika mfumo mmoja ambao ni wa kitaifa tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kila sekta ilikuwa na mfumo wake. Awali mfumo uliokuwa ukitumika haukuwa unaendana na mahitaji ya wakati hivyo kushindwa kufanya uchambuzi wa kina katika kusimamia rasilimali zilizokuwepo ikiwemo fedha.
Aidha,watumiaji wa mfumo huo wataweza kuutumia mahali popote kwa kuwa ni wa kitaifa na utaondoa changamoto ya kuwepo kwa matoleo tofauti tofauti. Hali hii itasaidia kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumika kwa watoa huduma wa mifumo ya awali katika halmashauri na mikoa yote nchini.
Kuwepo kwa mradi wa maboresho ya mifumo katika sekta za umma (PS3) kumesaidia wataalamu wa TEHAMA na watumiaji wengine wa mfumo wa PlanRep iliyoboreshwa kujengewa uwezo ili kuimarisha utendaji wao katika kuwahudumia wananchi. Miongoni mwa wanufaika wa mfumo huu ni waganga wakuu,wachumi, maafisa mipango, makatibu wa afya na watoa huduma katika ngazi mbalimbali hasa katika zahanati, vituo vya afya na shule.
Kuunganishwa kwa mfumo huu katika mifumo ya malipo, kukusanya mapato, kukusanya taarifa za sekta ya afya na mifumo mingine iliyokuwepo awali kutawezesha uchambuzi wa bajeti kufanyika kwa njia ya mtandao, hivyo kuifanya Mikoa, Wizara, halmashuri na taasisi za Serikali kuwa na toleo moja la bajeti.
Mfumo wa PlanRep iliyoboreshwa umetengenezwa na wataalamu wazalendo hivyo itakuwa rahisi katika kufanya maboresho endapo yatahitajika kwa kuzingatia mahitaji ya wakati na mikoa husika. Mradi huu wa kuboresha mifumo ya sekta za umma unatekelezwa katika Mikoa 13, Halmashauri 93 na baadaye utatumika nchi nzima.
COMMENTS