Na Mwandishi Maalum Serikali ya Israel imeahidi kuendelea kupanua wigo katika miradi yake mbalimbali iliyopo hapa nchini ikiwemo ...
Na Mwandishi Maalum
Serikali ya Israel imeahidi kuendelea kupanua wigo katika miradi yake mbalimbali iliyopo hapa nchini ikiwemo miradi ya afya ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Ahadi hiyo imetolewa jana na Waziri wa Sheria wa nchi hiyo Mhe. Aleyet Shaked alipotembeleaTaasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili kuona ushirikiano uliopo kati ya Taasisi hiyo na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini humo.
Mhe. Shaked alisema kuwa kwa upande wa afya katika Taasisi ya Moyo wamekuwa wakifanya matibabu ya moyo kwa watoto na katika siku za baadaye wataangalia namna ya kuongeza huduma hiyo ili iweze kuwasaidia watu wengi zaidi
“Nikirudi nyumbani nitafanya majadiliano na waziri wa Afya na kumpa mrejesho wa miradi tunayoifanya hapa nchini, nitamuomba kuendeleza kukuza uhusiano uliopo kwa kupanua wigo wa miradi yetu kwenye maeneo mengine ya afya katika sehemu zingine za nchi hii itasaidia kuweza kufikia watu wengi zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alisema kabla ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2015 asilimia 65 ya upasuaji wa moyo kwa watoto ulikua unafanywa na madaktari wa nje kwa kushirikiana na watanzania.
Hivi sasa madaktari wa Taasisi hiyo wanafanya upasuaji wa moyo kwa watoto kwa asilimia 70 na asilimia 30 inafanywa kwa ushirikiano na wageni wanaokuja katika kambi maalum za matibabu hii ni kutokana na upasuaji mwingine kuhitaji utaalam wa juu zaidi.
“Tangu tumeanza kufanya kazi kama Taasisi mwaka 2015 hadi sasa tumeshafanya upasuaji wa moyo kwa watoto 400 na asilimia 70 ya hao watoto wamefanyiwa na daktari wetu bingwa wa upasuaji wa Moyo kwa watoto Godwin Sharau ambaye amesoma nchini Israel”, alisema Prof. Janabi.
Mwaka 2015 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianza ushirikiano na SACH kwa kusomesha madaktari na wauguzi na kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo kwa watoto ambapo watoto wanaokutwa na matatizo yanayohitaji matibabu ya hali ya juu wanatibiwa nchini Israel bila malipo.
 |
Waziri wa Sheria wa Israel Mhe. Aleyet Shaked akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi mara baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi jana ya kuona ushirikiano uliopo wa matibabu ya moyo kwa watoto kati ya JKCI na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini Israel. Kulia ni Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Kambi.
|
 |
Waziri wa Sheria wa Israel Mhe. Aleyet Shaked akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi jana katika Taasisi hiyo. Mhe. Shaked alitembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kuona ushirikiano ulipo wa matibabu ya moyo kwa watoto, kusomesha madaktari na wauguzi kati ya JKCI na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini Israel.
|
 |
Waziri wa Sheria wa Israel Mhe. Aleyet Shaked akiangalia makala ya video inayoonyesha matibabu ya moyo kwa watoto yanayofanywa na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini Israel. Tangu mwaka 2015 JKCI kwa kushirikiana na SACH ya nchini Israel wanafanya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto ambapo watoto wanaokutwa na matatizo wanatibiwa hapa nchini na wanaokutwa na matatizo yanayohitaji matibabu ya hali ya juu wanatibiwa nchini humo bila malipo.
|
 |
Waziri wa Sheria wa Israel Mhe. Aleyet Shaked akisaini kitabu cha wageni alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jana kwa ajili ya kuona ushirikiano ulipo wa matibabu ya moyo kwa watoto, kusomesha madaktari na wauguzi kati ya JKCI na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini Israel. Kushoto ni Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Kambi na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi.
|
 |
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiongea na waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa ziara ya Waziri wa Sheria wa Israel Mhe. Aleyet Shaked alipotembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kuona ushirikiano ulipo wa matibabu ya moyo kwa watoto, kusomesha madaktari na wauguzi kati ya JKCI na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini Israel. (Picha na JKCI) |
COMMENTS