Na Is-haka Omar, Zanzibar. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ ameshiriki katika mazishi ya watoto ...
Na Is-haka Omar,
Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ ameshiriki katika mazishi ya
watoto wanne waliofariki dunia jana (juzi) baada ya kuingia kwenye gari
iliyokuwa sehemu ya maegesho na likajifunga hali iliyopelekea watoto hao kukosa
hewa na kufariki huko Kidongo Chekundu Unguja.
Marehemu hao
waliotambuliwa kwa majina ya Mwatma Mohamed Malawi (2), Haisam Mustafa(2),
Munawar Ahmed Khamis (3) na Muslim Hamza bakar (2) wote wamezikwa leo katika
maeneo tofauti ya Makaburi ya Mwanakwere na Kiembe samaki Mbuyu Mnene
Unguja.
Akizungumza mara baada
ya maziko hayo Naibu Katibu huyo huko katika makaburi ya Mwanakwerekwe, alisema
CCM imepokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa taarifa ya vifo vya watoto hao
na inatoa mkono wa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia zilizopata
msiba huo na kuwasihi waendelee kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki cha msiba huo.
Alisema watoto hao
walitarajiwa kuwa ni miongoni mwa viongozi na wataalamu wa fani mbali mbali wa
baadae hivyo msiba huo umeacha pengo kubwa kwa familia na taifa kwa
ujumla.
Aidha Dkt. Mabodi
aliwataka wazazi na walezi nchini kuwa karibu na watoto wao kwa kuhakikisha
mazingira yanayotumiwa na watoto kucheza yanakuwa katika hali ya usalama ili
kuepuka athari zinazoweza kusababisha majeraha ama vifo kwa watoto wao.
“ Kwa niaba ya CCM
Zanzibar nawaomba wanafamilia wote wawe wavumilivu kwa kipindi hichi cha msiba
huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea kufanya uchunguzi wa kina juu ya
kubaini chanzo halisi cha vifo hivi na kutoa taarifa kwa umma.”, alisema Dkt.
Mabodi.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti baadhi ya ndugu na wazazi wa marehemu hao walifafanua kuwa
(jana) juzi majira saa 5:00 asubuhi watoto hao walikuwa wakicheza katika maeneo
ya nyumbani kwao ghafla hawakuonekana mtaani hali iliyozusha hofu kwa familia
za watoto wao na wakachukua juhudi za kuwatafuta katika maeneo mbali mbali hasa
katika bandari na maeneo mengine kwa kuhofia kuwa wameibiwa na watu
wasiojulikana.
Akieleza zaidi Bw.
Ahmed Khamis ambaye ni baba mzazi wa mtoto aliyefariki ambaye ni Munawar,
alidai kuwa katika harakati za kuwatafuta watoto hao walifanikiwa kuwapata
majira ya saa 2:00 usiku wa july 16, Mwaka huu wakiwa ndani ya gari moja
lililokuwa limeegeshwa katika maegesho ya gari za mtaani ambalo mmiliki wake
aliliweka kwa muda mrefu na alikuwa amesafiri.
Bw. Ahmed alieleza
kwamba baada ya hapo yeye kwa kushirikiana na majirani mbali mbali
walishirikiana kuvunja milango ya gari hilo na kufanikiwa kuwatoa watoto hao
wakiwa wamezimia na kupelekwa hospitali kuu yaMnazi Mmoja ambapo baada ya
kufanyiwa vipimo na madaktari wakaambiwa kuwa tayari wamefariki dunia kutokana
na kukosa hewa kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa maelezo
ya shuhuda mmoja aliyehusika na harakati za kuwatoa watoto ndani ya gari
walipokutwa wamefariki alisema mazingira yake yanaonyesha kuwa kabla ya watoto
hao kufariki walikuwa wakichezea gari hilo na walipoingia ndani mlango
ulijifunga na kushindwa kutoka nje hali iliyosababisha kukosa hewa na kufariki
dunia.
Viongozi mbali mbali
wa serikali na Chama Cha Mapinduzi waliudhuria katika mazishi hayo wakiwemo
Katibu wa Kamati Maalum, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Bi. Waride
Bakari Jabu, Mbunge wa Jimbo la Jang’ombe Ali Hassan Omar ‘King’ na Waziri
wa Kazi,uwezeshaji, wazee, vijana wanawake na watoto
Maudline Castico.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Saadalla akishirikiana na wananchi wengine katika mazishi ya watoto hao. |
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Saadalla akishirikiana na wananchi wengine katika mazishi ya watoto hao. |
COMMENTS