STATE HOUSE ZANZIBAR OFFICE OF THE PRESS SECRETARY PRESS RELEASE Zanzibar ...

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 31.12.2017

RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa juhudi za
kuimarisha ukusanyaji wa mapato zimeiwezesha Serikali anayoiongoza kutekeleza
ahadi aliyoitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ya kupandisha
mishahara ya kima cha chini kwa asilimia mia kutoka TZS 150,000 mpaka TZS
300,00 kwa mwezi kwa watumishi wa Serikali.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika risala yake ya
kuukaribisha mwaka mpya wa 2018 aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, Ikulu
mjini Zanzibar na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza
kuongeza pesheni kwa wastaafu na kuendelea kutoa fedha za Pensheni ya Jamii kwa
wazee wote wanaostahiki.
Alieleza kuwa tangu mwezi April, 2017 walengwa wa
nyongeza hizo wamekuwa wakifaidika na neema hiyo ambapo pia, katika mwaka 2017
Serikali imezidi kuimarisha maslahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi wanaopata
mshahara wa kima cha chini jambo ambalo ni faraja kuona waajiri wengi katika
sekta hiyo wameshaitikia wito licha ya kuwepo baadhi waliotaka kurejesha nyuma
juhudi hizo za serikali.
Aliongeza kuwa uchumi wa Zanzibar unaendelea kuimarika na
katika robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2017 (Januari-Machi), kasi ya ukuaji
uchumi ilifikia asilimia 6.3 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 5.2 kwa
kipindi kama hicho cha robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2016 ambapo katika kipindi
cha robo mwaka ya pili (Aprili-Juni) kwa mwaka 2017 ukuaji wa uchumi nao
uliimarika na kufikia asilimia 8.2.
Hivyo, Dk. Shein alieleza kuwa ni jukumu la kila mmoja
katika mwaka huu mpya wa 2018 la kuongeza juhudi ili kuhakikisha kuwa
yanaendelea kutekelezwa vizuri malengo hayo yaliobainishwa kwenye MKUZA III na
mipango mengine ya maendeleo.
Dk. Shein aliendelea kutoa pongezi kwa wananchi wa Mikoa
yote ya Zanzibar kwa juhudi zao kwa maendeleo ya kutia moyo yaliyopatikana
katika sekta mbali mbali za maendeleo kwenye ziara za Mikoa aliyofanya Unguja
na Pemba zikiwemo sekta za kiuchumi na kijamii ikiwa ni katika kutekeleza Ilani
ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, Dira ya Maendeleo ya 2020, MKUZA
111 na Malengo ya Maendeleo Endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa miundombinu mbali mbali katika
sekta ya afya na hivi sasa juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuimarisha huduma
pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa vya utibabu katika hospitali na vituo
vya afya.
Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha uliomalizika
2017/2018, Serikali imetenga jumla ya TZS 7.0 bilioni kwa ununuzi wa dawa na
vifaa vya utibabu, sawa na ongezeko la asilimia 42.9 ikilinganishwa na kiwango
kilichotengwa kwa mwaka 2016/2017.
Kwa upande wa sekta ya elimu, Dk. Shein alisema kuwa
ikiwa tayari serikali imeshaanza ujenzi wa mradi wa skuli 9 za ghorofa katika
sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba, ili kuimarisha mazingira ya kusomea kwa
wanafunzi hapa nchini ambapo ujenzi wa skuli hizo utagharimu jumla ya TZS 24.4
bilioni ambazo ni mkopo kutoka Mfuko wa OPEC dhamira ikiwa ni kumaliza ujenzi
wa skuli hizo ifikapo Januari mwaka 2019.
Dk. Shein alieleza kuwa katika sherehe za Elimu bila ya
malipo zilizofanyika tarehe 23 Septemba, 2017 alitangaza rasmi kuondoa michango
katika elimu ya Sekondari kuanzia mwezi wa Julai, 2018 hatua iliyolenga
kuendeleza utoaji wa elimu bila ya malipo kwa skuli zote za msingi na sekondari
kwa watoto wote kwa misingi ile ile iliyoanzishwa na waasisi wa nchi hii.
Alieleza kuwa mwaka 2017 unamalizika ikiwa tayari kazi ya
kulishuhulikia tatizo la kupoteza fedha za mishahara kwa wafanyakazi
wanaochukua likizo bila ya malipo, wanaotoroka kazini, wanaolipwa kinyume na
utaratibu (hewa), ambapo taarifa rasmin itatolewa na Serikali muda mfupi ujao.
Aliongeza kuwa katika mwaka 2018, Serikali inaendeleza
utafiti wa mafuta na gesi kwa kutegemea taarifa itakayotolewa na wataalamu na
kutoa wito kwa wananchi kuwa watulivu na Serikali itatoa taarifa rasmi ya matokeo
ya utafiti huo unaofanywa kwa maslahi ya Zanzibar.
Aliwataka wananchi kutosikiliza maneno ya mitaani na
kwenye mitandao wakati serikali yao ipo na kuwataka kuendelea kuunga mkono
juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuiendeleza sekta yua
Mafuta na Gesi Asilia.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa Mpango Maalum wa
Kulifufua Zao la Karafuu ulioanzishwa mara tu baada ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar Awamu ya Saba kuingia madarakani mwaka 2010 kwa kupanda mikarafuu
mipya limeanza kutoa matokeo mazuri.
Alisema kuwa hadi tarehe 20 Disemba, 2017 wakulima wa
karafuu walikuwa wameshauza karafuu ZSTC zenye thamani ya TZS 108.8 bilioni
ambapo kiwango hicho cha fedha kimekuwa
na mchango mkubwa katika kuimarisha mzunguko wa fedha na kukuza sekta nyengine
za kiuchumi.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na wananchi wote wanaendelea kuwakumbuka wakati wote wanajeshi 15 wa
Jeshi la Wanachi wa Tanzania waliofariki huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
ambako walikuwa katika shughuli za kusimamia amani chini ya uongozi wa Umoja wa
Mataifa.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupanga na
kutekeleza mikakati mbali mbali ya kulinda na kudumisha amani nchini, Barani
Afrika na duniani kote kwa jumla.
Dk. Shein pia, aliwasisitiza wananchi wakati wakiupokea
mwaka mpya wa 2018, kila mmoja aweke dhamira ya dhati ya kufanya kazi kwa bidii
na maarifa na kuongeza jitihada za kuongeza kipato na kupambana na umasikini.
Aliwataka wananchi kushirikiana na Serikali kwa lengo la
kuimarisha utawala bora, kukuza uadilifu na uwajibikaji na kusimama imara kwa
vitendo katika mapambano dhidi ya rushwa, uhujumu wa uchumi na dawa za kulevya,
sambamba na kujidhatiti katika kuvitokomeza vitendo vya udhalilishaji wa
kijinsia.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi kuanza
kusherehekea mwaka mpya 2018 kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya
Sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 2018
pamoja na kushiriki katika ufunguzi na uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi
mbali mbali ya maendeleo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal
Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
COMMENTS