Fatma Salum-MAELEZO Serikali imedhamiria kuzalisha wataalamu wa maji wa kutosha kukidhi mahitaji ya sasa na kuwafikishia wananch...
Fatma Salum-MAELEZO
Serikali
imedhamiria kuzalisha wataalamu wa maji wa kutosha kukidhi mahitaji ya
sasa na kuwafikishia wananchi wote maji safi na salama kupitia miradi
mbalimbali inayotekelezwa kote nchini.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo cha Maji cha
Dar es Salaam Dkt. Shija Kazumba wakati wa mkutano na vyombo vya habari
uliolenga kueleza mikakati ya chuo hicho ya kuzalisha wataalamu wenye
sifa na weledi.
“Wanafunzi
waliopo sasa ni 1849, kati yao 489 ni wanawake na dhamira yetu ni
kuhakikisha kuwa kuna mafundi sanifu wa kutosha kulingana na mahitaji
ya sasa na ukuaji wa sekta ya maji”alisisitiza Dkt. Kazumba.
Alifafanua
kuwa chuo hicho kimeanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuwainua
wanafunzi wa kike ili wajiunge katika masomo ya uhandisi wa maji,
mafundi sanifu, upimaji wa ubora wa maji, umwagiliaji na hali ya hewa
lengo likiwa ni kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.
“Dhamira
ya kuwainua wanafunzi wa kike inaonyesha nia ya Serikali kuwawezesha
wanawake kushiriki kikamilifu katika kukuza na kuendeleza sekta
mbalimbali hapa nchini ikiwemo sekta ya maji”. Aliongeza Dkt. Kazumba.
Pia
alibainisha kuwa Serikali imewezesha kuwepo kwa maabara ya kisasa kwa
ajili ya kupima ubora wa maji, kupima ubora wa mita na maabara ya kukata
mabomba zote zikiwa na lengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa maji
safi na salama.
Dkt
Kazumba alitoa rai kwa Halmashuri zote nchini kuajiri Mafundi Sanifu na
Wahandisi wa Maji kwa ajili ya kuongeza tija katika sekta ya maji.
Alifafanua
kuwa Mafundi Sanifu waliohitajika kwa kipindi cha mwaka 2013 ilikuwa ni
3000 na mwaka 2014 ilifikia 6000 na dhamira ya Serikali ni kuhakikisha
kuwa kila mhandisi mmoja anakuwa na mafundi 5 wa kumsaidia kutekeleza
majukumu yake.
Chuo
cha Maji kilianzishwa mwaka 1974 kwa lengo la kuendeleza na kuzalisha
wataalamu wa sekta ya maji kupitia mafunzo, ushauri na tafiti
mbalimbali.
Mkuu
wa Chuo cha Maji Dkt. Shija Kazumba akiongea na waandishi wa habari leo
jijini Dar es Salaam kuhusu mkakati wa Chuo kuhakikisha Tanzania inakuwa
na Mafundi Sanifu wa kutosha katika sekta ya maji ili kuendana na kasi
ya Serikali kufikisha huduma ya maji kwa wananchi wote. Kulia ni Afisa
Habari na Masoko wa chuo hicho Bw. George Karumuna.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Chuo cha Maji na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.



COMMENTS