Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake. (Picha zote ...
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea Makadirio ya Mapato na Matumizi ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka 2017/2018
Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob akielezea jinsi Bajeti ya
Manispaa hiyo ilivyopitishwa kwa kuungwa mkono kwa 100% kwenye kikao
cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa hiyo kilichofanyika
4/03/2017.
Na Mathias Canal, Dar es salaam
Halmashauri
ya Manispaa ya Ubungo imebainisha namna ya kuboresha maisha ya wakazi
wake kwa kuweka mpango mzuri wa muda wa kati wa mwaka 2017/2018 – 2019/2020 ambao unalenga
kukuza uchumi, na kupunguza umaskini ili kufikia maendeleo endelevu ya
kijamii, kiuchumi na kimazingira kwa wananchi wake.
Mpango
huo umeandaliwa kwa kuzingatia sera na miongozo ya Kitaifa, kwa mujibu
wa sheria ya bajeti Na. 11 ya mwaka 2015, Dira ya Taifa ya Maendeleo
2025 ambapo Mpango mkakati ni kutekelezwa kwa matokeo makubwa sasa
(BRN), Sera ya Taifa ya UKIMWI, Sera za kisekta, Mipango Shirikishi
Jamii ya Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD) ya Kata na Mitaa.
Hayo
yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea juu ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya kawaida na ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka 2017/2018,
Makadirio yalijadiliwa na Waheshimiwa Madiwani katika Kamati za
Kudumu,na kuidhinishwa na baraza maalumu la madiwani jumamosi ya tarehe 04/03/2017 kwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Mstahiki
Meya alisema kuwa ili kutekeleza dhana nzima ya ung’atuaji wa madaraka,
mpango huu umeshirikisha jamii katika mpango shirikishi ambao huanzia
ngazi ya Mtaa ambapo Hali hiyo imezingatia vipaumbele na mahitaji halisi
ya wananchi katika maeneo yao.
Alisema
kuwa Mpango huo umejielekeza katika kutoa kipaumbele maeneo yanayoweza
kutoa matokeo ya haraka (quick wins) ambayo yatasaidia ukuaji wa uchumi
kwa haraka katika kipindi kifupi na kutoa huduma bora kwa wananchi wa
Ubungo.
Aidha
alieleza maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mpango huo kuwa ni pamoja
na Kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Manispaa, Ujenzi wa
ofisi za makao makuu ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Kuboresha
miundombinu ya Afya, Shule za Msingi na Sekondari, Kuboresha miundombinu
ya maji, mifereji, taa za barabarani barabara na Kilimo mjini,
Kuboresha hifadhi ya mazingira na ukusanyaji wa taka, Kuimarisha
ushirikishwaji wa jamii katika upangaji na utekelezaji wa miradi ya
maendeleo na Kuboresha mazingira ya wafanyabiashara ndogo ndogo.
Katika harakati za kuyafikia
mafanikio yaliyotajwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya
Ubungo ameeleza kuwa Manispaa hiyo Uimarisha mahusiano mazuri kati ya
Serikali, mashirika yasiyo ya Kiserikali na wadau wengine, Kuendelea
kujenga uwezo na ujuzi kwa watumishi katika utoaji wa huduma zilizo bora
na haraka, Kuimarisha Utawala bora, Uwajibikaji na Uwazi sambamba na
Kujenga uwezo wa viongozi wakiwemo Madiwani, Wenyeviti wa serikali za
mitaa katika kusimamia shughuli za wananchi.
Sambamba na hayo pia amesema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa mwaka 2016/2017 ilikadiria kutumia Sh. 116,045,935,228.99 ikiwa ni pamoja na fedha za mfuko wa barabara.
Kuanzia Julai hadi Disemba, 2016, Halmashauri ilikuwa imekusanya Sh. 1,024,839,737.74 fedha za vyanzo vya ndani sawa na asilimia 8 ya maoteo yaTsh 13,300,416,090.50 ya vyanzo vya ndani yaliyotarajiwa kukusanywa kwa nusu mwaka wa bajeti yaani Julai 2016 hadi Disemba 2016.
Katika kipindi hiki Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imeweza kutumia kiasi cha Sh. 150,764,997.88. ya
makusanyo yake ya ndani yaliyoanza kukusanywa mwezi Novemba 2016, na
hakuna fedha yoyote ya ruzuku iliyopokelewa hadi sasa kama inavyooneshwa
katika Jedwali hapa chini.
Jacob
ametaja changamoto mbalimbali zinazopelekea ucheleweshaji katika kutoa
huduma na kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na Mwamko mdogo
wa wananchi kuchangia shughuli za maendeleo, Fedha za miradi za Serikali
kuu na wafadhili kutoletwa kwa wakati na hivyo kuathiri utekelezaji wa
miradi kama ilivyopangwa. Miradi yote iliyopangwa kutekelezwa kwa fedha
za ruzuku haijaanza, Makusanyo hafifu ya mapato ya ndani kutokana na
mgawanyo wa Halmashauri na upya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Hivyo miradi iliyopangwa kutekelezwa kwa mapato ya ndani mingi
haijaanza kutekelezwa, Ukosefu wa maeneo ya kujenga majengo mapya kama
vile Shule za Msingi na Sekondari, pamoja na Madai makubwa ya fedha za
fidia katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo Sababu zilizopelekea kukusanya mapato ya ndani chini ya malengo ni pamoja na Serikali
kuhamishia kodi ya Majengo kukusanywa na Mamlaka ya mapato TRA ambapo
kwa wigo wa makusanyo uliopo wa kodi ya majengo ni shilingi bilioni 6,
kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 ya makusanyo ya ndani yenye makadirio ya
Tsh. 26.6 bilioni, Kushuka kwa mauzo ya wafanyabiashara hali
inayopelekea biashara kufungwa na malipo ya ushuru wa huduma kupungua,
na SUMATRA kubadilisha route za mabasi ya kariakoo (160) na mikoani
(350) kimepunguza makusanyo katika kituo chetu cha Simu 2000 (Sinza bus
terminal) ambapo takribani magari kati ya 510 yaliyokuwa yanaingia
kituoni yamepungua na kusababisha upungufu wa Sh. 12,900,000/= kwa kila
mwezi.
Sababu
zingine ni Upungufu wa vitendea kazi baada ya Mgawanyo wa Halmashauri
na hasa ukosefu wa magari yanayotumika kukusanyia mapato, Kipindi cha
mpito tangu kuanzishwa kwa Halmashauri hadi kuanza kukusanya mapato ya
ndani kwa Halmashauri yetu mpya ilipoanzishwa rasmi tarehe 1/07/ 2016,
imeanza kukusanya mapato yake ya ndani yenyewe kuanzia mwezi Novemba
2016, Walipakodi kuendelea kulipia katika Halmashauri mama (Kinondoni)
kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2016 kwa mazoea kiasi cha takriban
Sh. milioni 500 kimekusanywa kimakosa na Halmashauri ya Manispaa ya
Kinondoni mawasiliano yanafanyika ili kurejesha makusanyo hayo.
Ili kukabiliana na changamoto hizo Mikakati ya Halmashauri imetajwa kuwa ni pamoja na Kuendelea
kutoa elimu na kuhamasisha wananchi ili kutambua kuwa miradi ya
maendeleo wanayochangia ni kwa ajili ya manufaa yao wenyewe na vizazi
vijavyo, Kendelea kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa kubuni vyanzo
vipya kwa mujibu wa sheria na kuimairisha ukusanyaji wa mapato katika
vyanzo vilivyopo.
Mikakati mingine ni Kukusanya
mapato yote kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, na Kununua maeneo ya
pembezoni mwa mji na kuhakikisha tunalipa fidia kabla ya kuyatwaa maeneo
ya watu.
Vipaumbele
vitakuwa katika maeneo yafuatayo:-Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo
Mhe Boniface Jacob amebainisha kuwa Bajeti hiyo imelenga katika
kuboresha maisha ya wananchi na kukuza kipato cha mkazi ili kukuza
uchumi wa ndani ambapo ametaja vipaumbele 13 ambavyo vitapaswa kufanyiwa
kazi katika bajeti hiyo kuwa ni pamoja na Kuongeza ukusanyaji wa mapato
ya ndani kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, na Kuboresha utoaji wa
huduma za afya kwa kununua madawa na vifaa tiba na kuboresha miundo
mbinu ya afya kwa kupanua hospitali ya Sinza kwa kujenga ghorofa ya pili
jengo la OPD, Ujenzi wa wodi ya wazazi kituo cha afya mbezi, ujenzi wa
jengo la kuhifadhia chanjo Mabibo, kujenga zahanati ya King’azi Kwembe
Jumla ya Tsh. 5,732,424,610.00 zimetengwa.
Kuboresha
miundombinu ya barabara kwa kujenga Madaraja/ Makalvati, barabara kwa
kiwango cha lami, kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara, muda
maalum, maeneo korofi, njia za waenda kwa miguu, Ujenzi wa Mifereji
katika barabara za Manispaa ambapo Jumla ya Tsh 6.2 bilionzimetengwa,
Kuboresha miundo mbinu ya shule za Msingi na Sekondari kwa kununua
madawati, kujenga madarasa, vyoo, nyumba za walimu, maabara na ukarabati
wa miundombinu. Jumla ya Tsh.5.5 billion zimetengwa
na Kutoa mikopo kwa wajasiliamali wa dogo kwa vikundi vya wanawake na
vijana ili kuongeza ajira na kukuza kipato cha Mkazi. Jumla ya Tsh.1.9 billion zimetengwa.
Kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kutoa huduma kwa kujenga Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo. Tsh.1.7 billion zimetengwa, Kununua magari na mitambo magari 6 ya ofisi, gari moja la maji machafu na gari 1 la maji safi, jenereta. Jumla ya Tsh 1.35 billion zimetengwa, Kulipa fidia kupisha ujenzi wa miradi mabali mbali ya maendeleo na kufanya uthamini wa mali za Manispaa. Jumla ya Tsh.1.2 billion zimetengwa, Kuboresha usafi wa mazingira na na ukusanyaji taka na kununua magari makubwa ya taka Jumla ya Tsh.1 billion zimetengwa,
Kuboresha upatikana maji safi na salama kwa wakazi wa Ubungo kwa
kujenga na kukarabati miundo mbinu ya maji. Jumla ya Tsh.550 million zimetengwa
kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji na Mipango miji, kupima na
kumilikisha maeneo ya umma na kutekeleza mfumo wa anuani za makazi
(Postcode). Jumla ya Tsh.550 million zimetengwa.
Aidha
Halmashauri ya Maninspaa ya ubungo imetenga Tsh 42 milioni kwa mwaka
huu kwa ajili ya kijiji cha michezo kilichopo kibwegele ambapo kijiji
hicho kitakuwa na kiwanja cha mpira wa miguu na viwanja vya michezo ya
watoto, kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo Tsh 50 milioni zimetengwa,
na Kuboresha na kukarabati masoko Manispaa tumetenga Tsh 1.2 Bilioni,
kwa ajili ya kuboresha masoko ambayo ni Mabibo, Shekilango, Sinza one,
na Mbezi pia fedha hizo zitatumika kulipa fidia na kupima maeneo kwa
ajili ya wamachinga na maeneo ya uwekezaji.
COMMENTS