Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma Serikali haina mamlaka ya kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katik...
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali haina mamlaka ya kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa mikopo.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji ameeleza hayo leo
Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Baraza la
Wawakilishi Machano Othman Said juu ya lini Serikali itaweka utaratibu
wa kupunguza riba ya mikopo walau kufikia asilimia 10 – 12 badala ya
sasa ambayo ni asilimia 17 – 20.
“Mabadiliko
ya Sekta ya Fedha ya mwaka 1991 yalipelekea Serikali kujitoa katika
uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki nchini ili kuruhusu
mfumo wa soko huria, hususan nguvu ya soko kuamua viwango vya riba za
mikopo, riba za amana na gharama nyingine za huduma za kibenki,”
alifafanua Dkt. Ashatu Kijaji.
Aliendelea
kwa kusema kuwa viwango vya riba za mikopo na riba za amana pamoja na
riba za mikopo kati ya benki na benki hupangwa kwa kuzingatia gharama za
upatikanaji wa fedha, gharama za uendeshaji, riba za dhamana za
Serikali, sifa za mkopaji na hatari ya mkopaji kutolipa mkopo pamoja na
kasi ya mfumuko wa bei.
Aidha
Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia
viwango fulani vya riba katika biashara zao, kutaifanya Benki Kuu kukosa
nguvu na mamlaka ya kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara
kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza.
Vile
vile amesema kuwa kiwango cha hatari ya kutolipa mkopo ni miongoni mwa
vigezo vinavyotumiwa na mabenki katika kupanga viwango vya riba za
mikopo, ambapo kwa sehemu kubwa gharama za riba za mikopo hutegemea
zaidi gharama za upatikanaji wa fedha pamoja na gharama za uendeshaji.
Pia
amesema kuwa, ni muhimu kutambua kwamba kadri riba za mikopo zinapokuwa
juu, ndivyo riba za amana zinapokuwa juu pia, ambapo wastani wa riba za
kukopa kwa mwaka mmoja mwezi Juni, 2016 ulikuwa asilimia 13.67 wakati
wastani wa riba za amana za mwaka mmoja ulikuwa asilimia 11.52 ikiwa ni
tofauti ya asilimia 2.25.
COMMENTS