Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO. Tanzania Girl Guides Association (TGGA) wanategemea kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa chama hicho kwa...
Na Jacquiline Mrisho
– MAELEZO.
Tanzania Girl Guides
Association (TGGA) wanategemea kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa chama hicho kwa
njia ya kufanya shughuli mbalimbali za kuisaidia jamii.
Maadhimisho hayo yanayojulikana
kama ‘thinking day’ yatafanyika Februari 22 mwaka huu ambapo shughuli za
kuisaidia jamii zitaanza Februari 10 mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Makao Makuu wa Chama hicho, Rosaldina Majuva
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo.
Bi. Rosaldina amesema
kuwa siku ya maadhimisho ya chama hicho inaambatana na siku ya kumbukumbu ya
kuzaliwa kwa waasisi wao akiwemo Lord Baden Powell ambaye alikuwa kiongozi wa Boy
Scout pamoja na Kamishna Mkuu wa Girl Guides na Girl Scouts, Lady Olave Baden
Powell (mkewe).
“Tumepanga
kuadhimisha siku hii muhimu kwa kufanya shughuli za kijamii zikiwemo za kutoa
misaada kwa wahitaji, kutunza mazingira kwa kufanya usafi katika eneo la Coco
Beach na Magomeni na kupanda miti, kutoa elimu ya kujithamini, kujitambua na
kukataza unyanyasaji pamoja na kutembelea kituo cha wazee wa Kigamboni,”alisema
Bi. Rosaldina.
Kwa upande wake Katibu
wa chama hicho, Grace Shaba amefafanua kuwa chama hicho kimelenga kupanua
uelewa wa wanawake kwa ujumla kuhusu uzalendo, majukumu ya nchi yao, kujenga
ushirikiano wa kitaifa na kimataifa kupitia kambi za mafunzo, kutembelea na
kuwasiliana kwa njia za teknohama pamoja na kuwa tayari kufanya kazi kwa
manufaa yao na ya Taifa.
“Dira yetu ni kuwa na
jamii yenye wasichana na wanawake waliowezeshwa kufikia uwezo wa juu kabisa
katika kutimiza malengo yao na kuwa rasilimali bora ya Taifa,”alisema Bi. Grace.
Nae Kamishna Mkuu wa
Tanzania Girl Guides Association, Symphorosa Hangi amesisitiza wanawake na
watoto wa kike kujiunga na chama hicho kwani kinatoa elimu ya masuala ya
kijamii na kiuchumi yatakayosaidia kuwainua wanawake na watoto pamoja na taifa
kwa ujumla.
Mpaka sasa kwa
Tanzania,chama hicho kipo katika mikoa 22 kikiwa na jumla ya wanachama 101,824.
COMMENTS