Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amewataka wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi kujitathimi...
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amewataka wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi kujitathimini yale waliyoazimia kutekeleza kwa mwaka wa Fedha 2017/18 kama yamefikia lengo ili kuweza kusaidia kuboresha utendaji na kutafutia ufumbuzi masuala ambayo yanakwamisha ufanisi wa kazi na kuwezesha mazingira wezeshi kwa wafanyakazi.
Prof. Mbarawa amesema hayo mkoani Morogoro, wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi ambapo pamoja na mambo mengime amesisitiza umuhimu wa baraza hilo katika kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi wenye tija, staha na upendo.
"Ni matarajio yangu kuwa kila mjumbe kwa nafasi aliyonayo katika baraza hili atatumia fursa hii kutoa michango ya mawazo ili iweze kuwa mwongozo mzuri wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi", amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, ametoa wito kwa wajumbe hao kuhakikisha kuwa Wizara inashiriki kikamilifu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuwajengea watanzania miundombinu bora na imara ili kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda na hivyo kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya kuifanya nchi yetu iwe na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Profesa Mbarawa, amewataka wajumbe hao kujadili kwa kina Rasimu ya Bajeti na Mpango wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2018/19 ili kuweza kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Waziri Prof. Mbarawa, Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema kuwa mabaraza ya wafanyakazi yameanzishwa kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi ya Wizara, Idara na Taasisi za Umma kuhusu usimamizi wa rasilimali watu, utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi na weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
Ameongeza majukumu mengine kuwa ni kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi; kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi; maslahi ya Wanyakazi na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano)
|
COMMENTS