Na Dkt. Hamisi Kigwangalla. Kila siku nashuhudia wananchi wenzangu wakikalamika. Natamani kujibu. Naacha. Natamani kuwakumbush...

Na
Dkt. Hamisi Kigwangalla.
Kila siku nashuhudia wananchi wenzangu wakikalamika. Natamani kujibu.
Naacha. Natamani kuwakumbusha wananchi wenzangu. Naacha. Nasema mbona
sisi ni wepesi kusahau? Natamani kuwakumbusha wabunge wenzangu. Naacha.
Nasema na mimi sasa nipo kwenye Serikali. Ni mtunga sera, ni mfanya
maamuzi, nikisema watasema huyu ni 'Naibu Waziri'. Lakini kiukweli nina
hamu na shauku ya kuzungumza na wananchi wenzangu. Nami nitoe yangu ya
moyoni. Kama mwananchi mwingine yeyote yule tu.
Nina
haki hiyo. Na mimi haki yangu inalindwa na katiba na sheria za nchi
yetu.
Leo nimeona acha nipumue kidogo. Niseme. Niuvue userikali wangu. Niseme
kama mwananchi mwingine yeyote yule. Nianze kwa kuweka wazi kabisa hapa,
kwamba; haya ni yangu. Si ya Serikali.
Serikali ni ya Rais Magufuli, tumempa dhamana, ndiyo. Hili
halibishaniwi. Tumempa kazi, ndiyo.
Hili
pia halibishaniwi. Lakini kazi hii anaifanyaje? Tunazijua changamoto
anazokumbana nazo? Je, ana nia ya kuzitatua? Ni maswali ambayo
yanastahili majibu. Kwenye makala hii nitajaribu kuyafafanua kidogo kwa
mtazamo wangu kadri nitakavyojaaliwa.
Pamoja na kumpa dhamana Rais wetu, ni lazima tufahamu kuwa na sisi tuna
wajibu wa kutimiza kwa Taifa letu.
Tuna
kazi ya kufanya kumsaidia Rais wetu kubeba mzigo wa kuleta mapinduzi ya
kiuchumi na kijamii kwenye Taifa letu. Tusimuachie huu mzigo peke yake.
Tuubebe sote.
Nchi ina changamoto nyingi sana, siyo kwamba Rais ama Serikali yake
haizifahamu ama haina nia ya kuzitatua, ama Rais Magufuli amesinzia, ama
anastarehe; kila siku anahangaika kukuna kichwa, usiku na mchana
kuzitafutia ufumbuzi. Nadhani hili halina ubishani sana kwa mpenda
kweli.
Binafsi,
sina shaka kabisa juu ya uwepo wa nia thabiti ya kuleta mapinduzi.
Sina.
Kwenye biashara ya kujenga nchi changamoto haziishi siku moja. Ukimaliza
moja, nyingine inaibuka, na nyingine zinazaliwa kutokana na majawabu ya
changamoto uliyoitatua.
Juzi juzi hapa nilisema kuhusu mfumo wa afya wa nchi kubwa kama ya
Marekani kuwa na changamoto ya kuwabagua watu maskini na wale wa tabaka
la kati na kwamba unajenga matabaka makubwa sana yanayowanyima fursa
sawa baadhi ya watu kwenye Jamii.
Na
kwamba ObamaCare inajaribu kutoa majibu yanayolenga kuleta usawa kwa
kuwabana wenye kipato cha juu ili kuwahudumia wenye kipato cha chini.
Tayari imeonekana kuwa kuna changamoto za kuwakamua zaidi watu wa daraja
la kati, badala ya wale wa tabaka la juu kama 'design' na muundo wa
awali ulivyolenga, kwa kuwatwisha mzigo wa watu maskini, na kwamba
mpango huu kwa baadaye hautohimilika. Bado wanaendelea kubishana! Juzi
tumeshuhudia Rais Trump amekwama kwenye jaribio la kuurekebisha.
Kazi
ya kutatua changamoto ipo na inaendelea kwenye Taifa kubwa la Marekani
lenye miaka zaidi ya 200 ya demokrasia.
Mfano, tazama changamoto mpya iliyokuja na sera ya CCM kutoa elimu bure
mpaka kidato cha nne. Tamko hili la kisera limeleta changamoto nyingi za
kiutekelezaji. Kwanza, limeleta urahisi kwa familia nyingi kuona hakuna
sababu ya watoto wao, hata mmoja, kukosa elimu hii ya msingi. Wakati
tunapitisha sera hii hatukujua kuwa kuna watoto wengi kiasi hiki
tunachoshuhudia sasa walikuwa wakikosa fursa (missed opportunity) ya
elimu kwa sababu ya vigharama vidogo vidogo.
Tumeondoa
gharama hizi tumekutana na ongezeko kubwa la watoto kuandikishwa shule.
Mlipuko wa wanafunzi kuingia darasa la kwanza kwenye shule za msingi
kwa wingi umezaa changamoto mpya za upungufu wa madawati, vyumba vya
madarasa, idadi ya matundu ya vyoo, idadi ya walimu nk. Wakati
tukumbukeni vizuri kuwa juzi tu hapa Serikali ilikuwa inaajiri walimu
kwa kipaumbele cha juu kabisa kwa miaka mitano mfululizo, ambapo walimu
wote waliohitimu waliajiriwa!
Uchumi
wetu unakua kwa kasi nzuri, kama ni ndege ndiyo inaongeza spidi ili
ipate nguvu ya kupaa; bado uchumi hauna uwezo wa kuhimili mahitaji yetu
'yote' ya matumizi ya kila siku kama tunavyotamani, achilia mbali ya
kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kadri tunavyodiriki kuota
ndoto zetu. Mfano: Kwenye ajira bajeti ya watumishi (wage bill)
inaongezeka kila siku.
Hili
tu ni hitajio kubwa na nyeti sana la uchumi wetu.
Zamani nilipokuwa Mbunge - bila userikali, kilichokuwa kinanikera ni
kwamba, pamoja na changamoto tulizonazo watu wengine walikuwa wanaishi
kama wako peponi na wengine wanaishi kama wako motoni, hawa wa peponi
walifika huko kwa wizi, rushwa, ufisadi, ubadhirifu na matumizi mabaya
ya ofisi za umma, siyo kwa uchapakazi wala ubunifu. Tena bila huruma kwa
waliokuwa wakiishi kama vile wapo motoni. Huku wakiwa na dhamana ya
kuwaondoa motoni wananchi wenzetu waliobaki huko!
Leo
Rais JPM anakosolewa kwa kubana mianya ya rushwa, wizi, ubadhirifu wa
mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka na uchumi wa ujanja ujanja,
mambo ambayo nakumbuka mimi na wenzangu kwenye bunge la 10 tuliyapigia
kelele kwa nguvu sana, tena kwa uzalendo wa hali ya juu na bila hata
kuogopa kuwa tunapowashughulikia hawa ndugu wa peponi tunashusha imani
ya wananchi kwa chama chetu pia.
Sisi tuliamini kwamba hawa ni lazima tushughulike nao. Tuwaondoe ili
kukisafisha Chama. Tulikuwa wachache sana.
Tulipigana
kuwaondoa watu wa aina hiyo na tuliwatoa. Na kwa kiasi kikubwa
tulimkataa mwanaCCM mwenzetu, Ndg. Edward Lowassa, kwa sababu tuliamini
yeye na kundi lake (lilikokuwa kubwa ndani ya CCM) wangeigawana na
kuimaliza nchi yetu. Ilihitaji uwe mwendawazimu kumkataa ndugu huyu.
Lakini tulikita mguu waziwazi na kumkataa.
Tulionekana wasaliti wenye kustahili kufukuzwa Chamani.
Na
wengine tukifikia kufukuzwa Chama na baadhi ya viongozi wapuuzi,
wakiamini viongozi wa aina yetu hatukutakiwa, mpaka vikao vya juu
vilipopuuzia ndipo tulipona. Tulifika huku sababu kulikuwa na kundi la
wachache waliokuwa wanafaidika na mfumo uliokuwepo, hivyo waliona sisi
tunachafua maji yao ya kuogelea. Mpaka alipokuja Kanali Kinana na
kutupongeza wabunge wa aina yetu akisema, jitengeni na ushenzi wa baadhi
ya watu wanaochafua taswira ya Serikali ya Chama chetu ndipo
tulipumua.
Kuna
njia mbili tu unaweza kutatua changamoto zinazotukabili nchini kwa
'uhakika'. Nasema kwa uhakika maana ni aibu kubwa kuinjika chungu cha
ugali nyumbani kwako na kuwapa wanao uhakika wa ugali kumbe unategemea
unga wa kuomba ama kuazima toka kwa jirani!
Vipi
akikunyima?
Ukichaguliwa kuwa Rais, una ahadi na dhamana kubwa mabegani mwako, una
hamu na shauku kubwa ya kuanza kuzitekeleza, una ndoto nyingi za kutaka
kuleta mapinduzi kwenye nchi yako kwa heshima kubwa uliyopewa, unataka
kuacha alama isiyofutika!
Unachungulia hazina unakutana na madeni, mahitaji, utaratibu na
masharti; unatazama makusanyo uliyonayo. Unachoka kabisa! Nguvu
zinakuisha kabisa.
Hamasa
yako inavurugwa na uhalisia.
Unakumbuka ushauri wa wabunge kila siku bungeni - 'tubane
matumizi...tukate matumizi yasiyo ya lazima...tuweke kodi
hii...ile...Serikali ni dhaifu kwenye kukusanya kodi....tutanue wigo wa
kodi....kwa nini Tanzania na utajiri wote huu bado tunategemea misaada
kutoka nje kwenye bajeti yetu - mwishowe tutapewa pesa zenye masharti
magumu (mambo ya ushoga nk)...tuanzishe mahakama maalum ya mafisadi,
nk!'
Unaanza kutekeleza yote haya kama yalivyo - unalaumiwa!
Tusiwe
wepesi wa kusahau. Tusiwe wanafiki. Ni nani hakuwahi kukerwa na
watumishi hewa? Ni nani hakukerwa na safari za nje? Ni nani alilalamika
kuhusu uwepo wa uwiano wa bajeti ya matumizi ya kawaida mkubwa kuliko
bajeti ya maendeleo? Rais Magufuli toka aingie madarakani, haya ndiyo
maswali anayojaribu kuyapatia majawabu.
Njia za kupata fedha za kutatua changamoto kwa uhakika ni hizi mbili:
moja - ubane matumizi, ili unacho-save ukipeleke kwingine kikasaidie
kupunguza changamoto zako. Ndicho anachokifanya Rais Magufuli kila siku
toka amechaguliwa. Sisi wenye macho ya kizalendo na kiuhalisia tunaona
jitihada zake.
Mbili, ukusanye zaidi na ubane mianya ya kuvuja kwa mapato.
Ndicho
kinachofanyika. Kwa mwaka unaoisha makusanyo ya mapato ya Serikali
yamepita malengo.
Kuna njia nyingine za kupata fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji yetu.
Japokuwa haina washabiki wengi na inapigwa vita sana na watunga sheria
na wanaharakati mara nyingi. Hii ni ile ya misaada kutoka kwa wafadhili
na mikopo (ya ndani na nje). Hizi njia mbili zote zinapigiwa kelele sana
sababu; Moja, kwamba itasababisha tupewe pesa zenye masharti magumu
tusiyoyaweza, na nyingine, kwamba deni letu linakua sana - mwisho
halitohimilika! Njia ya mikopo ya ndani wanasema inaumiza uchumi wetu
nk.
Kwa
sasa tunachotakiwa kufanya ni kuongeza uzalishaji ili wigo wa serikali
kukusanya kipato chake utanuke zaidi. Na hili si la Rais peke yake, ni
letu sote. Kila mtu awe mzalishaji. Shime twende shambani, twende
viwandani, twende sokoni!
Kwangu mimi, kama hali inakuwa ngumu kwetu sote na iwe tu, ili mradi
wasiwepo kati yetu wanaofaidika na serikali ya watu huku wengine hawana
chakula, hawana dawa, hawana madawati nk. Napenda usawa, haki na
uwajibikaji. Namuunga mkono Rais wangu kwa sababu analeta usawa kwa watu
wetu. Nasimama na Rais wangu.
Kwangu hili la usawa, haki na uwajibikaji kwa wote ni kubwa sana.
Linagusa
historia ya machozi, jasho na damu ya makuzi yenye maumivu makali na
furaha nyakati nyingine kipindi cha makuzi yangu na watoto wengine wa
maskini kwenye Tanzania ya miaka ya 70 na 80. Maana mimi ni zao la mfumo
uliotoa haki na usawa kwa wote. Bila Tanzania hiyo mtoto wa maskini
kama mimi, hata ningekuwa na bidii na kipaji cha namna gani,
nisingefikia kusoma mpaka kuwa Daktari, na hata kufikia kutamani
kugombea nafasi ya ubunge. Sitaki kufikiri labda ningekuwa wapi mimi
leo!
Tufanye kazi kwa bidii na maarifa, zama zimebadilika.
Hakuna
mtu atakayethubutu kutuibia kwenye zama hizi. Walau hili ni la uhakika.
Na zile kesi za rushwa, wizi wa mali ya umma, matumizi mabaya ya ofisi
na ubadhirifu wa mali ya umma sasa zifike kwenye mahakama yake na kesi
zikimbie ili tuone haki ikitendeka.
Huwezi kupanda mchicha ukasubiria ukuwe kwa matarajio ya kuvuna bangi.
Tulimpa kura zetu Ndg. Magufuli, mwenye rekodi ya uchapakazi, uaminifu
na uadilifu, basi tutarajie uchapakazi, uaminifu na uadilifu; mwenye
rekodi ya kuacha alama ya kazi yake, basi ni lazima tutarajie kuona kazi
itakayoacha alama. Si vinginevyo.
Tungempa mla rushwa, tungeshuhudia rushwa. Tumevuna tulichopanda.
Tumevuna kazi tu. Tutulie tuone kazi.
Tuamke tufanye kazi. Tushiriki kujenga Tanzania Tuitakayo.
_____________
Imeandikwa na Dkt. Kigwangalla. Mwandishi ni Mwanafalsafa aliyegeuka kuwa Daktari, Mjasiriamali, Mwanasiasa na Mtunga Sera.
COMMENTS