Na Juma Farid, Zanzibar. WAZAZI na walezi nchini wameshauriwa kuwahimiza watoto wao kusoma kwa bidii elimu ya dini ya kiislamu il...
WAZAZI na walezi nchini wameshauriwa
kuwahimiza watoto wao kusoma kwa bidii elimu ya dini ya kiislamu ili kuandaa viongozi bora wa baadae watakaosimamia kwa uadilifu misingi imara ya dini hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Jimbo la
Donge, Dkt. Khalid Salum Mohamed wakati akizungumza katika mashindano ya
kuhifadhi Quran yaliyoandaliwa na Jumuiya
ya kuhifadhisha Kanda ya Donge yaliyofanyika Donge Kitaruni katika Madrasa ya
Twalibina Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja.
Ostadh Idd Shekha Makame kwa niaba ya Mwakilishi wa jimbo la Donge Dkt. Khalid Salum Mohamed akikabidhi misahafu 140 kwa Amir wa jumuiya ya kuhifadhisha Quran Kanda ya Donge, Wakanda Haji Kombo. |
Mwanafunzi Juma Kassim Choum akikabidhiwa zawadi ya msahafu baada ya kuhifadhi juzuu tano na kushinda kwa Alama 85. |
Alisema elimu ndio urithi wa kudumu na wenye
manufaa kwa watoto wa jinsia zote kwani wanakuwa na misingi ya maadili mema na kuepuka mambo
maovu.
Pia Dkt. Salum ambaye pia ni Waziri wa Fedha
na Mipango Zanzibar, aliwasihi wazazi, walimu na viongozi wa madrasa za Wilaya
hiyo kukaa pamoja na kupanga mikakati ya kudumu ya kuthibiti tatizo la
wanafunzi wa kiume wanaoacha mapema masomo ya kidini hiyo bila sababu za
msingi.
Akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi huyo, Ostadh
Idd Shekha Makame alieleza kwamba waumini wa dini hiyo wanatakiwa kuwa wamoja
na wenye kuamrishana mema na kukatazana mabaya wakati wote na sio katika
kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani pekee.
“Elimu ndio nyenzo pekee ya kuleta maendeleo
ya kudumu kwa mwanadamu yeyote na jamii yetu itapiga hatua za kimaendeleo kwa
haraka kama vijana wetu tutakuwa tumewarithisha rasilimali hiyo.”, alisema
Ostadh Shekha kwa niaba ya Dkt. Salum.
Hata hivyo
Ostadh Shekha alitoa wito kwa madrasa zilizoshiriki katika masindano
hayo kwamba licha ya kutoa elimu ya dini wanatakiwa kuanzisha miradi ya
maendeleo itakayozalisha kipato kitakachosaidia kutatua baadhi ya changamoto
zinazowakabili.
Pamoja na hayo Dkt. Salum alitoa zawadi ya
misahafu 140 na magunia manne ya Tende kwa vyuo vilivyoshiriki mashindano hayo.
Naye Katibu wa jumuiya hiyo, Haji Ali Makame alizitaja
changamoto zinazowakabili katika jumuiya hiyo kuwa ni kushuka kwa kiwango cha
uelewa wa masuala ya dini kutokana na kuwepo kwa tabia za baadhi ya waumini
kuiga utamaduni za kigeni.
Mashindano hayo yameshirikisha wanafunzi 97
kutoka vyuo vya Madrasa 10 za Mkoa wa Kaskazini Unguja waliosoma quran
kuanzia juzuu ya Pili hadi 17 ambapo washindi wa mashindano hayo wamepokea
zawadi mbali mbali.
COMMENTS