Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Open...
Madaktari
bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Open Heart International ya nchini
Australia (OHI) wakifanya upasuaji wa kuziba matundu ya moyo kwa mgonjwa wakati
wa kambi maalum ya matibabu ya moyo inayoendelea katika Taasisi hiyo. Tangu
kuanza kwa kambi hiyo tarehe 12/03/2017 hadi leo tarehe 14/03/2017 jumla ya
wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji kati ya hao watoto ni tisa na watu wazima
wawili. (PICHA NA ANNA NKINDA-JKCI).
NA ANNA NKINDA - JKCI
JUMLA ya wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi
maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ushirikiana na madaktari
wenzao wa Taasisi ya Open Heart International ya nchini Australia.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo ambaye pia ni
Daktari bingwa wa upasuaji wa Moyo Bashir Nyangasa, (wakwanza kushoto pichani
juu), wakati akielezea jinsi kambi hiyo ya upasuaji inavyoendelea kutoa
matibabu kwa wagonjwa.
Dkt. Nyangasa alisema, “Kwa kushirikiana na washirika wetu wa OHI
tulianza kambi maalum ya upasuaji kuanzia tarehe 10/03/2017 hadi leo
tarehe 17/3/2017 tumefanya upasuaji kwa wagonjwa 11 ambao
wanaendelea vizuri, kati ya hao watoto ni tisa na watu wazima ni
wawili”,.
Dkt. Nyangasa alisema katika kambi hiyo ambayo
inamalizika tarehe 17/3/2017 walipanga kufanya upasuaji kwa wagonjwa 25 kati ya
hao watoto ni 15 na watu wazima ni 10.
Kuhusu uhitaji wa damu kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa
Moyo Dkt. Nyangasa alisema wagonjwa hao wanahitaji damu nyingi hivyo basi
aliwaomba wananchi wajitokeze
kuchangia damu ambayo itatumika kwa wagonjwa.
“Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu na uchangiaji huu wa damu
usifanyike mara moja bali uwe endelevu kwani Taasisi inatoa
huduma kwa wagonjwa wakati wote siyo wakati wa kambi maalum za matibabu ya moyo
pekee yake”, alisisitiza Dkt. Nyangasa.
Tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2017 JKCI kwa kushirikiana na
baadhi ya washirika wake wa nje ya nchi ambao ni Madaktari Afrika
wa Marekani, Hospitali za Apolo Bangalore na BLK zote za nchini India
na Open Heart International ya Australia wamefanya matibabu ya moyo ya
kufungua na bila kufungua kifua kwa wagonjwa wa moyo wanaotibiwa katika Taasisi
hiyo.
COMMENTS