Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uvuvi kutoka Nchini China Bwana Lan Ping Yong kushoto akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar...


Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuimarisha Sekta ya Uvuvi katika azma
yake ya kujenga uchumi imara unaojitegemea utakaostawisha maisha ya
Wananchi wake.
Alisema
uimarishaji huo utaelekezwa zaidi katika ujenzi wa Viwanda Vidogo
vidogovya usindikaji wa mazao ya Baharini utakaotoa fursa ya kukaribisha
Makampuni na Taasisi za Kimataifa kuwekeza miradi yao Visiwani
Zanzibar.
Balozi
Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa
Viongozi wa Kampuni ya Uvuvi ya Hong Dong kutoka Nchini China ukiongozwa
na Mkurugenzi Mkuu wake Bwana Lan Ping Yong hapo Ofisini kwake Majengo
ya Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema
Sekta ya Uvuvi bado ina rasilmali ya kutosha inayoweza kusaidia uchumi
wa Taifa unaokwenda sambamba na fursa za upatikanaji wa ajira
zitakazosaidia kupunguza ukali wa maisha ya Wananchi walio wengi
Nchini.
“ Hii ni njia bora na mwafaka ya upatikanaji wa ajira hasa kwa Vijana ”. Alisema Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza ujumbe wa Viongozi wa Kampuni
hiyo ya Hong Dong ambao amewahi kukutana nao wakati wa ziara yake ya
Kiserikali ya hivi karibuni Nchini China kwamba juhudi zitafanywa na
Serikali katika kuona azma ya Kampuni hiyo ya kutaka kuwekeza Zanzibar
inafanikiwa.
Balozi
Seif alimuahidi Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya Hong Dong na Ujumbe
wake kuwa pande zinazohusika nchini zitakutana na kuangalia wazo la
Kampuni hiyo la uwekezaji kwa lengo la kuchukuliwa hatua za muelekeo wa
uanzishwaji wa uwekezaji huo.
Mapema
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uvuvi ya Hong Dong ya Nchini China Bwana
Lan Ping Yong alisema mradi wa Uvuvi unaotaka kuwekezwa Visiwani
Zanzibar utakuwa na uwezo wa kutoa fursa za ajira zisizopungua elfu
1,700.
Bwana
Ping alisema licha ya nafasi za ajira zikilengwa kwa Wazalendo lakini
pia utaambatana na wataalamu wa Kampuni ya Hong Dong kutoa mafunzo ya
Uvuvi kwa Wavuvi wa Kienyeji ili waendeshe miradi yao katika Mfumo wa
Kisasa unaokubalika Kimataifa.
Bwana
Ping alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba yapo mafanikio
makubwa yaliyokwisha patikana katika Nchi ya Mauritania iliyoko
Magharibi ya Bara la Afrika baada ya Kampuni hiyo kuwekeza Mradi wa
Uvuvi Nchini humo.
Alisema
mapato ya Wavuvi wadogo wadogo wa Nchi hiyo waliobahatika kuwemo kwenye
mradi huo kwa sasa yameongezeka na kuleta ustawi wa familia zao na
Taifa lao kwa ujumla.
Mkurugenzi
huyo wa Kampuni ya Hong Dong alisema Taasisi hiyo imetenga nafasi Tatu
kwa ajili ya Watendaji wa Sekta ya Uvuvi Zanzibar kwenda Nchini
Mauritania kujifunza hatua iliyofikia ya Uwekezaji wa Kampuni hiyo
katika Nyanja ya Uvuvi.
Wakati
huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alikutana na Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar Bwana J. C. Barupal
Ofisini kwake katika Majengo ya Baraza la Wawakilishi Mbweni Wilaya ya
Magharibi “B”.
Katika
mazungumzo yao Balozi Seif alisema Nchi ya India iliyopo Bara ya Asia
imeshapiga hatua kubwa katika masuala ya Teknolojia ya kisasa ambayo
Zanzibar kama Nchi inayoendelea inaweza kujifunza kwa kina Taaluma hiyo
kutoka kwa Walaalamu wa India.
Balozi
Seif alimueleza Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar kwamba Makampuni
ya India yana uwezo wa kuanzisha miradi yao katika sekta za Kilimo,
Biashara na Viwanda Visiwani Zanzibar ili kuitikia wito wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya kukaribisha Vitega uchumi vya miradi tofauti
Nchini.
Naye
kwa upande wake Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar Bwana J.C.
Barupal alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba India
itaendelea kuunga mkono harakati za maendeleo ya Zanzibar.
Bwana
Barupal alisema uungaji mkono huo umekuja kufuatia mafungamano ya muda
mrefu yaliyopo ya Ushirikiano wa Kihistoaria kati ya pande hizo mbili
hasa katika masuala ya Kibiashara yaliyotoa fursa kwa wafanyabaishara wa
India kuingiza bidhaa zao Visiwani Zanzibar karne nyingi zilizopita
nyuma.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
COMMENTS