Na Anitha Jonas – MAELEZO 25/02/2016 Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaas...
Na Anitha Jonas – MAELEZO
25/02/2016
Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Kassim Majaliwa amewaasa Mawaziri na Manaibu Waziri kuzingatia
sheria ya Maadili kwa Viongozi wa Utumishi wa Umma kwani maadili ni
nyenzo kubwa katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo
Ikulu jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua semina ya Maadili kwa Mawaziri
na Manaibu Waziri inayolenga kuwajengea uwezo mkubwa yanamna kiongozi wa
utumishi wa umma anavyotakiwa kutekeleza majukumu yake bila kukiuka maadili.
“Chimbuko la Maadili ya Utumishi wa
Umma ulianza tangu siku nyingi na umekuwa ukitajwa katika sehemu mbalimbali
ikiwemo katika Katiba ya nchi ya mwaka 1977, Sheria za Utumishi wa Umma pamoja
na Kanuni za Utumishiwa Umma,”alisemaMajaliwa.
Akiendelea kuzungumza katika Semina
hiyo WaziriMkuu alisisitiza kuwa Semina hiyo siyo semina elekezi kwa viongozi
hao kama jinsi imekuwa ikijadiliwa katika mitandao ya kijamii, bali ni semina
inayolenga kutoa mwongozo wa maadili ya viongozi wa umma na utekelezaji wa Hati
ya Ahadi ya Uadilifu na mada katika semina hiyo zitahusu masuala ya maadili
tuu.
Kwa upande wa Kamishna wa Maadili Jaji
Mstaafu Salome Kaganda kutoka Ofisi ya Rais Sekretariati ya Maadili ya Viongozi
wa Utumishi wa Umma amesema semina ya maaadili kwa viongozi ni jukumu la
Sekretariati ya maadili kuandaa kwani hiyo ni sehemu ya majukumu ya Ofisi ya
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Utumishi wa Umma na wao ndiyo wenye
wajibu wakuhakikisha viongozi wa utumishi wa umma wanazingatia maadili.
“Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi
wa Utumishi wa Umma inamamlaka ya kufanya uchunguzi kwa kiongozi yoyote wa umma
atakayesikika kukiuka maadili kama kiapo cha ahadi za uadilifu
kinavyosema,”alisema Jaji Mstaafu Salome.
Aidha Kamishna wa Maadili huyo
aliendelea kusema Ofisi ya Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Utumishi wa
Umma inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya rasimali fedha ambapo
wanazaidi ya miaka mitatu wameshindwa kufanya uhakiki wa mali za viongozi
pamoja na uchunguzi kutokana na changamoto hiyo.
Semina hiyo imeandaliwa na Ofisi ya
Rais Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Utumishi wa Umma kwa kushirikiana
na Ubalozi wa Marekani na Shirika la USAID.
COMMENTS