05 JUNI 2018 TAARIFA KWA UMMA Ufafanuzi kukosekana kwa huduma ya tiketi za kielektroniki kwenye baadhi ya vituo vya mabasi ya Mw...
05 JUNI 2018

TAARIFA KWA UMMA
Ufafanuzi kukosekana kwa huduma ya tiketi za kielektroniki kwenye baadhi ya vituo vya mabasi ya Mwendokasi kwa kipindi cha tarehe 3 na 4 Juni 2018.
Ni kweli kumekuwa na upungufu wa watoa huduma (Wakatisha tiketi) katika baadhi ya vituo vya mabasi ya Mwendokasa kwa siku tajwa hapo Juu. Jambo hili lilisababishwa na kampuni ya UDA-RT ambayo mbia wake mkubwa ni Simon Group inayomilikiwa na Bw. Robert Kisena, kukaidi kuwalipa mishahara watendaji hawa kwa kipindi kirefu.
Itakumbukwa kwamba Mnamo tarehe 24 Aprili 2018 kampuni ya Maxcom Africa PLC ilieleza Umma wa Watanzania kwamba kumekuwa na hali ya sintofahamu katika uendeshaji wa huduma za ukatishaji wa tiketi za kielektroniki na ukusanyaji wa Mapato katika vituo vya mabasi haya ya mwendokasi baada ya kuvamiwa na UDA-RT tarehe 13 Aprili 2018 na kuanza kutumia Tiketi za vishina.
Ikumbukwe tangu February 2017 Maxcom Africa PLC imekua ikiwadai UDA-RT kulipa madeni ya huduma pamoja na stahiki za wakatisha tiketi katika vituo vya mabasi ya Mwendokasi, jambo ambalo lilifika Mahakama kuu katika kesi ya msingi ya madai.
Ila mnamo Tarehe 26 Aprili 2018 Serikali kupitia kwa wakala wa serikali anayesimamia Mradi huu wa Mabasi ya yaendayo haraka (DART Agency) waliunda kamati maalumu za kuishauri DART Agency namna bora la kushughulikia swala la madeni baina ya UDA-RT(mdaiwa) na Maxcom Africa PLC(mdai), ili kunusuru hasara na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kutokea. Kamati zilianza kukutana tarehe 27 Aprili 2018 chini ya Usimamizi wa DART Agency.
Katika hatua za awali, wakala wa Serikali DART-Agency alitoa maagizo kwa UDA-RT kulipa mishahara kwa wakatisha tiketi hawa kwa wakati na pia kurejesha majukumu yote ya ukatishaji Tiketi pamoja na ukusanyaji fedha kwa kampuni ya Maxcom Africa PLC (Haya yapo kwenye barua ya Tarehe 11 Mei 2018 yenye Kumbu: NA.BA.32/291/01-F/6 kutoka kwa Wakala wa mabasi yaendayo haraka kwenda kwa Mtendaji mkuu wa UDA-RT).
Pamoja na maagizo haya ya Wakala wa Serikali, UDA-RT walikaidi maagizo haya na kuendelea kukusanya fedha japo waliruhusu wakatisha tiketi kuendelea na kazi ya kukatisha tiketi huku Maxcom Africa wakiendelea na Jukumu lao la kuhakikisha tiketi za kielektroniki zinaendelea kupatikana kipindi chote kwani kamati zilizoundwa na serikali zilikuwa bado hazijatoa maazimio yake.
Kwa busara zetu baada ya kuona jitihada za serikali katika kutafuta suluhu ya Jambo hili, Maxcom Africa tuliamua kusimamisha kesi yetu ya madai ili kuipa serikali na kamati za usuluhishi nafasi ya kulichunguza na kulitolea maamuzi ya pamoja jambo hili kama serikali ilivyoelekeza.
Kwa kipindi cha zaidi ya Miezi miwili sasa Tangu serikali iunde kamati na kutoa maagizo mbalimbali kwa wenzetu wa UDA-RT, kampuni ya Maxcom Africa PLC, imeandika barua mbalimbali kwa UDA-RT kuwahimiza kulipa stahiki za wafanyakazi hawa (Wakatisha Tiketi)ili waweze kumudu gharama za maisha, Jambo ambalo halikufanyika kwa zaidi ya miezi 2 kupelekea vijana hawa kushindwa kufika kazini siku ya tarehe 3 na 4 Juni 2018.
Tarehe 4 Juni 2018 Kampuni ya Maxcom Africa PLC tulilazimika kutumia njia mbadala kunusuru tatizo hili kuendelea kuwa kubwa, ikiwamo kuwagharamia wakatisha Tiketi gharama za nauli na fedha kidogo ya kujikimu wakati tunaendelea kutafuta Ufumbuzi wa Tatizo hili.
Tunaishauri kampuni ya UDA-RT kuepuka kuisababishia hasara serikali kwa kubeba abiria bure, kwani chanzo cha haya ni wao wenyewe UDA-RT kutolipa mishahara ya wakatisha tiketi mpaka leo ( tangu mwezi Machi 2018 mpaka sasa).
Kampuni ya UDA-RT imekua na sababu nyingi kila kukicha za kukwepa kuwalipa watoa huduma wake ikiwamo wazabuni wengine na sasa limefikia hatua ya wao kukwepa hata kulipa mishahara ya wafanyakazi, huku wakilalamika kila mara kupata hasara bila kutoa sababu za msingi.
Maxcom Africa PLC tunaamini Wakala wa usimamizi wa mabasi ya Mwendo haraka (DART Agency) ana endelea kupitia mapendekezo ya kamati zilizoundwa na pia anaendelea kutafuta mfumo bora wa usimamizi wa mradi huu na tunaamini atamaliza hayo ndani ya muda mfupi. Hivyo tunatoa rai kwa UDA-RT kuepuka kuendelea kuweka vikwazo katika hili, kuheshimu maazimio ya vikao vilivyokaa baina ya serikali na watoa huduma (UDA-RT na Maxcom) ili kunusuru upetevu wa Mapato ya serikali na usumbufu kwa abiria katika kipindi hichi cha mpito.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma
Maxcom Africa PLC
________________
Bw. Deogratius Lazari

COMMENTS