Na Greyson Mwase, Dar es Salaam Aprili 30, 2018 Leo tarehe 30 Aprili, 2018 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amezindua ripoti ya Nane...
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Aprili 30, 2018
Leo tarehe 30 Aprili, 2018 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amezindua ripoti ya Nane ya ulinganishi wa mapato ya Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi Asilia na Mafuta Tanzania (TEITI) kwa kushirikiana na Mtaalam Mwelekezi, Boas & Associates na MM Attoneys.
Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha wawakilishi kutoka Kamati ya TEITI, Wizara ya Madini, makampuni ya mafuta na gesi, Waziri Kairuki amepongeza Kamati ya TEITI na Sekretarieti kwa mchango wake katika uandaaji wa ripoti hiyo.
Mbali na Pongezi hizo, Kairuki ameiagiza Kamati ya TEITI kuongeza nguvu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa mpana wa umuhimu na wajibu wa TEITI kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na warsha mbalimbali pamoja na vipindi vya redio na televisheni.
Amesisitiza kuwa, kipaumbele kiwekwe kwenye maeneo yaliyozungukwa na shughuli za utafutaji na uzalishaji wa madini, mafuta na gesi asilia na kupata taarifa ndani ya kipindi cha miezi sita.
Awali akielezea ripoti hiyo, Kairuki amesema kuwa ripoti hiyo inahusu tathmini ya mapato ya madini katika kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai, 2015 hadi tarehe 30 Juni, 2016 na kufafanua kuwa jumla ya shilingi 434,627,874,380 zilipokelewa serikalini kutoka kwenye kampuni 55 za madini, mafuta na gesi asilia zilizoshiriki zoezi la ulinganishi.
Hata hiyo amesema taarifa inaonesha kuwa kampuni zililipa kiasi cha shilingi 465,164,747,725 za kitanzania serikalini na kusababisha tofauti kati ya malipo kuwa ni pungufu ya shilingi 30,536,873,345 za kitanzania chini ya kiasi ambacho Serikali imekiri kupokea.
“ Ni lazima tufahamu ni vipi imejitokeza tofauti hii na ninachukua fursa hii kuelekeza taarifa hii kupelekwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajiili ya uchunguzi kama kifungu 18(1) cha Sheria ya TEITI ya mwaka 2015 kinavyotaka,” alisema Waziri Kairuki.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amefafanua kuwa ripoti imeonesha kuwa sekta ya madini imechangia zaidi kwa asilimia 85 na sekta ya mafuta na gesi ikionyesha kuchangia asilimia 15 ya mapato ya Serikali chini ya Sekta ya Madini kwa mwaka 2015/16
Akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya madini, Kairuki amesema kuwa ili kuhakikisha madini yanakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, Serikali imeanza kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.
Ametaja hatua nyingine ambayo ni endelevu kuwa ni kufanya tathmini ya jinsi gani nchi inapata mapato yake kwenye sekta ya madini kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa.
Ameendelea kusema kuwa jukumu linafanywa na taasisi mbalimbali za Serikali lakini TEITI nayo inatekeleza jukumu husika kwa kuhakikisha taarifa za mapato ya madini zinatolewa kwa uwazi kwa wananchi na wadau mbalimbali katika Serikali, Sekta Binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Wakati huo huo akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa mara baada ya ripoti kuzinduliwa na kukabidhiwa kwa Kamati ya TEITI hatua inayofuatia ni kamati ya TEITI kuwasilisha ripoti hiyo kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili achukue hatua kwenye hoja zilizotokana na ripoti hiyo.
Profesa Msanjila amezitaka kampuni nyingine ambazo hazikushiriki katika kipindi cha ukaguzi kujitokeza katika ukaguzi unaofuata ili takwimu halisi za mapato zifahamike.
Aidha, ametumia fursa hiyo kukaribisha kampuni nyingine zenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya madini kujitokeza kwa wingi ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati, waliokaa mbele) Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (wa tatu kutoka kulia waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka Kamati na Sekretarieti ya TEITI mara baada ya kuzindua ripoti hiyo.
COMMENTS