JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU Simu: 255-22-2114512, 2116898 E-mail: press@ikulu.go.tz ...
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 15 Machi, 2018 amefungua kiwanda cha kutengeneza sigara cha Philip Morris Tanzania Limited kilichopo Kingolwira Mkoani Morogoro na kuagiza viongozi wote nchini kuwalinda na kuwavutia wawekezaji.
Pamoja na agizo hilo Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wawekezaji wote wanaojenga viwanda kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha viwanda hivyo vinakuwa na tija ili wakulima waweze kupata masoko ya uhakika ya mazao yao, Watanzania kupata ajira na Serikali kupata kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
“Niwaombe wawekezaji msisite, endeleeni kujenga viwanda vya kutosha katika nchi hii, niwaombe viongozi na watendaji wenzangu katika Serikali kuanzia Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa wilaya mpaka Wakurugenzi mtengeneze mazingira mazuri ya kusaidia wawekezaji kuwekeza, sisi viongozi ndani ya Serikali kamwe tusije kuwa chanzo cha kuzuia wawekezaji kuwekeza” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Philip Morris Tanzania Limited kwa uwekezaji wa kiwanda hicho uliogharimu Shilingi Bilioni 65 na kampuni ya Mansoor Industries Limited kwa uendeshaji wa kiwanda.
Meneja Mkuu wa kampuni ya Philip Morris Tanzania Bi. Dagmara Piasecka amesema uamuzi wa kampuni hiyo kuwekeza hapa nchini ni uthibitisho wa mtazamo na imani ya muda mrefu iliyonayo kwa Tanzania kutokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya biashara, amani na utulivu, ukuaji mzuri wa uchumi na sera nzuri ya viwanda inayosimamiwa vizuri na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mansoor Industries Limited Mhe. Mansoor Shanif Hirani amesema kiwanda hicho kilichoanza kujengwa mwaka 2017 kina uwezo wa kutengeneza sigara Milioni 400 na kulipa kodi kiasi cha Shilingi Bilioni 12 kwa mwaka, kimetoa ajira kwa watu 224 na kitaingiza fedha za kigeni kwa kuuza sigara ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe amesema mkoa huo wenye viwanda zaidi ya 3,000 unaendelea na kampeni kubwa ya ujenzi wa viwanda vingine 300 katika mwaka huu.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa ujenzi wa viwanda unaendelea vizuri katika nchi nzima na amebainisha kuwa vipo viwanda vingi vilivyokamilika na vimeanza uzalishaji.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amejibu ombi la kupatiwa maji lililotolewa na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe. Aziz Abood kwa kumhakikishia kuwa Serikali itafanyia kazi tatizo la uhaba wa maji kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Morogoro na maendeleo ya viwanda.
Katika mkutano huo Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero ya wafanyabiashara ndogondogo kunyang’anywa bidhaa zao na Manispaa ya Morogoro kwa madai ya kuendesha shughuli zao katika maeneo yasiyoruhusiwa, na ameiagiza manispaa hiyo kuacha kuwanyanyasa na badala yake waboreshe mazingira yao na kuepusha hatari ya milipuko ya magonjwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Morogoro
15 Machi, 2018
![]() |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia mojawapo ya hatua katika utengenezaji wa Sigara mara baada ya kufungua kiwanda hicho mkoani Morogoro.
|
![]() |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia mojawapo ya vifungashio vya Sigara hizo kiwandani hapo mara baada ya kukifungua.
|
![]() |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe mara baada ya kuzindua kiwanda cha Sigara mkoani Morogoro.
|
![]() |
Msanii mkongwe wa Bongo flavour Selemani Msindi au Afande Selle akitumbuiza katika sherehe za ufunguzi wa kiwanda cha Sigara mkoani Morogoro.
|
COMMENTS