Mkuu wa Kitengo cha Uchumi na Takwimu Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (ACF) Maria Kullaya amepokea msaada wa Kompyuta m...
Mkuu wa Kitengo cha Uchumi na Takwimu Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (ACF) Maria Kullaya amepokea msaada wa Kompyuta mpakato moja na Printa moja kutoka katika Kampuni ya Tanzania Tooku Garment Co.Ltd, kwa ajili ya kuboresha kitengo cha Takwimu cha Jeshi hilo.
Msaada huo wenye thamani ya sh.1.5 million ambao umetolewa na Kampuni ya Tanzania Tooku Garment Co.Ltd umepokelewa mapema leo Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliopo barabara ya Ohio Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akipokea msaada huo Kamishna Msaidizi Maria alisema, msaada huu umetolewa wakati muafaka kwani utasaidia kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi katika ukusanyaji wa taarifa na utunzaji wa kumbukumbu tofauti na hapo awali.
Tunatarajia kuvitumia vifaa hivi kwa lengo mahususi pamoja na kuvitunza vizuri “Vifaa hivi vitakuwa chachu kwa kitengo cha takwimu kwani tulikuwa na uhaba wa vitendea kazi” alisema Kamishna Msaidizi Maria.
Naye Meneja wa Kampuni hiyo Bw. Rigobert Massawe, akizungumza wakati akikabidhi msaada huo, alisema “lengo ni kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutimiza majukumu yake kwa ufanisi kwani kwa kufanya hivyo tunatimiza wajibu wetu wa kurudisha huduma kwa jamii”.
Kamishna Msaidizi Maria anaishukuru kampuni hiyo kwa kuwapa msaada wa vitendea kazi hivyo, pia kupitia nafasi hii naomba wadau wengine waige mfano huu kwa kulisaidia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Nyanja mbalimbali ili liweze kutimiza majukumu yake ya kuokoa Maisha na Mali za Watanzania.
COMMENTS