WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameungana na wanafamilia, wananchi wa Songea katika kuomboleza kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo la Songea,...
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameungana na
wanafamilia, wananchi wa Songea katika kuomboleza kifo cha aliyekuwa mbunge wa
jimbo la Songea, Bw. Leonidas Gama, nyumbani kwa marehemu Likuyu wilayani
Songea.
Bw. Gama amefariki dunia jana (Ijumaa, Novemba 24,
2017) katika Hospitali ya Peramiho
mkoani Ruvuma alikokuwa akipatiwa matibabu. Marehemu anatarajiwa kuzikwa
Jumatatu, Novemba 27, 2017 katika kijiji cha Likuyu wilayani Songea.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu amesema
kifo hicho ni pigo kwa Serikali kwa sababu marehemu alishirikiana nayo vizuri
tangu akiwa mtumishi wa umma na hata baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo
la Songea.
Waziri Mkuu amesema msiba huo umeleta mtikisiko mkubwa kwa
sababu baada ya kurudi nchini kutoka India alikokuwa akipatiwa matibabu
aliwaeleza kuwa hali yake kwa sasa ni nzuri. ”Ametuachia pengo kubwa ambalo
hatuna namna ya kuliziba.”
Ameongeza kuwa alipokea taarifa za msiba huo kwa huzuni na
mshtuko mkubwa kwa sababu siku mbili kabla ya Waziri Mkuu kuanza ziara yake
mkoani Ruvuma, Bw. Gama alimpigia simu na kumjulisha kwamba yeye anatangulia
Songea kumpokea.
“Kifo ni mipango ya Mwenyezi Mungu na kwamba Bw. Gama
ametangulia nasi tutafuata, hivyo wajibu wetu sote ni kumuombea kwa Mwenyezi
Mungu ailaze roho yake mahali pema. Gama alikuwa kiongozi na mwanga wa
maendeleo.”
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaomba wanafamilia,
mke wa marehemu na watoto na wananchi wa jimbo la Songea waendelee kuwa
watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa
wetu.”
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bibi Christine
Mndeme alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutenga muda wake na kwenda kuwafariji
wafiwa licha ya majukumu mengi na makubwa aliyonayo.
Awali msemaji wa familia Bw. Issa Fusi alimshukuru Waziri
Mkuu pamoja na viomgozi mbalimbali waliojitokeza na kuwafariji baada ya kutokea
kwa msiba huo.”Kaka yetu tulimpenda sana kazi ya Mungu haina makosa.”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, NOVEMBA 25, 2017.
COMMENTS