Na Ismail Ngayonga MAELEZO DAR ES SALAAM 25.11.2017 WAFANYABIASHARA na Wajasiriamali Wanawake nchini wametakiwa kuwa na uthubutu...
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
25.11.2017
WAFANYABIASHARA na Wajasiriamali Wanawake nchini wametakiwa kuwa na uthubutu wa kutenda na kufikia malengo waliyojiwekea kwa kutumia fursa zilizopo ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi katika jamii inayowazunguka.
Wito huo huo umetolewa (juzi) Novemba 23, 2017 Jijini Dar es Salaam na Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mwajuma Magwiza wakati wa mkutano wa Jukwaa la Mwanamke Mjasiriamali na Ubunifu liliondaliwa na Taasisi ya Dominion Leadership Connect.
Magwiza alisema Wanawake ndio kundi kubwa katika jamii ya Watanzania na wanapaswa kutambua kuwa hakuna njia ya mkato katika kuyafikia mafanikio yao kiuchumi na badala yake wajihangaishe katika kutatua changamoto zilizopo ili kupata mafanikio katika shughuli mbalimbali za kila ikiwemo biashara na ujasiriamali..
“Serikali imefungua milango ya ushirikiano kwa kuanisha fursa za kujikwamua kiuchumi kwa Wafanyabiashara na Wajasiriamali wanawake, zipo taratibu zilizoanishwa katika kuzifikia fursa hizo na hivyo ni wajibu wetu kuachana na mazoea ya utamaduni ulijiongezeka katika jamii yetu” alisema Magwiza.
Kwa mujibu wa Magwiza alisema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili Wafanyabiashara na Wajasiriamali Wanawake nchini ikiwemo ukosefu wa mtaji ya biasharara, ambapo hata hivyo halmashauri mbalimbali nchini zimeanza kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kutenga asilimia 5 ya bajeti zao kwa ajili ya kusaidia vikundi vya Wanawake na Vijana.
Aidha Magwiza aliwataka Wafanyabiashara na Wajasiriamali Wanawake kutambua kuwa mtaji sio kigezo cha kukwama katika kujiletea maendeleo yao na badala yake watumie majukwaa yao kuwa chachu ya mabadiliko ya kifikra na hatimaye kufikia malengo waliyojiwekea.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya GIBR FARM, Hadija Jabir alisema safari ya mabadiliko ya kiuchumi kwa Wafanyabiashara na Wajasiriamali Wanawake nchini itapata mafanikio makubwa iwapo jamii hiyo itaunganisha nguvu ya pamoja katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowazunguka.
Aliongeza kuwa ili mafanikio hayo yaweze kupatikana ni wajibu wa Wafanyabiashara na Wajasiriamali Wanawake walielezane ukweli na uwazi uliopo katika kubaini fursa na kutumia rasilimali zilizopo ili ziweze kuwaletea maendeleo ya haraka.
“Safari ya kujikwamua kiuchumi huwa ngumu katika ngazi za awali, kwa upande wetu kampuni ya GIBR FARM inayojihusisha na uzalishaji wa mbogamboga na matunda, tumefanikiwa kupanua wigo wa soko na sasa tunauza bidhaa zetu katika nchi za Sweden, Italy na Ujerumani” alisema Hadija.
Naye Mwanzilishi wa Kampuni ya uzalishaji kuku ya GOKUKUZ, Bulla Boma alisema kumekuwepo na changamoto ya fursa za masoko katika mauzo ya bidhaa kwa Wafanyabiashara na Wajasiriamali Wanawake hususani waliopo katika mfumo usio rasmi, hatua inayowafanya wengi wao kukatishwa tamaa wakiwa katika ngazi za awali.
Hata hivyo alisema kutokana na kupanua wigo wa ushirikano na mawasiliano na Wafanyabishara na Wajasiriamali wakubwa waliopo nchini, kampuni yake kwa sasa imejiwekea malengo ya kupanua wigo wa bidhaa hiyo katika soko la kimataifa.
Kongamano hilo lilibeba kauli mbiu ya “Mwanamke Mjasiriamali na Ubunifu” lililenga katika kuhamasisha Wafanyabiashara na Wajasiriamali wanawake nchini kuibua na kutumia fursa za kiuchumi ili kuweza kuwaletea maendeleo yao katika jamii.
COMMENTS