Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesema itahakikisha inapata hati za viwanja vyake vya ndege ili kupunguz...
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA), imesema itahakikisha inapata hati za viwanja vyake vya ndege ili
kupunguza uvamizi kutoka kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw.
Richard Mayongela alitoa kauli hiyo leo
kwenye mkutano na wafanyakazi uliofanyika katika ukumbi ya Transit uliopo jengo
la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI),
ikiwa ni moja ya mikakati ya mamlaka hadi kufikia Juni 2018.
Bw. Mayongela alisema tayari wameanza
taratibu za kupata hati miliki kwa viwanja 13, vikiwemo vya JNIA na Mwanza
zilizofutwa awali.
Hata hivyo, Wananchi wamekuwa na
tabia za kuvamia maeneo ya viwanja vya ndege kwa kufanya makazi na mashamba,
jambo ambalo ni hatarishi kiusalama.
Bw. Mayongela alisema mkakati
mwingine ni kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuimarisha
ulinzi kwenye maeneo ya viwanja vya ndege 58 vinavyomilikiwa na serikali na
ambavyo havipo chini ya serikali.
“Pia tutaanda kikosi kazi
kitachosaidiana na wenzetu wa TANROADS katika usimamizi na uangalizi wa viwanja
vya ndege vinavyoendelea kujengwa maeneo
mbalimbali nchini,” alisema Bw. Mayongela.
Katika hatua nyingine Bw. Mayongela
alisema pia mamlaka inampango wa kuendeleza miundombinu mbalimbali yakiwemo
majengo ya abiria, Mizigo, ufungaji wa taa za kuongezea ndege na ufungaji
kamera za usalama (CCTV) kwenye viwanja vya Arusha, Mwanza, JNIA na Dodoma.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali
Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias aliwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa
uweledi na uwazi, ili kufikia malengo yaliyowekwa na hatakuwa tayari kumfukuza mtumishi
kazi kwa masuala yasiyokuwa na msingi.
“Ninafungua milango kwa wafanyakazi
mje ofisini kwangu kwani hii ni ofisi ya rasilimali watu na sio rasilimali mtu,
naweka milango wazi mje tujadili masuala ya kazi ya kujenga na sio majungu,”
alisisitiza Bw. Thobias.
COMMENTS