Na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW Serikali ya Tanzania imedhamiria kuboresha na kulinda ustawi wa watoto wote Tanzania na kupunguza...
Na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
Serikali ya Tanzania imedhamiria kuboresha na kulinda ustawi wa watoto wote Tanzania na kupunguza athari zinazotokana na VVU, umasikini, vifo vya wazazi ulemavu, utelekezaji wa watoto, ndoa, mimba za utotoni na ukatili dhidi ya watoto.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga mjini Dodoma wakati akisaini Mwongozo wa Kitaifa kuhusu Mafunzo ya Usimamizi Jumuishi wa Mashauri ya Watoto kwa Wasimamizi wa Mashauri ya watoto Ngazi ya Jamii.
Katibu Mkuu Sihaba Nkinga amesema kuwa Mwongozo huu una lengo la kutekeleza Mpango wa Taifa wa Pili wa Huduma Kwa Watoto Walio Katika Mazingira Hatarishi (2013-2017) unaolenga kuboresha ustawi na ulinzi wa watoto kwa kulinda haki zao, kuzuia na kupunguza matukio hatarishi na yenye madhara kwa watoto.
“Mwongozo huu utatusaidia kupambana na changamoto zinazowakabili watoto wetu katika kulinda Haki, ustawi na ulinzi wao” alisema Bibi Sihaba.
Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Bw. Rabikira Mushi amesema kuwa wasimamizi wa Mashauri ya Watoto Ngazi ya Jamii watapatiwa mafunzo kuhakikisha mashauri ya dharura yanashughulikiwa haraka na mashauri yote ya ulinzi yanapewa rufaa kwa katika mifumo iliyopo kwa uangalizi wa Afisa Ustawi wa Jamii.
Ameongeza kuwa Mafunzo hayo yanalenga kuwaandaa Wasimamizi wa Mashauri ya Watoto Ngazi ya Jamii kuelewa na kuzingatia ipasavyo hatua za uratibu wa Mashauri ya Watoto kwa kuanzia na utambuzi wa tukio wa mtoto aliyefanyiwa unyanyasaji au ukatili hadi kutoa msaada stahiki kwa Mtoto aliye katika mazingira hatarishi katika jamii zetu.
Mwongozo huu utasaidia kuandaa Mfumo wa Usimamizi Jumuishi wa Kitaifa kuhusu Mashauri ya watoto katika ngazi ya Jamii ambao utawezesha uratibu kwa kuunganisha wasimamizi wa ustawi wa jamii, ulinzi, na kutoa huduma zinazohusiana na maambukizi ya VVU kwa kuunganishwa na Mifumo iliyopo katika ngazi za Serikali za mitaa.
Mwongozo wa Kitaifa kuhusu Mafunzo ya Usimamizi Jumuishi wa Mashauri ya Watoto kwa Wasimamizi wa Mashauri ya watoto Ngazi ya Jamii umeratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na OR-TAMISEMI kwa hisani ya Shirika la USAID/PEPFAR.
COMMENTS