Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amepokea taarifa ya utekelezaji wa agizo alilotoa la kuundwa kwa katiba...
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amepokea taarifa ya utekelezaji wa agizo alilotoa la kuundwa kwa katiba mpya ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya MBOMIPA na kuagiza ifanyiwe marekebisho ya mwisho kabla ya kuwasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya mijadala.
Alipokea taarifa hiyo juzi (Ijumaa, Septemba 29, 2017) katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, mjini Iringa. Aliagiza kuundwa upya katiba hiyo alipofanya ziara ya kikazi kwenye eneo la Jumuiya hiyo katika kijiji cha Tungamalengawilayani Iringa mapema mwezi Agosti mwaka huu.
Kufuatia ziara hiyo pamoja na taarifa ya tume aliyoiunda kuchunguza suala hilo alibaini mapungufu mbalimbali ya kikatiba na kuamua kutoa agizo la kuundwa upya kwa katiba hiyo na kuvunja kabisa bodi ya wadhamini ya jumuiya hiyo. Miongoni mwa mapungufu hayo ni katiba iliyokuwepo awali kukinzana na Sheria mama pamoja na kanuni zake.
Katiba kutoeleza namna ya upatikanaji wa viongozi na namna ya kuwawajibisha, kutoeleza majukumu ya bodi ya wadhamini kwa usahihi na namna ya upatikanaji wa bodi hiyo pamoja na kutoleza wajibu wa wawekezaji katika jumuiya kwa jumuiya yenyewe na kwa Serikali kwa ujumla wake.
Kubwa zaidi ambalo lilisababisha kuvunjwa kwa bodi hiyo ni jumuiya hiyo kujiendesha kwa hasara huku ikiomba fedha kwa wahisani kwa ajili ya kujiendesha wakati kimsingi asasi hiyo ilipaswa kuwa msaada mkubwa kwa wanachama wao ambao ni vijiji vinavyounda Jumuiya hiyo.
Taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo iliwasilishwa kwenye kikao hicho na Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Kissah Mbilla kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo. Taarifa hiyo ilijadiliwa na kutolewa mapendekezo mbalimbali ya kuiboresha.
“Baada ya michango yote hii mizuri tuliyotoa hapa leo, nendeni sasa mkairekebishe vizuri izingatie maeneo yote ya msingi ikiwemo mgawanyo sawa wa mapato, kuzingatiwa kwa maeneo ya mapito ya wanyamapori na idadi ya wanachama ijumuishe vijiji vyote vilivyoanzisha Jumuiya hiyo ili kuepusha migogoro ya baadaye inayoweza kujitokeza” aliagiza Prof. Maghembe.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani ambaye ni alikuwa Mwenyekiti wa Tume iliyoundwa na Waziri Maghembe kuchunguza mgogoro huo wa MBOMIPA, baadhi ya wajumbe wa tume hiyo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Amina Masenza.
Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori MBOMIPA iliundwa mwaka 2007 ikiwa wanachama ambao ni vijiji 21 vilivyopo katika tarafa ya Idodi na Pagawa kwenye halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijini mkoani Iringa. Eneo la jumuiya lina ukubwa wa kilomita za mraba 777 na linapakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Eneo hilo limekuwa likitumika kwa ajili ya shughuli za utalii wa picha, utalii wa uwindaji, utalii wa kiutamaduni na utalii wa kutembea kuangaliwa wanyama. Miongoni mwanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni ndege wa aina mbalimbali, mamba, tembo, nyati, swala na wengineo wengi ambao huingia na kutoka kutokea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
COMMENTS