Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) Dkt. Kijaji: Serikali haijaongeza kodi mpya Na Mwandishi Wetu...
Dkt. Kijaji: Serikali haijaongeza kodi mpya
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amewahakikishia wafanyabiashara wa mkoa wa Mwanza kwamba serikali haijaongeza aina mpya ya kodi isipokuwa imeziba mianya ya ukwepaji kodi ili kuhakikisha kuwa inakusanya kila kodi anayostahili kulipa mfanyabiashara kwa mujibu wa sheria.
"Serikali imefunga mianya ya ukwepaji kodi ili iweze kukusanya kodi stahiki kwa ajili ya kutekeleza huduma za jamii kwa wananchi wake, ambao pia ni miongoni mwa watoto wenu", amesema Dkt Kijaji.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipokutana na wafanyabiashara wa mkoa wa Mwanza ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa yenye lengo la kukutana na wafanyabishara na kuzungumza nao masuala ya ulipaji kodi pamoja na kukumbushana wajibu wa haki za mlipakodi.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji amesema serikali inatumia jumla ya Shilingi 22 bilioni ili watoto wa kitanzania wapate kusoma bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne, hivyo basi, serikali inatoa wito kwa wafanyabiashara wote nchini kuunga mkono juhudi za serikali kwa kulipakod​i kwa mujibu wa sheria ili nchi yetu ipige hatua zaidi ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii.
Aidha, Dkt. Kijaji ameongeza kuwa kodi ni lazima idaiwe na ilipwe na ni wajibu na haki kwa mfanyabiashara kulipa kodi na kuahidi kuwa wizara yake kupitia Mamlaka ya Mapato inaweka mazingira mazuri ya ulipaji kodi kwa kutumia mifumo rahisi isiyosababisha kero miongoni mwa walipakodi.
COMMENTS