Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewatoa hofu wana Singida na watanzania wote kuwa kuelekea kipindi cha mvua barabara kuu zot...
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewatoa hofu wana Singida na watanzania wote kuwa kuelekea kipindi cha mvua barabara kuu zote za kuingia na kutoka Mkoani Singida zinapitika vizuri.
Dkt Nchimbi ameyasema hayo mara baada ya kukagua ukarabati wa barabara ya Malendi Wilayani Iramba ambapo ameridhishwa na ubora wa kazi hiyo huku akimtaka Mkandarasi wa barabara hiyo kuongea muda wa kazi ili kukamilisha matengenezo makubwa kabla ya mvua kubwa kuanza.
Amesema barabara kuu za Kuingia na kutoka Singida ni kiunganishi cha mikoa katika kila upande pamoja na kuiunganisha mikoa hiyo na nchi za jirani kama Rwanda, Burundi na Kongo ambazo hutumia barabara hizo.
Dkt Nchimbi amemtaka mkandarasi Medics Technique Group of Company kuichukulia kwa uzito na thamani ya kimataifa barabara ya Malendi kwa kuwa kutokamilika kwa muda kutawaadhiri watanzania wengi na nchi za jirani kushindwa kusafirisha bidhaa zao kwa wakati.
“Thamani ya barabara hii sio ya ki mkoa, hapa pakiwa na shida watakaoumia sio wana Iramba au Singida pekee, kuna magari yanasafirisha bidhaa kutoka bandarini Dar es Salaam kuelekea nchi za jirani watapata shida pia, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha hapa panapitika kwa usalama”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa kutokana na matarajio ya Mkoa wa Singida kupata mvua za wastani na juu ya wastani mkandarasi huyo aongeze masaa mawili kila siku ili kazi hiyo iishe mapema na ifikapo mwezi Disemba magari yaweze kupita juu ya hiyo barabara.
Dkt Nchimbi amemtaka mkandarasi huyo kutengeza njia ya mchepuo yenye viwango vya juu ili barabara hiyi ipitike wakati wowote na katika hali yoyote ile.
Aidha amezitaka halmashauri kujiandaa kupokea mvua kwa kukagua mabwawa kama yanaweza kupokea maji ya mvua vizuri pamoja na mifereji inayopitisha maji isafishwe mapema ili mvua hizo zisilete madhara bali zisaidie kuifanya Singida kuwa ya Kijani na yenye maji ya kutosha.
Amewaasa wananchi kuandaa mashamba kwa ajili ya kilimo ili wasipishane na kipindi cha kulima, kupanda au palizi bila kusahau kurekebisha makazi yao ili yawe imara kwa kuhimili mvua za aina yoyote.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida Mhandisi Leonard Kapongo amesema mradi wa Malendi unahusisha matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilomita mbili kwa upande wa Singida na mita 500 kwa upande wa Mkoa wa Tabora huku ukigharimu shilingi bilioni tatu.
Mhandisi Kapongo amesema Mkandarasi Medics Technique Group of Company anatarajiwa kukamilisha kazi zote mwezi Machi mwakani kwa kujenga madaraja mawili, makaravati mawili na barabara hiyo kwa kiwango cha lami ijapokua hadi kufikia Disemba barabara hiyo itapitika bila ya lami.
Ameongeza kuwa ana imani kuwa mkandarasi huyo mzawa atakamilisha kazi hiyo kwa uboa unaotakiwa kutokana na ujuzi na vifaa alivyonavyo huku akieleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutafanya barabara zote kuu kuwa katika kiwango cha lami yenye ubora zaidi.
Naye Diwani wa Kata ya Mgongo Mkumbo Wilson ameishukuru serikali kwa kufanya marekebisho katika barabara hiyo ya Malendi kwakuwa imekuwa ni eneo lenye matatizo hasa kipindi cha mvua nyingi.
Wilson amesema kipindi cha mvua hasa miaka miwili iliyopita maji yalikuwa yanajaa na kufunika barabara hiyo hivyo kuhatarisha maisha ya wasafiri na wakazi wa Malendi.
Ameongeza kuwa uharibifu wa mazingira katika mashamba yaliyo jirani na barabara hiyo yameongeza tatizo la kujaa maji eneo hilo kwakuwa mvua zikinyesha maji yanashindwa kuzuiwa mashambani na kujaa barabarani hivyo wataongeza bidii katika kuelimisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira.
Baadhi ya mafundi wakiendelea na ujenzi wa barabara ya Malendi Wilayani Iramba yenye urefu wa kilomita mbili ili iwe na ubora wa juu wa kupitika katika kipindi cha mvua.
|
COMMENTS