JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA BUNGE LA TANZANIA Tele: +255 026 2322761-5 Fax No. +255 026 2324218 E.mail: info@bunge.go.tz...
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIABUNGE LA TANZANIA | ||
Tele: +255 026 2322761-5
Fax No. +255 026 2324218
E.mail: info@bunge.go.tz |
Ofisi ya Bunge
S.L.P. 941
DODOMA |
TAARIFA KWA UMMA
_______
Kwa siku za hivi karibuni imeibuka tabia kwa baaadhi ya Wanasiasa na Wananchi kulishambulia Bunge na Viongozi wake kwa kutoa maelezo potofu kwamba Bunge la Kumi na Moja halina meno, halitekelezi wajibu wake ipasavyo na kwamba Bunge limetekwa na Serikali hivyo linaendeshwa kwa kufuata maelekezo kutoka Serikalini. Aidha, kwa kutumia lugha za kejeli, matusi na uchochezi watu hao wamekuwa wakilikebehi Bunge na Viongozi wake, mathalan kwamba Mhe. Spika anatumia ubabe, ameshindwa kusimamia uhuru na hadhi ya Bunge, hafuati Kanuni na hatendi haki kwa baadhi ya Wabunge.
Gazeti la kila wiki la MwanaHALISI Toleo Namba 409 la Jumatatu, Septemba 18 -24, 2017 nalo limefuata mkondo huo wa kulishambulia Bunge kupitia makala zenye vichwa vya habari kama vile “Risasi yakwama kwenye waleti” (Saed Kubenea), “ Ndugai anatamani aendeshe Bunge Kiimla” (Chris Alan,) “Ndugai Atumia Polisi Kuita Kubenea, Zitto” (Mwandishi Wetu), “Ubabe wa Ndugai si Ujasiri” (Gululi Kashinde) na “Kwa Mwenendo huu Ndugai hatamkaribia Sitta” (Mwananchi, Buguruni Malapa). Makala zote hizo zimejaa upotoshaji kuhusu uendeshaji wa shughuli za Bunge. Makala zote hizi zina maelezo yanayopotosha mwenendo wa shughuli za Bunge na mamlaka aliyonayo Mhe. Spika katika kusimamia shughuli za Bunge.
Ni wazi kuwa upotoshaji huo, kashfa na matusi vinalenga kumshambulia na kumdhalilisha Mhe. Spika na Bunge kwa ujumla pamoja na kumchonganisha Mhe. Spika na Wananchi. Chanzo cha kashfa hizo ni maelezo ya Mhe. Spika aliyoyatoa kwa nyakati tofauti kufafanua utaratibu wa matibabu kwa Wabunge, kauli na vitendo vya baadhi ya Wabunge vinavyovunja Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na utekelezaji wa shughuli za Bunge.
Bunge linachukua fursa hii kufafanua kwamba, Ibara ya 100 na 101 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 imetoa uhuru kwa Wabunge kujadili hoja mbalimbali Bungeni na kufikia uamuzi. Kanuni za Bunge zimeweka utaratibu mahususi wa kuwezesha uamuzi wa wengi kuwa ndio uamuzi ya Bunge. Hivyo, Katiba, Sheria na Kanuni za Bunge hazitoi nafasi kwa chombo kingine chochote kulielekeza Bunge jambo au uamuzi unaopaswa kufikiwa.
Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge (Sura ya 296) inatoa ufafanuzi wa Haki na Kinga za Bunge na Wabunge. Vilevile Sheria hiyo na Kanuni za Kudumu za Bunge vinazuia mtu yeyote kuingilia kinga, uhuru, haki na madaraka ya Bunge na kutoa adhabu kwa wanaokiuka Sheria na Kanuni hizo. Miongoni mwa makatazo hayo ni kusema uongo, kudhalilisha Bunge na kudharau mamlaka ya Mhe. Spika.
Mbunge au Mwananchi anayekiuka misingi ya kinga, uhuru haki na madaraka ya Bunge hufikishwa kwenye Kamati ya Bunge inayosimamia masuala ya maadili ambako mlalamikiwa hutakiwa kupewa Hati ya Wito (Summons). Endapo mlalamikiwa atakataa wito huo, Sheria imeweka utaratibu wa kulitumia Jeshi la Polisi kuhakikisha anafika mbele ya Kamati.
Kumekuwa na upotoshaji kuhusu utaratibu uliotumika katika kuunda Kamati Maalum za Bunge. Mhe. Spika ana mamlaka kuunda Kamati mbalimbali kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa shughuli za Bunge. Kanuni zilizopo zinajitosheleza hivyo hakuna uwezekano wowote wa Mhe. Spika kushinikizwa kupanga Wajumbe wa Kamati. Vilevile Kanuni ya 5 imempa Mhe. Spika mamlaka ya kuamua jambo lolote ambalo halijawekewa utaratibu na Kanuni za Bunge. Moja ya mambo hayo ni uundwaji wa Kamati Maalum za Bunge. Utaratibu huu ndio uliotumiwa na Mhe. Spika kuunda Kamati zilizofanya uchunguzi kuhusu Mfumo wa uchimbaji wa Madini ya Tanzanite na Almasi nchini. Aidha kwa kutumia mamlaka yake chini ya Kanuni ya 5 Mhe. Spika alizielekeza Kamati hizo kuwasilisha kwake Taarifa za uchunguzi huo. Kwa muktadha huo taarifa hizo huwa haziingii Bungeni. Utaratibu huo sio mpya kwani Kamati iliyofanya uchunguzi kuhusu bomba la gesi, kushauri kuhusu vyanzo vipya vya mapato (Chenge 1 & 2) zilitumia utaratibu huo.
Madai kwamba Bunge linaendeshwa kibabe na kwa misingi ya kibaguzi kwa itikadi za vyama pia si sahihi. Kanuni ya 5(4) inatoa fursa kwa Mbunge yeyote asiyeridhishwa na namna Mhe. Spika anavyoendesha Bunge au uamuzi anaoutoa kuwasilisha sababu za kutoridhishwa kwake kwa Katibu wa Bunge ambaye atafanyia kazi kwa mujibu wa Kanuni.
Aidha Kanuni ya 71 inatoa haki kwa raia yeyote ambaye atajisikia kwamba amepata athari hasi kutokana na kauli, maneno au shutuma kutokana na mjadala Bungeni kuwasilisha maelezo yake kwa Mhe. Spika. Kanuni hiyo imetoa haki ya raia huyo kujisafisha dhidi ya kauli hizo.
Aidha, katika kusimamia utaratibu wa majadiliano Bungeni Kanuni za 59 – 68 hutumika. Kanuni hizo zinazuia Wabunge kutoa kauli za uongo, zisizoruhusiwa na zenye kuudhi. Katika kusimamia utekelezaji wa Kanuni hizi walalamikaji hudhania kuwa Mhe. Spika anatumia ubabe.
Kanuni za 74, 75 na 76 zimeweka utaratibu mahsusi kwa ajili ya kudhibiti fujo Bungeni ambapo Kanuni hizo zimempa Mhe. Spika mamlaka ya kuhakikisha kwamba amani na utulivu unakuwepo Bungeni wakati wote wa Vikao vya Bunge. Kwa kutumia mamlaka yake huweza kuwatoa nje Wabunge wanaokiuka Kanuni hizo na vilevile anayo mamlaka ya kumtaka Mpambe wa Bunge kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge na kudhibiti fujo zinapotokea ikiwemo kuwatoa nje ya ukumbi Wabunge wanaosababisha vurugu. Ikumbukwe kwamba, hakuna adhabu yoyote iliyowahi kutolewa kwa Mbunge kinyume cha Sheria na Kanuni.
Kuhusu madai ya kutelekezwa kwa Mhe. Tundu A. Lissu, Bunge linapenda kuukumbusha umma kwamba, Mhe. Spika zaidi ya mara moja alitoa ufafanuzi kuhusiana na jitihada zilizofanywa na Viongozi wa Bunge katika kuhakikisha Mhe. Tundu A. Lissu anapata matibabu. Aidha alielezea kuhusu uamuzi uliofikiwa na Viongozi wa CHADEMA na familia ya Mhe. Tundu A. Lissu kwamba waliona ni busara kumsafirisha Mheshimiwa Lisu kwenda Nairobi nchini Kenya kupata matibabu kwa utaratibu binafsi badala ya utaratibu wa kawaida wa matibabu kwa Wabunge kwa njia ya Bima ya Afya.
Tunapenda kuukumbusha Umma kwamba Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi kinachoendeshwa na Sheria, Kanuni, taratibu zilizowekwa na kuzingatia mila na Katiba, desturi za Mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania. Toka kuanzishwa kwake chombo hiki kimekuwa rafiki kwa wananchi kwa kusikiliza na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili, hivyo wananchi wasikubali kupotoshwa kwa maneno ya baadhi ya watu wenye chuki na nia mbaya dhidi ya Bunge na Viongozi wake. Aidha, ikumbukwe kwamba maneno na vitendo vya dharau, kushusha heshima na kulidhalilisha Bunge ni mambo yasiyokubalika na yanapaswa kupigwa vita na watu wote wanaoitakia mema nchi yetu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano,
Ofisi ya Bunge,
DODOMA.
20 Septemba, 2017
COMMENTS