- Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli S.L.P 2643, DAR ES SALAAM Simu: +255 22 2135747/8; 213...
-
|
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
B/Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz
|
Septemba 5, 2017
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
THBUB yatoa zuio la kusitisha operesheni ya kuwahamisha na kuwachomea wananchi wa Loliondo makazi yao
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) jana (Septemba 4, 2017) ilitoa zuio la muda (interim order) kusitisha operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu wananchi katika maeneo wanayoishi na kuwachomea makazi (maboma) yao huko Loliondo Wilaya ya Ngorongoro ili kulinda haki za pande zote.
Tume imechukua hatua hiyo kwa mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa Ibara ya 130(1) (f) na (h) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 25(1) (d) cha Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (Sura ya 391) ya Sheria za Tanzania.
Hatua hii imefikiwa kufuatia Tume kupokea malalamiko ya wananchi walioathiriwa na zoezi hilo kutoka Tarafa ya Loliondo Wilayani Ngorongoro, ambapo imeanza kufanyia uchunguzi malalamiko hayo.
Kwa mujibu wa taarifa za wananchi hao katika operesheni hiyo iliyoanza Agosti 12, 2017 na inayotekelezwa kwa pamoja na uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro, askari wa wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Jeshi la Polisi wilayani Ngorongoro kumekuwepo na uvunjwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Wananchi hao wanadai kuwa wameondolewa kwa nguvu katika vijiji vyao halali vinavyotambuliwa kisheria, wamechomewa makazi yao moto isivyo halali na kuchukuliwa mifugo yao.
Pamoja na zuio hilo Tume imeziandikia mamlaka husika kuzitaka ziwasilishe kwake nyaraka zote zinazoonesha uhalali wa zoezi la kuwaondoa wananchi kwa kuwachomea makazi yao na kukamata mifugo yao.
Imetolewa na:
(SIGNED)
Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Septemba 5, 2017

COMMENTS