Na Beatrice Lyimo - MAELEZO Hivi karibuni taasisi ya Mpango wa Hiari wa Nchi za Umoja wa Afrika Kujipima kwa Vigezo vya Utawala Bora (A...
Na Beatrice Lyimo - MAELEZO
Hivi karibuni taasisi ya Mpango wa Hiari wa Nchi za Umoja wa Afrika Kujipima kwa Vigezo vya Utawala Bora (APRM) imezindua ripoti ya kwanza ya Utawala Bora nchini ikiwa ni kiashiria kimojawapo cha utekelezaji wa yale yaliyoandaliwa na kielelezo cha utayari wa Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
![]() |
Makamu
wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akionesha ripoti ya APRM nchini hivi karibuni.
|
Kimsingi APRM ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya iliyokuwa Mpango Mpya wa Maendeleo ya Kiuchumi Barani Afrika (NEPAD) ambao uliamini kuwepo kwa maendeleo thabiti kwa utawala bora katika siasa, uchumi na huduma muhimu kwa jamii.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka APRM inasema lengo la uanzishwaji ni kuhimiza utekelezaji wa sera, viwango na mienendo inayaokubalika kitaalamu ili kujenga utengemano wa kisiasa, ukuaji chanya wa uchumi, maendeleo endelevu na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda na hatimaye bara zima kwa ujumla.
Pia kubadilisha uzoefu na kuimarisha mfanikio yaliyofanikiwa hadi sasa na kutambua changamoto zilizopo na kushirikiana kuzigeuza kuwa fursa za maendeleo.
Taarifa hiyo inasema kuwa malengo hayo yanaweza kufikiwa kupitia mchakato wa APRM unaolenga kubaini mianya iliyopo katika kutekeleza utawala bora katika Nyanja hizo muhimu za kutafuta njia za kukabiliana na udhaifu uliopo.
Vilevile malengo hayo yanaendelea kubaki kuwa madhubuti hata baada ya NEPAD kubadilishwa muundo wake kwa kuundwa Taasisi ya kuratibu shughuli zake itakavyokuwa ndani ya AU.
Mpango huo una umuhimu mkubwa kwani unawapa Waafrika fursa ya kujitathmini wenyewe badala ya utamaduni uliozoeleka wa Bara la Afrika kusemewa na watu wa mataifa mengine.
Kwa upande wa Tanzania ilisaini Mkataba wa awali wa Makubaliao (MoU) kwa kujiunga na mchakato wa APRM Mei 2004 na kuadhinishwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano mwaka 2005.
Hata hivyo badae jukumu hilo lilihamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa wizara unganishi kati ya Serikali, APRM Tanzania na Makao makuu ya APRM yayiloko Afrika Kusini.
Mchakato wa APRM unahusisha tathimini ya Utawala Bora inayofanywa na wataalamu wa ndani ya nchi na ule unaofanywa na wataalamu toka nje ya nchi ambapo mchakato ndani ya nchi unahusu utafiti wa maktaba unaolenga kupata takwimu na maelezo mengine juu ya hali halisi ya utawala bora.
Katika hatua hiyo, Tanzania imetajwa kuwa moja ya nchi katika Bara la Afrika inayotekeleza kwa vitendo dhana ya utawala bora, demokrasia, amani na utulivu hali inayochochea ustawi wa wananchi wake na katika Bara la Afrika kwa ujumla.
Akizindua ripoti ya APRM nchini Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anasema kuwa ripoti imeonesha Tanzania imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuboresha maisha ya wananchi wake hasa kwa kutoa kipaumbele katika kutoa huduma bora za afya, maji, elimu na nishati kwa wananchi wake.
“Kwa niaba ya Serikali naahidi kuwa tutaendelea kusaidia mpango huu ili uwe endelevu na kutoa matunda yaliyokusudiwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo,Asasi zisizo za Kiserikali,wananchi na kila mmoja wetu” Anasisitiza Mhe. Suluhu.
Akifafanua juu ya changamoto zilizoainishwa katika ripoti hiyo Mhe. Suluhu anasema kuwa Kwa kuona umuhimu Serikali imeweka mkakati na kuujumuisha katika Dira ya maendeleo ya mwaka 2025 inayolenga kuleta mabadiliko na kukuza uchumi kwa kufanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unategemea viwanda.
Mhe. Suluhu anasema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika kujenga uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha kunakuwa na nishati yakutosha kuchochea ukuaji wa sekta hiyo na kuwepo kwa mpango kazi unaotekelezwa kati ya mwaka 2011-2035 kwa kuzingatia mipango ya muda mfupi,muda wa kati na muda mrefu katika kuhakikisha kuwa kuna upatikanaji wa uhakika wa nishati, kazi inayotekelezwa na Wakala wa Huduma za Umeme Vijijini (REA).
Anaongeza kuwa eneo jingine ni uwezeshaji wanawake kiuchumi, kielimu, kuwapa fursa wanawake kupata mikopo,huduma za afya, elimu na kuwajengea uwezo ili waweze kushiriki kikamilifu katika uzalishaji mali na kujenga uchumi kwa kuondoa changamoto zinazowakabili katika sekta ya ardhi.
Pia anabainisha kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua katika kupambana na vitendo vya rushwa na imekuwa ikiwafikisha mahakamani wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kwa kuunda Taasisi ya kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na kuiimarisha ili iweze kutekeleza majukumu yake vyema.
Hata hivyo APRM inamkakati wa kuongeza nguvu katika kuimarisha mawasiliano ya umma kati ya APRM Tanzania na wadau ili kuwapa taarifa za mara kwa mara kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano ya umma na zinazoweza kuwafikia watanzania wengi na kw haraka.
Mpango wa Hiari wa nchi za Umoja wa Afrika Kujipima kwa vigezo vya utawala bora (APRM) ,ulibuniwa na viongozi wa umoja huo mwaka 2003 kuziwezesha nchi wanachama kujitathmini kwa vigezo vya utawala bora katika maeneo yafuatayo, Demokrasia na Utawala wa kisiasa, Usimamizi wa uchumi, utendaji wa mashirika ya Biashara, maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi.
COMMENTS