Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakandarasi nch...
Na Jacquiline Mrisho -
MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakandarasi nchini kujitathmini,
kurekebisha makosa yao pamoja na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na
Serikali badala ya kuilalamikia kuwa haiwasaidii.
Rais Magufuli
ameyabainisha hayo wakati akiongea na wafanyabiashara wa sekta binafsi katika mkutano
wa 10 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika leo Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
Rais Magufuli amesema
kuwa tenda mbalimbali za ujenzi wa miundombinu zimekuwa zikitolewa na Serikali mara
kwa mara lakini wakandarasi nchini wamekuwa hawazitumii fursa hizo na matokeo
yake zinatolewa kwa wakandarasi kutoka nchi zingine.
“Serikali inatangaza
tenda nyingi za ujenzi wa miundombinu na kwa kiasi kikubwa huwa inawalenga
wakandarasi wa ndani kuliko wanaotoka nje lakini wakandarasi wetu wamekuwa
hawazitumii fursa hizo, Serikali itachoka kuwabeba hivyo wakae wajitathmini,”
alisema Rais Magufuli.
Ameongeza kuwa
wakandarasi wanatakiwa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili waweze kupata
tenda zinazotolewa na Serikali kwa urahisi pia amewataka wawe wazalendo katika
upangaji wa bei za kazi zao.
Akitoa mfano wa kukosa
uzalendo, Rais Magufuli amesema kuwa wakandarasi wa hapa nchini walipoombwa
kutoa bei za ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walitaja kiasi
cha shilingi kati ya bilioni 150 na 200 wakati Wakala wa Majengo (TBA) waliyajenga
kwa bilioni kumi tu.
Aidha, Rais Magufuli
amewapongeza wafanyabiashara wa sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali
katika kujenga uchumi wa viwanda na kuwahakikishia kuwa Serikali iko pamoja nao
katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.
Kwa upande wake Waziri
Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ametoa siku moja kwa taasisi zinazohusika na huduma
za bandari zikiwemo za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango
Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuanza kutoa huduma zao kwa
saa 24.
“Tumeamua kufanya hivyo
ili kurahisisha huduma kwa wafanyabiashara kwani wamekua wakipata shida kwa
kutumia muda mrefu kupata huduma katika bandari yetu, nafikiri njia hiyo
itachochea wafanyabiashara kuwekeza zaidi”, alisema Mhe. Majaliwa
Ametoa rai kwa
wafanyabiashara wa sekta binafsi kuwekeza kwenye kilimo kwani maendeleo ya
ujenzi wa viwanda unategemea malighafi zinazotokana na kilimo.
Aidha Majaliwa alisema
Serikali imekusudia kupanua wigo katika sekta ya kilimo kwa kuleta zana bora za
kilimo, kuendelea kupunguza kodi katika mazao pamoja kuiwezesha Benki ya Kilimo
kuendelea kutoa mikopo kwa wingi.
Nae, Mwenyekiti wa
Taasisi ya Sekta Binafsi, Dkt. Reginald Mengi ameipongeza Serikali kwa
kutekeleza ahadi mbalimbali walizojiwekea zikiwezo za elimu bure, ujenzi wa
miundombinu, ununuzi wa ndege pamoja na kukaa na wananchi na wadau mbalimbali
kusikiliza na kutatua changamoto zao.
COMMENTS