Vyombo vya habari nchini hususani redio za kijamii zimetakiwa kuandika habari ambazo zinaelezea changamoto ambazo zinawakabili wana...
Vyombo
vya habari nchini hususani redio za kijamii zimetakiwa kuandika habari
ambazo zinaelezea changamoto ambazo zinawakabili wananchi katika maisha
yao ya kila siku na jinsi ambavyo wanaweza kuzitatua.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.
Anastazia Wambura wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu wajibu
wa redio za kijamii kwa maendeleo vijinini ambayo yamehusisha wasimamizi
wa redio za kijamii na wawakilishi wa Halmashauri wa wilaya hizo ambao
wanawakilisha halmashauri zao katika shughuli za uendeshaji wa redio
hizo za jamii.
Alisema
wanahabari na vyombo vya habari ni muhimu nchini kwa maendeleo ya Taifa
lakini kama wasipokuwa makini katika utendaji wao wa kazi kunaweza kuwa
na madhara makubwa hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanazingatia maadili
ya uandishi wa habari.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi
Kida (wa kwanza kulia) akizungumza na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe. Anastazia Wambura (wa pili kulia) kabla ya
kufungua mafunzo ya siku mbili kuhusu wajibu wa redio za kijamii kwa
maendeleo vijinini ambayo yamehusisha wasimamizi wa redio za kijamii na
wawakilishi wa Halmashauri wa wilaya hizo ambao wanawakilisha
halmashauri zao katika shughuli za uendeshaji wa redio hizo za jamii.
Alisema
sehemu kubwa ya wananchi ambao wanaishi vijijini hawapati taarifa
muhimu zinazohusu maendeleo yao zikiwepo taarifa za kilimo, afya,
mazingira na haki za kibadamu hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanaandika
habari ambazo wananchi wamekuwa hawazipati kwa muda mrefu.
“Ni
jukumu lenu sasa kuhakikisha redio hizo zinatimiza malengo yake hususani
katika kumuelimisha wanajamii, kuwajengea uwezo wa kutambua na
kupambana na mazingira ili kuinua hali zao za kimaisha,” Mhe. alisema
Wambura.
Alisema
mafunzo hiyo ni muhimu kwao kama wawakilishi wa redio za kijamii sababu
itawapa mbinu ambazo wanaweza kuzitumia ili waweze kujisimamia wao
wenyewe bila kuwa tegemezi kwa kuomba fedha kutoka sehemu zingine.
“Natambua
changamoto zilizopo katika uendeshaji wa redio za kijamii ambazo ni
kama upatikanji wa habari endelevu na zinazolingana na mahitaji ya jamii
husika, uhaba wa rasilimali fedha za kuendeshea redio husika, na
udhaifu katika usimamizi stahiki wa taasisi hizo lakini kwa hakika
mafunzo haya ni muhimu kwa vile yanalenga kutatua changamoto hizo,”
alisema Wambura.
Aidha
Naibu Waziri Wambura amewashukuru Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na
Kijamii (ESRF) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa
kutoa mafunzo hayo ambayo yatasaidia kujenga Taifa lenye waandishi na
wasimamizi wa habari wenye weledi na kazi zao pia mafunzo hayo
yanakwenda sambamba na dira ya wizara ya kuwa na Taifa lililohabarishwa
vizuri ifikapo 2025.
Kwa
upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Tausi Kida amesema mafunzo
hayo yamekuja baada ya kufanyika utafiti mwaka 2014 kwa ufadhili wa
UNDP, utafiti ambao ulifanyika kwenye wilaya tano nchini na kugundua
kuwa njia bora ya upashaji habari katika maeneo hayo ni kwa kutumia
redio.
Amesema
baada ya matokeo hayo ya utafiti walipendekeza kuanzishwa kwa redio
jamii katika maeneo ambayo utafiti ulifanyika ili kurahisisha taarifa
mbalimbali za kuelimisha wananchi ambazo zitakuwa chachu kubwa ya
maendeleo kuwafikia wananchi kwa urahisi.
“ESRF
kwa ufadhili wa UNDP ilisimamia uanzishwaji wa redio jamii nne ambazo ni
Redio Unyanja (Nyasa), Redio Bunda (Bunda), Redio Kagera (Bukoba
Vijijini) na Redio Ileje (Ileje) na redio zingine mbili Redio Sengerema
(Sengerema) na Redio Mazingira (Bunda) zilipata misaada mbalimbali kwa
ajili ya kujiendesha,” alisema Dk. Kida.
Mafunzo
hayo yamehusisha wasimamizi wa redio za kijamii kutoka wilaya tano
nchini ambazo ni Ileje, Bukoba Vijijini, Bunda, Nyasa na Sengerema
pamoja na wawakilishi wa halmashauri wa wilaya hizo ambao wanawakilisha
halmashauri zao katika shughuli za uendeshaji wa redio hizo za jamii.
Mkuu
wa Idara ya Maarifa na Ubunifu wa ESRF, Bi. Margareth Nzuki akitoa
taarifa kwa washiriki wa mafunzo kuhusu wajibu wa redio za kijamii kwa
maendeleo vijinini.
COMMENTS