Aagiza Mkuu wa Kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu wa TFS kuhamishwa kituo cha kazi. · Awataka Majangili wachuk...
Aagiza Mkuu wa Kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu wa TFS kuhamishwa kituo cha kazi.
·
Awataka Majangili
wachukue Matrekta wakalime, Ujangili sasa haulipi.
Waziri wa Maliasili
na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ametangaza mabadiliko muhimu katika biashara
ya mkaa nchini na kusema kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu hakuna mkaa wowote
utakaosafirishwa kutoka wilaya moja kwenda nyingine ili kunusuru misitu inayoteketea
kwa kasi hapa nchini.
Amesema hayo leo wakati
akifungua mkutano wa 24 wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na
Utalii uliofanyika katika ukumbi wa LAPF mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wajumbe
mbalimbali kutoka kwenye Idara, Vitengo na Taasisi mbalimbali zilizopo chini ya
Wizara hiyo.
“Kuanzia mwezi Julai
hakuna ruhusa ya kutoa vibali vya kuhamisha mkaa kutoka wilaya moja kwenda wilaya
nyingine, mkaa utachomwa, utauzwa ndani ya wilaya kwa ajili ya matumizi ya
watanzania wanaohitaji nishati ya mkaa, lakini biashara ya mkaa ya kutoa Dodoma
kwenda Dar es Salaam mpaka Zanzibar marufuku.
“Wamekata misitu
yetu yote, mito yetu imekauka, tunashindwa kupata maji ya umwagiliaji kwasababu
watu wengi huko nje wanataka mkaa wetu, Tanzania jamani sio shamba la bibi,
wale wote watakaotoa mkaa kutoka eneo moja hadi jingine kinyume na sheria hii
watashuulikiwa kwa utaratibu wa uhujumu uchumi”, amesema Maghembe.
Amesema kuwa kwa
upande wa miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro na Tanga
vitaanzishwa viwanda maalumu vya kuzalisha mkaa ambao utauzwa kwa vibali
maalumu katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Amesema mkaa huo hautakuwa na
athari nyingi za kimazingira kwa sababu utazingatia taratibu za uzalishaji
endelevu.
Wakati huo huo,
Waziri Maghembe amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
kumuhamisha kituo cha kazi Mkuu wa Kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa
Misitu wa Wakala hiyo, Arjason Mloge kutoka Makao Makuu ya Taasisi hiyo kwenda chuo
cha Viwanda vya Misitu (FITI) kilichopo mkoani Kilimanjaro na badala yake
atafutwe mtu mwingine muaminifu.
Amesema uamuzi huo ni
kufuatia udhaifu uliojitokeza katika usafirishaji wa rasilimali za misitu ndani
na nje ya nchi ikiwemo usafirishaji kwa kutumia nakala za vibali ambazo sio
halisi, yaani “Photocopies”. “Agizo hili litekelezwe mara moja kabla ya saa
sita mchana wa leo na niwe nimepewa nakala ya barua hiyo ya uhamisho” amesema.
Kufuatia uamuzi huo
amepiga marufuku kuanzia leo usafirishaji wa mazao ya misitu ndani na nje ya
nchi kwa kutumia nakala zisizo halisi (Photocopies). Ameongeza kuwa katika
kuunga mkono Sera ya Uchumi wa Viwanda ya Serikali ya awamu ya tano hakuna gogo
litakalosafirishwa kwenda nje ya nchi.
“Wawekezaji
wanahimizwa kujenga viwanda vya kuchakata magogo hayo hapa nchini ili kutoa
ajira kwa Watanzania pamoja na kutoa faida halisi inayotokana na rasilimali
hizo kwenye uchumi wa taifa”, amesema.
Akizungumzia
changamoto ya mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini amesema Sheria ya Uhifadhi
wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 sehemu ya 21 (1) hairuhusiwi kabisha
kuchunga mifugo katika Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na
Hifadhi za Misitu. Amewataka watumishi wa Maliasili kusimamia Sheria hiyo
pamoja na kutoa wito kwa wananchi kuifuata kikamilifu.
Katika hatua
nyingine, Waziri Maghembe amewataka majangili wote nchini kuachana na biashara
hiyo haramu ambayo hailipi kwa sasa na badala yake wachukue matrekta wakalime.
“Mtu ambaye alikuwa
anaishi kwa kutegemea ujangili sasa atafute trekta akalime, kwa sababu akifanya
ujangili tukamkamata tu, na tukimkamata atakaa kwenye hoteli ya mkuu wa
magereza (magereza) kwa zaidi ya miaka 25”.
Aidha, Waziri Maghembe
ametoa pongezi kwa watumishi wote wa Wizara ya Maliasili kwa kazi nzuri wanayofanya
ya kupambana na ujangili nchini pamoja na ulinzi wa maliasili za taifa (Misitu,
Wanyamapori na Mambo ya Kale) ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 20.5 kwenye
pato la taifa. Amesema matokeo chanya ya kupambana na ujangili yameanza
kuonekana japo ujangili bado upo.
Kwa upande wake
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki amemueleza Waziri Maghembe
kuwa maelekezo yote aliyoyatoa yamepokelewa kwa ajili ya kuyafanyiwa kazi, huku
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexandre Songorwa akimueleza
Waziri huyo kuwa watalinda na kusimamia Malisili za Taifa na kwamba katu hawapo
tayari kuandikwa kwenye vitabu kuwa walishiriki katika kutoweka kwa maliasili hizo.
Hamza
Temba
Wizara ya Maliasili na
Utalii
Dodoma
10
Aprili, 2017

COMMENTS