Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akizungumza na Mjumbe Maalum, Balozi Ha...
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine
Mahiga (Mb.) akizungumza na Mjumbe Maalum, Balozi Harro Adt
aliyewasilisha Ujumbe Maalum kutoka kwa Kansela wa Ujerumani, Mhe.
Angela Merkel kwenda kwa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli. Pamoja na mambo mengine walizungumzia pia namna
ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Mazungumzo yakiendelea.
Waziri Mahiga akiagana na Balozi Adt mara baada ya kumaliza mazungumzo.
Waziri
Mahiga (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mjumbe
Maalum, Balozi Adt (wa nne kushoto) pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka
Wizarani pamoja na Ubalozi wa Ujerumani nchini.
===================================================
Mhe.
Waziri Mahiga ameyesema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Balozi Harro
Adt, Mjumbe Maalum wa Kansela wa Ujerumani, Mhe. Angela Merkel kwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli alipofika
Wizarani kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe huo.
Katika
mazungumzo yao, Mhe. Waziri Mahiga alisema kuwa, Ujerumani na Tanzania
zina mahusiano ya kihistoria tangu enzi za ukoloni hadi sasa. Katika
masuala ambayo Tanzania inanufaika na ushirikiano huo ni pamoja na
ujenzi wa miundombinu, maboresho katika sekta ya elimu na mchango katika
uhifadhi wa wanayamapori.
“Uhusiano
wa Tanzania na Ujerumani ni wa kihistoria tangu ukoloni. Hata hivyo
Ujerumani wamejaribu kutafsiri ushirikiano wetu katika misingi bora sasa
kuliko ile ya kikoloni. Ujerumani imekuwa ikiisaidia Tanzania moja kwa
moja katika sekta mbalimbali kama elimu, wanyamapori na miundombinu na
misaada mingine imekuwa ikipitia Umoja wa Ulaya” alisema Waziri Mahiga.
Akizungumzia
ziara ya Balozi Adt nchini, Mhe. Waziri Mahiga alisema Mjumbe huyo
Maalum wa Kansela wa Ujerumani ameleta ombi kwa Mhe. Rais na kwa
Watanzania la kuiunga mkono Ujerumani kwenye nafasi ya Mjumbe asiye wa
Kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa uchaguzi
utakaofanyika mwaka 2018. Aliongeza kusema kuwa, Ujerumani imedhamiria
kugombea nafasi hiyo ikiwa na dhamira ya kuunga mkono mageuzi ndani ya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo kuziunga mkono nchi za
Afrika kwenye harakati za kupatiwa nafasi mbili za kudumu kwenye Baraza
hilo.
Aidha,
Mhe. Waziri Mahiga alifafanua kwamba, katika kufikia malengo hayo
Ujerumani imejiwekea misingi mikuu minne ambayo ni:- Kusaidia jitihada
za amani na usalama duniani; Kusimamia Haki ndani ya Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa; Kuhamasisha mageuzi ya Teknolojia na Kuhimiza
ushirikiano na Ubia wa Kimataifa.
Mhe.
Mahiga alieleza kuwa kwa kuzingatia misingi hiyo, amemueleza Balozi Adt
azma ya Tanzania kuiomba Ujerumani iisadie Afrika kujenga Jengo la
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ambapo Tanzania ndio
Makao yake Makuu huko Mjini Arusha.
Mhe. Mahiga pia alimhakikishia Balozi Adt kuwa ameupokea ujumbe wa Kansela wa Ujerumani na atauwasilisha kwa Mhe. Rais.
Kwa
upande wake Balozi Adt, Mjumbe Maalum kutoka Ujerumani alisema kuwa
amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata baada ya kuwasili nchini. Pia ana
imani kuwa Tanzania ambao ni rafiki wa kihistoria wa Ujerumani itawaunga
mkono kwenye nafasi hiyo ili kuwawezesha kutekeleza malengo
waliyojiwekea ikiwemo kuhakikisha Afrika inapata nafasi mbili za kudumu
kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 12 Machi, 2017
COMMENTS