Balozi wa Sweden Nchini Katarina Rangnitt ameunga mkono jitihada za serikali ya awamu wa Tano katika mapambano dhidi ya ru...
Balozi
wa Sweden Nchini Katarina Rangnitt ameunga mkono jitihada za serikali
ya awamu wa Tano katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi kama hatua
ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii kwa viwango
vinavyotakiwa kote nchini.
Balozi
huyo wa Sweden nchini Katarina Rangnitt amesema hayo 3 March 2017 baada
ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Balozi
Katarina Rangnitt amesisitiza kuwa serikali ya Sweden inafurahishwa
sana na jitihada hizo za serikali ambazo zinalenga kukomesha vitendo
hivyo vya rushwa na mapambano dhidi ya umaskini ili kusaidia wananchi
kuishi maisha mazuri kwa kupata huduma bora zikiwemo za afya,maji na
elimu kwa ubora unaotakiwa.
Balozi
huyo amesema kuwa Sweden itaendelea kushirikiana na serikali ya
Tanzania kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo Tanzania Bara na
Zanzibar kama hatua ya kujenga na kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo.
Kuhusu
mabadiliko ya tabia ya nchi na masuala ya usawa wa kijinsia, Balozi
huyo amesema kuwa nchi yake ipo mstari wa mbele kuhakikisha jitihada za
utunzaji wa mazingira zinaimarishwa hivyo serikali ya Sweden ipo tayari
kushirikiana kikamilifu na Tanzania katika kukabiliana tatizo hilo.
Kwa
upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe
Samia Suluhu Hassan imeipongeza na kuishukuru nchi ya Sweden kwa
ufadhili wake katika bajeti ya kuu serikali na kwenye miradi mbalimbali
ya maendeleo hasa kwenye sekta za nishati,elimu, tafiti na afya.
Makamu
wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amemhakikishia balozi huyo wa Sweden
nchini kuwa serikali ya awamu ya Tano itaendelea kupambana ipasavyo na
vitendo vya rushwa, kuondoa ukiritimba katika sekta mbalimbali nchini
hatua ambazo zitasaidia serikali kupata wawekezaji wengi kutoka mataifa
mbalimbali Duniani kuja kuwekeza hapa nchini.
Amesisitiza
kuwa ili kufikia malengo ya kuwa na Tanzania ya Viwanda Serikali
itaendelea kushirikiana ipasavyo na sekta binafsi ili kuhakikisha
malengo hayo yanafikiwa kwa haraka.
Ameeleza
kuwa Tanzania na Sweden zina mahusiano ya muda mrefu tangu miaka 1930
hivyo ni muhimu kwa mahusiano hayo yakadumishwa na kuendelezwa kwa ajili
ya manufaa ya wananchi wa Tanzania na Sweden.
Kuhusu
uhifadhi wa mazingira na usawa wa kijinsia,Makamu wa Rais Mhe Samia
Suluhu Hassan amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Sweden katika
mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira na masuala ya usawa wa
kijinsia.
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amemweleza balozi huyo kuwa milango ya
ofisi yake ipo wazi muda wote hivyo kama ana jambo zuri na lenye manufaa
kwa taifa au anakwazwa na jambo lolote basi afike ofisi kwake ili
wajadiliane na kuona namna ya kutafutia ufumbuzi.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, (kushoto), akizungumza na Balozi wa Sweden Nchini Katarina Rangnitt Ikulu jijini Dar es Salaam Machi 3, 2017.(PICHA NA VPO)
COMMENTS