WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Bw. Christopher Ole Sendeka kuchukua hatua kali kwa wote waliohu...
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Bw. Christopher Ole Sendeka kuchukua
hatua kali kwa wote waliohusika na upotevu zaidi ya sh. bilioni moja za vyama
vya ushirika.
Waziri Mkuu alitoa kauli
hiyo jana jioni (Ijumaa, Januari 27, 2017) alipozungumza na watumishi wa Mkoa
wa Njombe wakati wa majumuisho
ya ziara yake ya kikazi ya siku saba mkoani hapa.
Alisema kati ya fedha hizo
sh. milioni 532.736 zilipotea katika SACCOS ya Kurugenzi Njombe pamoja na sh. milioni 900 zilizopotea katika
Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo kiitwacho Wafanyabiashara Njombe SACCOS.
“Maofisa
Ushirika nchini mmeendelea kudhoofisha jitihada za Serikali katika kuimarisha
ushirika. Katika eneo hili ninahitaji Mkuu wa Mkoa ufuatilie suala hili na
kuwachukulia hatua wahusiuka wote,” alisema.
Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wote wa Wilaya
kuwatumia warajisi wa ushirika kuimarisha ushirika Mkoani Njombe.”Tunataka
ushirika ulete tija kwa wananchi na hatutaki ushirika ulioambatana na harakati
za kugawa watu. Endeleeni kuwashughulikia wanaushirika wasio waaminifu,”.
Aidha,
Waziri Mkuu aliwasisitiza watumishi wa umma wote nchini kuzingatia uadilifu,
uaminifu, kutojihusisha na rushwa na kutumia ipasavyo fedha za umma Serikali
itachukulia hatua kali dhidi ya watumishi wote wanaotumia nafasi zao
kujinufaisha binafsi.
Alisema
anataarifa za Watendaji wa Wakuu wa Wilaya ya Makete akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri
hiyo Bw. Francis Namsumbo, Mweka Hazina Bw. Edward Mdagachule, Ofisa Utumishi,
Bw. Nicodemas Tindwa na Mkaguzi wa Ndani Bw. Michael Shija kuhusika na upotevu
wa sh. milioni 71 zikiwemo sh milioni 41 za UNICEF.
Waziri
Mkuu alisema kuwa watumishi hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utoaji wa
rushwa kwa vyombo mbalimbali ili kuficha ubadhilifu huo. “Mkuu wa Mkoa
hakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kuhusiana na matukio haya,”.
Pia
alimuagiza Mkuu huyo wa Mkoa kuhakikisha kuwa ……..wa Wanging’ombe Bw. Edwin
Kigoda anachukuliwa hatua stahiki kwa ubadhilifu wa sh. milioni 37.9 zilizotolewa
kwa ajili ya kuwajengea uwezo Walimu katika stadi za Kusoma, Kuandika na
Kuhesabu (KKK).
Mbali
na watumishi hao pia Waziri Mkuu alimtaka Bw. Ole Sendeka kumchunguza na
kumchukulia hatua Ofisa Ardhi wa Mji wa Njombe, Bw. Addo Kabange ambaye
anatuhumiwa kuuza viwanja mara mbili, kuchukua rushwa na kujipatia viwanja
vingi kwa bei nafuu na kuviuza kwa wananchi kwa bei ya juu.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu
alisema atawaelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), Msajili
wa Hazina na Mrajisi wa Ushirika kuanza kufuatilia malalamiko kuhusu umiliki wa
kiwanda cha chai cha Lupembe pamoja na kufuatilia mwenendo wa mgawanyo wa hisa
za kiwanda hicho.
Alisema alipotembelea kiwanda cha chai
cha Lupembe ambapo alifarijika kukuta kiwanda hicho kimeanza kufanya kazi baada
ya kusimama kwa takriban miaka nane kutokana na mgogoro uliopo baina ya
mwekezaji wa Kiwanda hicho na Umoja wa Wakulima wa Chai Muvyulu.
Waziri Mkuu alisisitiza kwamba Serikali
ya Awamu ya Tano haitavumilia migogoro ya kuzuia ajira kwa wananchi, hivyo aliahidi
kushughulikia malalamiko kutoka pande hizo mbili na kutafuta njia ya kutatua
mgogoro uliopo.
Alisema baada ya kusomewa taarifa ya
kiwanda na kwa upande mwingine taarifa ya wanaushirika alibaini kuwepo kwa mgogoro
unaohitaji kutatuliwa ili kuwezesha shughuli za kiwanda kuendelea kwa amani na
usalama.
Aidha, Waziri Mkuu alielekeza shughuli
za ulimaji na uvunaji wa majani ya chai kutoka kwa wakulima na kupeleka katika
kiwanda hicho iendelee na kiwanda kisisimamishe kazi ili kulinda soko la
wakulima na ajira za watumishi wa kiwanda hicho,” alisema.
Alisema kwa kuwa kiwanda hicho kinamilikiwa
kwa ubia, alimwelekeza Mkurugenzi wa kiwanda hicho kuhakikisha kuwa wanaweka
wawakilishi wawili au watatu wa wanaushirika katika Bodi ya Kiwanda hicho.
Katika
hatua nyingine Waziri
Mkuu alizungumzia suala la kuchelewa kuanza kwa mradi wa chuma cha Liganga,
ambapo alisema ucheleweshaji huo si wa makusudi bali ni mpango wa Serikali wa
kujiridhisha na vipengele mbalimbali vya mkataba ili uwe wa manufaa kwa
Watanzania.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema baada
ya kutembelea eneo ambalo uchimbaji utakapofanyika, na kujionea maendelezo ya
wananchi yaliyopo, alipata mashaka na kiasi cha sh. bilioni 13 kilichotengwa na
wawekezaji kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo.
Alisema Serikali haina budi kufanya
tathmini ya kina na kujiridhisha. “Nataka nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge (Deo
Ngalawa-Ludewa) na Mwenyekiti wa NDC kujiridhisha na wahusika wanaotarajiwa
kupata fidia hiyo,”.
Akizungumzia
kuhusu maslahi ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali
kupitia Bodi ya Motisha na Mishahara inaendelea kufanya tathmini ya uzito wa
kazi ili kupanga upya viwango vya motisha na mshahara kwa watumishi wote.
Pia
aliwasisitiza waajiri wote wakiwemo Wakurugenzi kutenga fedha kwa ajili ya
likizo, masomo na uhamisho, kuandaa leave
roster na mipango ya mafunzo kwa watumishi.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI,
JANUARI 28, 2017.


COMMENTS