Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kushoto) akioneshwa Ramani ya Kijiji cha Ololosokwan na Diwa...
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kushoto) akioneshwa Ramani ya Kijiji cha Ololosokwan na Diwani
wa Kata hiyo, Yanick Ndoinyo alipotembelea kijiji hicho hivi karibuni
kuona changamoto za uhifadhi. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha
Ololosokwan, Emmanuel Salteimoi.
Kundi la mifugo likiwa ndani ya Pori Tengefu la Loliondo, karibu kabisa na mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akizungumza
katika kikao cha wadau wa mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo
alichokiitisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo mkoani Arusha hivi karibuni.
NA HAMZA TEMBA - WMU
............................................................................
Serikali
ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli mara tu
ilipoingia madarakani mwezi Oktoba mwaka juzi ilitoa vipaombele vyake
kadhaa vya kutelezwa na wizara zake mbalimbali huku Wizara ya Maliasili
na Utalii ikikabidhiwa majukumu mazito matatu ya kutekeleza katika
kipindi cha uongozi wake.
Wizara
ya Maliasili na Utalii, imesema kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa
malengo yake ya uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Kuendeleza Utalii
pamoja na utekelezaji wa vipaombele ilivyopewa na Serikali ya awamu ya
tano kuwezesha kufikia malengo hayo yanatimia kwa wakati.
Kwa
upande wa utatauzi wa migogoro kwenye maeneo ya hifadhi nchini, Wizara
hiyo imejipanga kuwashirikisha wadau wote wanaohusika na migogoro hiyo
kwa kukaa nao pamoja kwenye vikao vya majadiliano na kuweka mikakati ya
pamoja ya kufikia suluhu ya migogoro hiyo kwa faida ya Serikali na wadau
wote wanaohusika.
Hivi
karibuni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani
alifanya ziara ya kiutafiti katika Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Pori
Tengefu la Liliondo, lengo kuu la ziara hiyo ikiwa ni kuona uhalisia wa
changamoto zilizopo pamoja na kupata taarifa sahihi kutoka kwa wadau
husika, alifanya hivyo bila ya kujitambulisha kwa lengo la kupata
taarifa sahihi kuhusiana na migogoro hiyo.
Akiwa
katika Tarafa ya Loliondo alitembelea kijiji cha Ololosokwan, Pori
Tengefu la Liliondo, sehemu ya mpaka wake na Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti na eneo la muwekezaji, kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) na kampuni ya &Beyond (Kleins Camp).
Akiwa
katika eneo hilo alizungumza na viongozi wa kijiji cha Ololosokwan
ambao waliwasilisha changamoto kadhaa ikiwemo ongezeko la mifugo kutoka
nchini Kenya na vijiji jirani hususani wakati wa kiangazi kwa ajili ya
kutafuta malisho na uelewa tofauti wa mpaka baina ya vijiji na Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti.
Diwani
wa Ololososkwan, Yanick Ndoinyo alisema uhifadhi umekuwa ukiwanufaisha
kwa kiasi kikubwa kwa kuwa kupitia utalii kijiji hicho hupata fedha
taslim zaidi ya shilingi milioni 300 kwa mwaka kupitia mikataba ya
wawekezaji na mgao kutoka Serikalini.
Pamoja
na mchango huo amesema “wawekezaji wa eneo hili wamekuwa wakitekeleza
miradi ya jamii ambapo wamechimba visima vinne, wamejenga madarasa
mawili na kisima kingine kinajengwa jirani na kata hii, lakini kampuni
zote kwa ujumla zinatoa ajira kwa wanavijiji, kwahiyo kwakweli sisi ni
kijiji ambacho tumeona manufaa ya utalii “
Ndoinyo
alisema fedha hizo zimekuwa zikisaidia kusomesha watoto masikini
kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu, kusaidia ujenzi wa zahanati na
huduma nyingine za jamii.
Kwa upande wa kampuni ya Ortello
Business Corporation (OBC) ambao wamewekeza katika pori hilo kupitia
Afisa Mahusiano wao, William Parmat walisema changamoto kubwa
inayowakabili ni ya wananchi kuingiza mifugo katika eneo la uwekezaji
jambo linalosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo wanyamapori
kutoweka.
Muwekezaji
huyo alisema wapo tayari kuweka makubaliano ya uhifadhi na wananchi
pamoja na kusaidia kujenga miundombinu ya huduma za jamii. Alisema
changamoto ya mifugo imesababishwa na msukumo wa baadhi ya asasi za
kiraia kwa wananchi kwamba Serikali inataka kuchukua pori hilo hivyo
waingize mifugo yao kwa ajili ya kulilinda.
Naibu
Waziri Makani aliuahidi uongozi wa kijiji cha Ololosokwan pamoja na
wawekezaji hao kuwakutanisha wadau wote wanaohusika na mgogoro wa pori
hilo kwa ajili kujadili changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wa
kudumu.
Inaelezwa
kuwa eneo la Pori Tengefu la Loliondo lina umuhimu wa pekee katika
uhifadhi kwa sababu ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori, mapito ya
wanyamapori na vyanzo vya maji. Kutokana na sababu hizo, eneo hilo
linapaswa kuendelea kuhifadhiwa ipasavyo, kwa kuwa linachangia kwa
kiwango kikubwa kuimarisha mfumo wa ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti.
Siku
chache baada ya ziara hiyo ya kiutafiti, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
alifanya ziara ya kikazi mkoani Arusha na kuwaagiza viongozi wa Serikali
kukaa pamoja na wadau wanaohusika na migogoro ya ardhi katika Tarafa ya
Loliondo na kuitafutia suluhu ya kudumu.
Baada
ziara hiyo ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri Makani aliendelea na ziara yake
katika tarafa ya Loliondo ambayo aliikatisha kupisha ziara Waziri Mkuu.
Mara hii ziara hiyo ikihusisha pia ufuatiliaji wa maagizo ya Waziri
Mkuu aliyoyatoa kwenye ziara yake mkoani Arusha.
Aliwasili
Loliondo kwa ajili ya kuweka mkakati wa kumaliza changamoto ya mgogoro
uliodumu kwa zaidi ya miaka 25 kati ya mwekezaji, wanavijiji, mashirika
yasiyo ya kiserikali (NGOs), suala la mifugo, uharibifu wa mazingira na
utata wa mpaka wa Hifadhi ya Serengeti na Loliondo.
Tarehe
29 Desemba, 2016 alifanya mkutano na wadau wanaohusika moja kwa moja na
mgogoro wa Loliondo, mkutano huo ulifanyika katika ofisi ya Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo, Kupitia
mkutano huo aliunda kamati maalum ya kutafuta suluhu ya kudumu ya
mgogoro huo.
Kamati
hiyo inahusisha taasisi za serikali, asasi za kiraia, viongozi wa dini,
wazee wa kimila (Leigwanan), viongozi wa vijiji, wajumbe wa kamati
teule ya vijiji 15 ya mpango bora wa matumizi ya ardhi na uendelezaji wa
uhifadhi na wawakilishi wa wanawake na vijana. Aliunda pia kamati ya
kuandaa kanuni za kundesha vikao vya kamati hiyo.
Naibu
Waziri huyo aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, na Mkuu wa
Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Mfaume Taka akateuliwa kuwa Makamu
Mwenyekiti.
“Kamati
ya kanuni itumie muda wa wiki mbili hadi kufikia tarehe 17 Januari,
2017 iwe imeshakamilisha rasimu ya kanuni ili tarehe 18 Januari, 2017
tuzipitie, tuzijadili na kuzipitisha. Hatua itakayofuata ni mawasilisho
ya taarifa mbalimbali kutoka kwa wadau pamoja na majadiliano”, alisema
Makani.
Aliagiza
pia taarifa mbalimbali za kamati zilizowahi kushuulikia mgogoro huo
miaka ya nyuma na mapendekezo yake pamoja na taarifa mbalimbali za
sheria za uhifadhi na vijiji kwa ajili ya kusaidia majadiliano hayo
ziwasilishwe.
Kikao
hicho kilikubaliana kazi hiyo ifanyike ndani ya miezi mitatu hadi
kufikia tarehe 31 Machi, 2017 iwe imekamilika na muafaka upatikane kwa
ajili ya kuishauri Serikali namna bora ya kumaliza mgogoro huo.
Wadau
wote walikubaliana kushiriki vikao vya majadiliano huku wengine
wakipongeza hatua iliyofikiwa na Serikali ya kutaka kumaliza mgogoro
huo, hata hivyo Naibu Waziri Makani alitoa angalizo kwa wadau hao; "Kuna
watu humu ndani na hata nje ambao hawataki tumalize migogoro Loliondo,
nitoe rai kwao, waache chokochoko.
“Wafikishiwe
salamu, tutawabaini, tutawakamata na kuwashitaki kwa kosa la kukwamisha
jitihada za Serikali kuwaletea wananchi maendeleo yao, Wananchi muone
umuhimu wa jitihada za Serikali kumaliza changamoto hii na kutuunga
mkono”, alisema Makani.
Akizungumza
katika mkutano huo, mchangiaji mmoja ambaye hakutambulisha jina lake
alisema “Eneo hili Loliondo lenye kata saba na vijiji 15 lilikosekana
dawati la pamoja, kwa mfumo huu tutaenda mbele, Taasisi nyingi zimekuwa
zikipotosha umma kuhusiana na taarifa za Loliondo, tutashukuru kuona
tunapata muafaka kupitia kamati hii iliyoundwa leo”
Changamoto
ya Mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo ni mkwamo kwa maendeleo ya
wananchi wa Loliondo na Taifa kwa ujumla, Kila mwananchi wa Loliondo ana
nafasi kubwa ya kuhakikisha mgogoro huu unafikia tamati kwa
kushirikiana na Serikali na wadau wengine. Kila mmoja atimize wajibu
wake mgogoro huu utakuwa historia na Loliondo itakua salama na kupiga
hatua kimaendeleo.
COMMENTS