WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Ofisi ya Rais Tawa...
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi pamoja
na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda mkoani
Mtwara kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha shule tisa za
mwisho katika matokeo ya kidato cha pili kutoka mkoani humo.
Pia
ameziagiza halmashauri nchini kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili kuhakikisha
wanawasimamia vizuri walimu jambo litakalowezesha kuboresha ufundishaji na
hatimaye kupata matokeo mazuri.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Januari 17, 2017) wakati akizungumza na
watumishi na wananchi wa mkoa wa Katavi alipowasili Ikulu ndogo ya Mpanda kwa
ajili ya kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya
Manispaa ya Mpanda.
Kwa
mujibu wa matokeo hayo kati ya shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye
mtihani huo, tisa zinatoka katika Mkoa wa Mtwara na moja Tanga. Shule za Mtwara
zilizofanya vibaya ni Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga,
Msimbati, Salama na Lukodoka huku ya Tanga ikiwa ni Nywelo.
“Viongozi
wa Wizara ya Elimu Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waende Mtwara wakafuatilie kwa kina wajue
kuna nini hadi shule tisa kati ya 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya
mitihani ya kidato cha pili mwaka jana zitoke huko,” amesisitiza.
Mbali
na kuuagiza huongozi wa wizara hizo kwenda mkoani Mtwara pia Waziri Mkuu amewataka
wasimamie vizuri mikoa ambayo awali ilikuwa na matokeo mabaya na sasa inafanya
vizuri na wahakikishe shule za mikoa hiyo hazishuki na badala yake ziendelee kupata
matokeo mazuri zaidi.
Awali,
akisoma taarifa ya mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu,
Raphael Muhuga alisema katika matokeo ya mtihani kidato cha pili ya mwaka jana
mkoa wake ulishika nafasi ya pili kitaifa ukiongozwa na mkoa wa Geita.
Alisema
kwa sasa wanajipanga kuhakikisha katika mitihani ya mwaka huu wanashika nafasi
ya kwanza kitaifa, hivyo alitoa wito kwa watendaji wa Idara ya Elimu, wakuu wa
shule, wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha malengo hayo
yanafanikiwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JANUARI 17, 2017.

COMMENTS