Mwanadiplomasia mahiri wa Tanzania aliyepata pia kuwa Katibu Kiongozi-Ikulu, Balozi Ombeni Sefue ameteuliwa kuwa Mtanzania wa kwa...
Mwanadiplomasia
mahiri wa Tanzania aliyepata pia kuwa Katibu Kiongozi-Ikulu, Balozi
Ombeni Sefue ameteuliwa kuwa Mtanzania wa kwanza kuingia katika Jopo la
Watu Mashuhuri katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora
(APRM).
Kwa
mujibu wa Katibu Mtendaji wa APRM tawi la Tanzania, Rehema Twalib
anayehudhuria mikutano ya Umoja wa Afrika na APRM mjini Addis Ababa,
Ethiopia, Balozi Sefue ameidhinishwa kwenye kikao cha juu ya Wakuu wa
Nchi za Umoja wa Afrika ambao ni wanachama wa APRM kilichofanyika juzi
Jumamosi mchana.
“Haikuwa
kazi rahisi kupata nafasi hii. Nchi nyingi za Afrika zilileta majina ya
watu wao mashuhuri ili kuingia katika jopo hili muhimu. Balozi Sefue
licha ya kuwa na utumishi uliotukuka kama mwanadiplomasia mkongwe pia
aliungwa mkono kwa nguvu zote na Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania,”
alisema Katibu Mtendaji huyo.
APRM
ni Mpango wa Afrika uliobuniwa na Wakuu wa Umoja wa Afrika kwa lengo la
kuwa na chombo kitakachosaidia kuhimiza nchi wanachama kuenzi utawala
bora na utoaji wa huduma bora za kiuchumi, biashara na za kujamii kwa
wananchi wao kupitia mfumo wa kujitathmini zenyewe na kukosoana.
Kwa
mujibu wa tovuti ya APRM, Jopo la Watu Mashuhuri ni chombo cha juu cha
kuwashauri Wakuu wa Nchi Wanachama wa APRM katika uendeshaji wa Mpango
huo na husimamia mchakato mzima wa kujitathmini.
Wajumbe
wa jopo hilo ambao hudumu hadi miaka minne hupendekezwa na nchi zao na
baada ya mchakato mrefu wenye ushindani majina ya waliokidhi vigezo
huwasilishwa na kuidhinishwa na na kikao cha juu katika APRM-Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali.
Tanzania
ni miongoni mwa wanachama 35 kati ya nchi 54 wa Nchi za AU zilizojiunga
na APRM na ilijiunga rasmi na Mpango huo tangu mwaka 2004.Tayari
Tanzania ilishafanyiwa tathmini ya kwanza ya utawala bora na inaendelea
kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa.
Katika
mkutano huo Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za APRM Rais Uhuru Kenyatta wa
Kenya aliwapongeza wajumbe wa jopo hilo na kuwata kushiriki vyema katika
kuihuisha APRM na kuwa chombo chenye thamani kubwa kwa Afrika kama
walivyotarajia waasisi wake akina Thabo Mbeki, Olusegun Obasanjo,
Benjamin Mkapa na wengine.
Balozi
Sefue ataungana na wajumbe wengine wapya ambao ni pamoja na Prof.
Ibrahim Agboola Gambari (Nigeria), Balozi Mona Omar Attia (Misri) Bi.
Fatma Zohra Karadia (Algeria), Askofu Don Dinis Salomão Sengulane
(Msumbiji) na Prof. Augustin Loada (Burkina Faso). Wajumbe wa zamani
wanaoendelea ni pamoja na Prof. Youssouf Khayal (Chad) ambaye kwa sasa
atakuwa Mwenyekiti wa Jopo hilo na Brigitte Mabandla (Afrika Kusini)
ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti.
Mkutano
huo pia ulijadili Ripoti za tathmini za nchi katika maeneo anuai ya
utawala bora kwa nchi za Kenya (ikiwa ni ripoti ya pili kuwasilishwa),
Sudan, Chad, Senegal, Djibouti pamoja na ripoti ya utekelezaji ya
Zambia.


COMMENTS