Na Anna Nkinda - JKCI 21/11/2016 Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa kiasi cha shilingi milioni 580 fedha ambazo...
Na Anna Nkinda - JKCI
21/11/2016 Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
imeokoa kiasi cha shilingi milioni 580
fedha ambazo Serikali ingezitumia kwa
kuwapeleka wagonjwa wa moyo 20 nchini
India kwa ajili ya matibabu ambapo kwa kila mgonjwa angegharamiwa kiasi cha
shilingi milioni 29.
Hayo yamesemwa leo na
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alipokuwa akielezea kuhusu
upasuaji kwa wagonjwa wa moyo wanaoufanya hivi sasa kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wa Moyo
kutoka Taasisi ya Open Heart International (OHI) ya Nchini Australia .
Prof. Janabi aliongeza kuwa upasuaji huo wa wagonjwa
unaenda sambamba na utoaji wa elimu kwa wataalamu wa ndani wakiwemo madaktari,
wauguzi, wagavi na mafundi wanaohusika na utengenezaji wa mashine za kimatibabu.
“Idadi ya wagonjwa
watakaofanyiwa upasuaji ambao utachukuwa muda wa siku sita ni 20 kati ya hao
watoto ni 15 na watu wazima ni watano”.
“Tunafanya upasuaji kwa wagonjwa watatu kwa
siku hadi sasa jumla ya wagonjwa nane wameshafanyiwa upasuaji na hali zao
zinaendelea vizuri kati ya hao watu wazima watatu na watoto watano”, alisema
Prof. Janabi.
Alizitaja gharama
wanazolipa wagonjwa hao ni shilingi laki
tano kwa ajili ya vipimo vya maabara hii ni kwa wagonjwa wenye uwezo wa kulipia,
kwa wagonjwa wasio na uwezo wanalipiwa na Serikali, Rotary Club Dar es Salaam
na Bahari Beach na BAPS Charity na
wagonjwa ambao ni wanachama wa Bima ya Afya wanalipiwa na bima zao.
Prof. Janabi alisema, “Wagonjwa
wanaotumia kadi za Bima ya Afya ni wachache, nawashauri wananchi wajiunge na Bima ya Afya kwani gharama za
matibabu ni kubwa na tunakoelekea watu hawataweza kulipa na sisi kama Taasisi hatuwezi
kufanya upasuaji bure kwani tunahitaji kununua vifaa tiba ili tuweze kutoa
huduma nzuri kwa wagonjwa wetu”.
Alizitaja changamoto
wanazikabiliana nazo katika zoezi hilo la upasuaji kuwa ni pamoja na damu kwani
wanatumia damu chupa sita hadi nane kwa mgonjwa mmoja hii inatokana na wagonjwa
kutokuwa na damu ya kutosha.
Tangu mwaka 2015 Taasisi
hiyo imekuwa ikifanya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa kushirikiana na Taasisi
za kimataifa zikiwemo za OHI, Okoa Moyo wa Mtoto (Save Child Heart –SACH) na Mending Kids (MKI) ya nchini Marekani na
madaktari kutoka nchi hizo wamekuwa wakija na vifaa tiba na kijigharamia nauli.
COMMENTS