Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watumishi wa Mamalaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dod...
Baadhi ya Watumishi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu CDA wakimsikilizwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao, Ofisini kwake jijini Dar es Salaam Oktoba 6, 2016.
Baadhi ya Watumishi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu CDA wakimsikilizwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao, Ofisini kwake jijini Dar es salaam Oktoba 6, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Kiwanja
chauzwa kwa sh. milioni 240 lakini zilizoingia CDA ni milioni 6 tu
*Ahimiza
kasi ya upimaji viwanja, asema waliolipa nusu wasinyang’anywe
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera na Bunge), Bw. Uledi Mussa afuatilie malipo ya kiwanja kilichouzwa na CDA
kwa sh. milioni 240 lakini fedha iliyoingia ofisini ni sh. milioni 6 tu.
“Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ninataka ufuatilie mauzo ya
kiwanja namba 26 block AA eneo la Kikuyu East ambacho kimeuzwa kwa sh. milioni
240 lakini fedha iliyoingia CDA ni sh. milioni 6 tu. Nataka kujua nani ameingiza
milioni 6 na nani kachukua hizo sh. milioni 234,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo mchana (Alhamisi, Oktoba 6, 2016)
wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao
Makuu Dodoma (CDA) kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.
Bila kutoa ufafanuzi zaidi, Waziri Mkuu amesema eneo hilo lilipaswa kuwa
na kituo cha mafuta na akataka apatiwe taarifa mapema iwezekanavyo.
Pia amemwagiza Katibu Mkuu huyo afuatilie mkataba wa upangishaji wa jengo
la CDA ambalo wamepangishwa taasisi ya Tunakopesha Limited kwa madai kuwa mhusika
alipewa bure na sasa anataka kulipangisha tena ili apate cha juu.
Waziri Mkuu amewaonya watumishi hao pamoja na viongozi wao waache tabia
ya kushirikiana na madalali kuuza viwanja na akawataka wachape kazi
wakijielekeza na kasi ya Serikali ya kuhamia Dodoma.
“Tabia ya watumishi kushirikiana na madalali kuuza ardhi sasa basi. Hata
hivyo, nimefarijika kukuta mmeanza kuweka mfumo wa kielektoniki katika baadhi
ya huduma. Ni lazima mauzo ya viwanja sasa hivi yafanyike kwa njia ya
kieletroniki, madalali hawana nafasi,” amesisitiza.
Ameutaka uongozi wa CDA uongeze kasi ya upimaji viwanja kwa sababu
mahitaji ni makubwa lakini akaonya kuwa wakati zoezi hilo likifanyika, wananchi
walionunua viwanja na bado hawajamalizia kuvilipia, wasinyang’anywe kwa kigezo
cha kutaka kuwauzia wengine.
“Mimi nataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke. Lakini pia
msitumie fursa hii kuwanyang’anya watu wenye umiliki halali eti kwa sababu
Serikali inataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke,” amesema.
“Kama mtu amepewa offer au
hati yake asinyang’anywe hata kama amelipia nusu asinyang’anywe. Ahimizwe
kumalizia hilo deni na ninyi kazi yenu ni kupima viwanja vingine,” amesisitiza.
“Natambua mnayo benki ya viwanja, lakini inabidi muongeze idadi ya
viwanja vingi zaidi. Tumeita wawekezaji waje kujenga nyumba za kuishi
watumishi, mahoteli na viwanda na maeneo yote haya inabidi yatengwe rasmi,”
amesema.
Amesema jumla ya viwanja 70,000 vimepimwa tangu CDA ianzishwe mwaka 1973.
Amesema kama wataendelea na kasi hiyo wakati mahitaji yameongezeka, itawachukua
zaidi ya miaka 40 kukamilisha mahitaji ya viwanja 100,000 ambavyo vinatarajiwa
kuanza kupimwa hivi karibuni.
Mapema,
akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Eng. Paskasi
Muragili amesema usanifu wa upimaji viwanja 20,000 umekamilika na kwamba wana
lengo la kupima viwanja vingine 100,000 ifikapo Juni 2017.
Waziri Mkuu alitembelea Ofisi ya CDA na kukagua mfumo wa utunzaji
mafaili wa zamani pamoja na uhamishaji wa taarifa za wenye viwanja kwenye mfumo
wa kompyuta. Pia alikagua mifumo ya uuzaji viwanja kwa njia ya mtandao ambayo
hata hivyo bado haijakamilika.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amepokea mchango wa zaidi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Wilaya wa
Kongwa, Bw. Deogratius Ndejembi zikiwa ni kwa ajili ya wakazi wa mkoa wa Kagera
walioathirika kwa tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu.
Pia
Waziri Mkuu amepokea mchango mwingine wa zaidi ya sh. milioni tano kutoka kwa
makundi mbalimbali ya wafanyabiasha wa Manispaa ya Dodoma wakiwemo wamiliki wa
hoteli, nyumba za kulala wageni, waendesha bodaboda na madereva wa daladala.
Akipokea
msaada huo, Waziri Mkuu amewashukuru wafanyabiashara hao na kuwahakikishia
kwamba fedha hizo zitapelekwa mkoani Kagera na kuwafikia walengwa kama
ilivyokusudiwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, OKTOBA 6, 2016
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, OKTOBA 6, 2016

COMMENTS