Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo Bw. Abdul-Razaq Badru akifafanua jambo katika mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam leo (...
HESLB yafafanua vigezo utoaji mikopo
·
Uhakiki wa
wanafunzi wanaoendelea na masomo waja
·
Waliokosa sababu
zatajwa, wapewa nafasi ya kukata rufaa
Na Mwandishi
Wetu
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya
Juu (HESLB) imetoa ufafanuzi kuhusu vigezo inavyotumia katika kuchambua,
kupanga na kutoa mikopo kwa wanafunzi 20,183 (asilimia 74) wa mwaka wa kwanza
hadi sasa kati ya 25,717 iliyopanga kuwapa mikopo katika mwaka huu wa masomo,
2016/2017.
Idadi iliyobaki (asilimia 26) ya
wanafunzi wa mwaka wa kwanza itajazwa na waombaji ambao baadhi ya nyaraka walizowasilisha
zinaendelea kuchambuliwa ili kuthibitisha uhalisi wake na baadhi zitajazwa na
waombaji ambao wanakata rufaa na kuwasilisha nyaraka zinazothibitisha uhitaji
wao kwa mujibu wa vigezo vya mwaka huu.
Aidha, katika mwaka huu wa masomo,
Serikali imepanga kutumia jumla ya Tshs 483 kutoa mikopo kwa wanafunzi 93,295
wanaoendelea na 25,717 wa mwaka wa kwanza.
Katika mkutano na waandishi wa habari
leo (Jumapili, Oktoba 30, 2016), Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq
Badru amesema vigezo vikuu vinavyotumika mwongozo uliotangazwa na Bodi hiyo
wakati ilipotangaza kuanza kupokea maombi mwezi Juni mwaka huu ambao unataja
makundi makuu matatu ya watakaopata mikopo.
Vigezo vilivyotumika kutoa mikopo
Kwa mujibu wa Bw. Badru, kundi la
kwanza linajumuisha wanafunzi waombaji wa mikopo wenye uhitaji maalum kama
wenye ulemavu uliothibitishwa na Waganga Wakuu wa Wilaya na yatima ambao katika
maombi yao waliwasilisha nakala za vyeti vya vifo zilizothibitishwa na makamishna
wa viapo.
“Kundi la pili linajumuisha waombaji wa
mikopo ambao baada ya uchambuzi wa taarifa zao walizowasilisha na baada ya
kulinganisha na gharama za jumla za masomo yao ya sekondari, wamebainika kuwa
wana uwezo mdogo wa kugharamia masomo yao ya elimu ya juu na hivyo kuwa na
uhitaji zaidi wa mikopo,” amesema Bw. Badru.
Katika mkutano huo uliofanyika katika
Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Bw. Badru ametaja kundi la tatu na la
mwisho kuwa linajumuisha waombaji wa mikopo ambao wenye ufaulu wa juu katika
matokeo yao ya kidato cha sita na wamechaguliwa kujiunga na fani za kipaumbele
kwa taifa.
Fani hizo ni Sayansi za Tiba, Ualimu wa
Sayansi na Hisabati, uhandisi wa Kilimo, Mafuta na Gesi na Sayansi za Ardhi,
Usanifu Majengo na Miundombinu.
Makundi ya wanafunzi waliopata mikopo
“Hivyo basi, hadi sasa tumetoa mikopo
kwa wanafunzi 20,183 wakiwemo wanafunzi yatima 4,321, wenye ulemavu 118,
wanafunzi wenye uhitaji waliosomeshwa na taasisi mbalimbali katika masomo ya
sekondari (87), wanafunzi wanaosoma kozi za kipaumbele 6,159 na wanafunzi
wanaosoma kozi zisizo za kipaumbele lakini wanaotoka kwenye familia duni 9,498,”
amefafanua Bw. Badru.
Sababu za kukosa mikopo
Katika mkutano huo, kiongozi huyo wa
HESLB pia ameeleza kwa kina sababu nyingine za waombaji 27,053 ambao
hawajapangiwa mikopo.
Ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na baadhi
ya waombaji (90) kuwa na umri wa zaidi ya miaka 30, waombaji mikopo waliopata
udahili kwa sifa linganishi (equivalent qualifications) na waombaji waliomaliza
masomo ya kidato cha sita zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Kundi jingine la waombaji waliokosa mikopo
katika awamu ya kwanza ni waombaji waliopata nafasi katika vyuo kwa ufaulu wa
mitihani waliyofanya kama watahiniwa binafsi (Private Candidates) na waombaji
ambao hawakurekebisha fomu zao za maombi ingawa waliitwa kufanya hivyo.
Nafasi ya rufaa na uhakiki wa wanafunzi
wanaoendelea na masomo
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji
huyo pia amewataka waombaji ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo
unaotangazwa, kuwasilisha rufaa zao kwa njia ya mtandao utakaofunguliwa kuanzia
katikati ya wiki ijayo.
“Tunafahamu kuwa kuna baadhi ya
wanafunzi wamekosa mkopo kwa kutowasilisha baadhi ya nyaraka ingawa tuliwaomba
kufanya hivyo, hawa na wengine wenye sababu za msingi, watapata fursa ya
kuwasilisha rufaa zao kwa njia ya mtandao na nakala kuzituma kwa utaratibu
tutakaoutangaza wiki inayoanza kesho,” amesema Bw. Badru.
Aidha, katika mkutano huo, Bw. Badru
amesema bodi ya Mikopo inatarajia kuanza kazi kuhakiki taarifa za wanafunzi
wanaoendelea na masomo ambao wanapata mikopo ya elimu ya juu kwa lengo la
kubaini kama ni wana uhitaji wa mikopo hiyo kwa mujibu wa vigezo au hapana.
Katika zoezi hili linalotarajiwa kufanyika
kwa siku 30 kuanzia mwezi ujao (Novemba, 2016), wanafunzi wote ambao ni
wanufaika watalazimika kujaza dodoso maalum litakalokusanya tarifa za kiuchumi
za wazazi na walezi wao ili kuweza kupata uhalisia wa sasa.
“Wanafunzi watakutana na dodoso katika
akaunti zao katika mtandao wetu wa maombi ya mikopo (OLAMS) na watapaswa
kujaza. Wale ambao hawatajaza dodoso hili kwa njia ya mtandao tutasitisha
mikopo yao na wale ambao baada ya uchambuzi tutabaini hawana uhitaji, nao
tutasitisha mikopo yao na watapaswa kuanza kurejesha fedha walizokopokea,’
amefafanua.
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
UFAFANUZI KUHUSU VIGEZO VYA UTOAJI MIKOPO KWA MWAKA WA MASOMO 2016/2017
1.0 UTANGULIZI:
Baada ya kukamilika kwa Awamu ya Kwanza ya upangaji wa mikopo kwa wanafunzi 20,183 kati ya 25,717 wa mwaka wa kwanza wa wanaotarajiwa kupewa mikopo mwaka huu (2016/2017), kumejitokeza taarifa zinazokinzana kuhusu zoezi zima la utoaji wa mikopo.
Taarifa hii inalenga kuongeza uelewa katika maeneo matano ambayo tunaamini kupitia kwenu, yatatoa ufafanuzi kwa waombaji wa mikopo na wadau wengine. Maeneo hayo ni:
- Utaratibu/Mchakato wa uombaji mikopo;
- Vigezo vinavyotumika kupanga na kutoa mikopo kwa mwaka 2016/2017;
- Takwimu na makundi ya waliopangiwa mikopo kwa mwaka 2016/2017;
- Makundi ya waombaji ambao hawajapangiwa mikopo na sababu;
- Hatua zinayofuata;
2.0 UTARATIBU/MCHAKATO WA KUOMBA MKOPO
Kimsingi, maombi yote ya mikopo yalipitia katika hatua kuu zifuatazo:
- Juni 29 – Agosti 11, 2016: Kutolewa kwa tangazo lenye maelezo ya kina ili waombaji wenye sifa wawasilishe maombi yao kwa njia ya mtandao wa Bodi (Online Loan Application and Management System – OLAMS). Maombi yote ya mkopo hufanywa kwa njia ya mtandao;
- Agosti – Septemba, 2016: Uhakiki (verification) wa fomu (hard copies) za maombi ya mikopo zilizowasilishwa kwa njia ya EMS ambao ulifanywa na Bodi ya Mikopo na kubaini kuwa fomu za maombi 10,027 zilikuwa na dosari kadhaa zikiwemo kukosekana kwa viambatanisho muhimu kama vyeti vya kuzaliwa, vifo au nakala za vitambulisho vya wadhamni n.k
Waombaji wote wenye dosari walitakiwa kurekebisha na kuwasilisha nyaraka za ziada katika kipindi cha siku kumi.
- Septemba 30 – Oktoba 10, 2016: Waombaji wa mikopo waliitwa ili kufika au kutuma nyaraka muhimu zilizokosekana katika fomu zao za maombi ya mikopo. Nyaraka hizo ni kama uthibitisho wa vifo vya wazazi, picha ya muombaji, mdhamini n.k,
Hadi mwisho wa zoezi la marekebisho jumla ya maombi 5,443 yalirekebishwa sawa na asilimia 54 ya maombi yote yaliyokuwa na dosari.
2.0 VIGEZO VINAVYOTUMIKA KATIKA KUPANGA MIKOPO
Utoaji wa mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu ulizingatia vigezo ambavyo viliwekwa na Serikali na kutangazwa kwa waombaji. Kwa ufupi, vigezo hivyo vimezingatia yafuatayo:
Vigezo vya utoaji mikopo vinazingatia mambo yafuatayo:
- Uyatima na ulemavu
- Uhitaji wa waombaji wanaotoka katika familia zenye hali duni ya kimaisha hususani waliosoma katika shule za umma
- Vipaumbele vya kitaifa vinavyoendana na mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka mitano, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mafunzo ambayo yatazalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya kitaifa katika fani za kipaumbele kama vile;
- Fani za Sayansi za tiba na Afya,
- Ualimu wa Sayansi na Hisabati,
- Uhandisi wa Viwanda, Kilimo, Mifugo,Mafuta na Gesi Asilia,
- Sayansi Asilia, na
- Sayansi za ardhi, Usanifu Majengo na Miundombinu
3.0 TAKWIMU ZA MAKUNDI YA WANAFUNZI WALIOPANGIWA MIKOPO
Kwa ajili ya kumbukumbu, ni vema kukumbuka kuwa upangaji wa mikopo 2016/2017 umezingatia bajeti ya shilingi 483 bilioni iliyopitishwa na Bunge kwa ajili ya kuwakopesha jumla ya wanafunzi 119, 012 kati yao, wanafunzi 25,717 ni mwaka wa kwanza na wanafunzi 93,295 wanaendelea na masomo katika taasisi mbalimbali nchini.
Baada ya uchambuzi wa maombi ya mikopo kukamilika, jumla ya waombaji 20,183 wamepangiwa mikopo katika Awamu ya Kwanza ambayo imekamilika na orodha zenye majina ya wanufaika hao zimetumwa kwa vyuo walivyopangiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU). Mchanganuo wa idadi hiyo ni kama ifuatavyo: Mgawanyo wa wanufaika
Mgawanyo wa wanufaika
|
Jumla
|
Wadahiliwa yatima waliopata mkopo
|
4,321
|
Wadahiliwa wenye ulemavu
|
118
|
Wadahiliwa waliothibitishwa ufadhilikutoka katika taasisi mbali mbali
|
87
|
Wadahiliwa wahitaji wanaosoma kozi za kipaumbele
|
6,159
|
Wadahiliwa wahitaji wanaosoma kozi zingine wanaotoka katika familia zenye vipato duni
|
9,498
|
Jumla
|
20,183
|
4.0 WAOMBAJI AMBAO HAWAKUPANGIWA MIKOPO NA SABABU ZAO
Waombaji wafuatao hawakujumuishwa katika uchujaji na upangiwaji wa mikopo kwa mujibu wa vigezo na sifa za ukopeshaji (Idadi kwenye mabano).
Kundi la Waombaji
|
Idadi
|
Walidahiliwa ambao hawakuomba mkopo
|
6,581
|
Wadahiliwa waliofuzu kama wahitimu wa binafsi (private candidates)
|
8,781
|
Wadahiliwa waliofuzu kwa vigezo wianishi (‘equivalent qualifications’)
|
9,940
|
Wadahiliwa walioshindwa kukamilisha maombi yao ya mikopo hata baada ya kupewa fursa ya kurekebisha dosari
|
1,416
|
Wadahiliwa na walioomba mkopo waliomaliza kidato cha sita zaidi ya miaka mitatu
|
245
|
Wadahiliwa na walioomba mikopo wenye umri unaozidi miaka 30
|
90
|
Jumla
|
27,053
|
Baada ya uchujaji huu, idadi ya waombaji wenye sifa stahiki ilipungua hadi 30,957 ambao waliingizwa kwenye mfumo wa kuchakata na kupanga mikopo kwa mujibu wa sifa zao na vigezo vilivyowekwa.
5.0 HATUA ZINAZOFUATA
- Kukamilisha Awamu ya Pili
- Baada ya kukamilisha upangaji na utoaji mikopo kwa Awamu ya Kwanza yenye wanafunzi wa 20,391 wa mwaka wa kwanza, Bodi inaandaa Awamu ya Pili ya upangaji mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza ili kukamilisha lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi 25,717 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka huu, 2016/2017.
- Kupokea rufani za waombaji ambao hawakuridhika na matokeo upangaji wa awamu ya kwanza. Zoezi hili la litaanza Nov 2 na kukamilika baada ya siku 90;
- Kuhakiki taarifa za wanufaka wote wa mikopo wanaoendelea na masomo ili kubaini uhitaji wao wa sasa. Wale wanataokutwa na hadhi zisizo stahili, wataondokewa na sifa za kuendelea kupata mikopo na kulazimika kurejesha kiasi watakachokuwa wamepokea tayari, kuanzia Novemba 2016;
- Kufanya uhakiki na uchunguzi wa wanufaika wote waliopata mikopo katika mwaka huu wa 2016-17 ili kubaini wanufaika wasiokuwa na sifa stahiki, zoezi litaanza Novemba 2016;
- Kuhuisha taarifa za wanufaika wote walizotuma wakati wa kuomba na baadae kupangiwa mikopo. Uhakiki huo utafanywa kwa njia ya dodoso. Kila mnufaika atalazimiak kujaza dodoso maalumu kwa njia ya mtandao kupitia katika akaunti yake ya mtandao (Online Loan Application and Management System).
6.0 HITIMISHO
Bodi ya Mikopo inatekeleza sera ya uchangiaji wa gharama za elimu ya juu. Hivyo, wadau mbalimbali wakimwemo wazazi na walezi wanahimizwa kuiunga mkono Serikali katika ugharamiaji wa elimu ya juu, hasa kwa wale ambao hawakupata fursa ya mikopo.
Imetolewa na:
ABDUL-RAZAQ BADRU
MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
OKTOBA 30, 2016

COMMENTS