Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Prof. Innocent Ngalinda akizungumza na washiriki wa mafunz...
Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika
(EASTC) Prof. Innocent Ngalinda akizungumza na washiriki wa mafunzo na
waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mafunzo maalumu ya
Ukusanyaji Takwimu Rasmi uliofanyika leo katika chuo hicho kilichopo
Changanyikeni jijini Dar es salaam.
Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri
wa Kitaalamu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Dkt. Frank Mkumbo
akizungumza na washiriki wa mafunzo na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi
wa mafunzo maalumu ya Ukusanyaji Takwimu Rasmi uliofanyika leo katika chuo
hicho kilichopo Changanyikeni jijini Dar es salaam.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo maalumu ya
Ukusanyaji Takwimu Rasmi wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Chuo cha Takwimu
Mashariki mwa Afrika (EASTC) Prof. Innocent Ngalinda wakati wa uzinduzi wa
mafunzo hayo uliofanyika leo katika chuo hicho kilichopo Changanyikeni jijini
Dar es Salaam.
NA ALBERT FEN
Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika
(EASTC) Prof. Innocent Ngalinda amezindua mafunzo maalumu ya Ukusanyaji Takwimu
Rasmi ambayo yalianza tarehe 17 Oktoba mwaka huu chuoni Changanyikeni jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa mafunzo
hayo, Prof. Ngalinda amesema mafunzo
hayo yameandaliwa kwa nia ya kumpatia mshiriki ujuzi katika ukusanyaji takwimu
kwa ajili ya kuzichakata na kuwa takwimu rasmi.
“Washiriki hawa watafundishwa mbinu
shirikishi, utatuzi wa matatizo mbalimbali wakati wa ukusanyaji takwimu, sensa
na viwango vya tafiti mbalimbali, utunzaji wa Vifaa vya ukusanyaji takwimu kama
vile simu za mkononi na kumpyuta mpakato pamoja
na kubadilisha madodoso ya kawaida na kuwa ya kisasa”, amesema Prof. Ngalinda.
Akizungumzia malengo ya mafunzo hayo Naibu
Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu wa chuoni hapo Dkt.
Frank Mkumbo amesema lengo ni kuwawezesha wakusanyaji takwimu kukusanya takwimu
halisi na zenye ubora kwa ajili ya kupanga mipango mbalimbali ya Maendeleo.
“Lengo
kuu la mafunzo haya ni kuhakikisha kuwa wakusanyaji takwimu rasmi wanakuwa na
weledi wa kutosha katika kukusanya takwimu bora na zenye tija kwa taifa”
amefafanua Dkt. Mkumbo.
Jumla
ya washiriki 110 wamejiunga na mafunzo hayo maalumu ya muda wa miezi miwili kwa
awamu ya kwanza ambayo yatamalizika mwezi Disemba, 2016 na watakaomaliza na
kufaulu watapatiwa cheti cha Ukusanyaji Takwimu. Awamu ya pili ya mafunzo hayo
yanatarajiwa kuanza Novemba mwaka huu na kumalizika Januari, 2017.
COMMENTS