Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Global Fund, Mark Dybul (kulia kwake) kwe...
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Global Fund, Mark Dybul (kulia kwake) kwenye hoteli
ya Windsor Agosti 26,2016.Kushoto kwake ni Balozi wa Tanzania nchini Japan,
Mathias Chikawe. (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Global Fund, Mark Dybul kwenye hoteli ya Windsor Agosti 26,2016
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Global Fund, Mark Dybul kabla ya mazungumzo yao kwenye hoteli ya Windsor
jijini Nairobi, Agosti 26,2016.
**************
WAZIRI MKUU ASHIKIRI MKUTANO WA APRM NAIROBI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania iko tayari kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo ni
wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala
Bora barani Afrika (APRM) ili iweze kuboresha hatua ilizofikia kwenye mpango
huo.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa,
Agosti 26, 2016) wakati akichangia mada katika
Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Mpango
wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM Forum) uliofanyika kwenye
hoteli ya InterContinental jijini Nairobi, Kenya.
“Nitumie fursa hii kukiarifu kikao chako kwamba Tanzania imeshaanza
kutekeleza mpango kazi wa Kitaifa ambao umejikita kutatua changamoto katika
sekta za maji, elimu, kilimo, nishati na miundombinu kama zilivyoainishwa
kwenye kikao cha APRM,” alisema.
“Ili kuhakikisha kuwa zinafanyiwa kazi haraka, changamoto hizi za kisekta zimepewa
kipaumbele kwenye Mpango wetu wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano wa
2016-2021 ambao umejikita zaidi kwenye viwanda,” aliongeza.
Tanzania ilifanyiwa tathmini yake Januari, 2013 kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi
za Umoja wa Afrika kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
Mapema, akifungua mkutano huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema viongozi wa
Afrika hawana budi kukubaliana na kuungana kutafuta suluhisho katika ushindani
wa kibiashara.
Alisema nchi wanachama wa mpango huo hawana budi kujenga umoja kama njia ya
muafaka ya kufikia makubaliano hayo.
Wakati huohuo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema bara la Afrika linakabiliwa na
changamoto 11 (strategic bottlenecks) ambazo zinakwamisha maendeleo ya bara hilo
na akataka zitafutiwe ufumbuzi ili kuzisaidia nchi nyingi barani humo.
Akiwasilisha mada binafsi katika mkutano huo, Rais Museveni alisema kwa
zaidi ya miaka 50, amekuwa kiongozi katika sehemu kadhaa na kwamba amebaini
kuwa changamoto hizo zimezuia ukuaji wa uchumi barani Afrika pamoja na
mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Alisema asilimia kubwa ya changamoto hizo haikupata ufumbuzi hata wakati
malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs) yalipokuwa yanatekelezwa.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni mikanganyiko ya kiitikadi ambayo huzaa
ubinafsi na maslahi binafsi; kuwepo kwa mataifa dhaifu (weak states); nguvukazi
duni (kitaaluma na kiafya), uduni wa miundombinu (barabara, maji, umeme, tehama)
ambao unashindwa kuvutia uwekezaji; uhaba wa viwanda unaolazimisha nchi kusafirisha
mali ghafi na uhaba wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa barani Afrika.
Changamoto nyingine ni uduni wa huduma za kijamii unaosababisha huduma
mbovu kwenye maeneo ya utalii, mabenki na mahoteli; kilimo duni kisichotumia
mbolea, dawa za kuua wadudu, mbegu za kisasa au njia za umwagiliaji; makosa ya
kisera kama vile ubinafishaji au utaifishaji mali zinazomilikiwa na sekta
binafsi; ukandamijazi wa demokrasia na ukosefu wa maadili miongoni mwa watumishi
wa umma.
Naye Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisema kwa vile changamoto hizo zinagusa
nchi nyingi za Afrika, ni vema iundwe timu ya wataalamu watakazipitia zote na
kuainisha zipi zinafaa kufanyiwa kazi na kisha taarifa yao iwasilishwe kwenye
kikao kijacho cha Wakuu wa Nchi wanachama.
Akifunga mkutano huo, Rais Kenyatta aliitaka sekretarieti ya APRM ipitie
changaoto hizo na kuziwakilisha kwenye kikao chao kijacho ambacho alisema
kitafanyika Januari 2017, mjini Addis Ababa, Ethiopia katika tarehe itakayopangwa
baadaye.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, AGOSTI 27,
2016.
COMMENTS