Waziri Mkuu wa Lesotho, Mhe. Dk. Pakalitha Mosisili Na Mwandishi Wetu KIKAO maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali na...
![]() |
| Waziri Mkuu wa Lesotho, Mhe. Dk. Pakalitha Mosisili |
Na Mwandishi Wetu
KIKAO maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali na Kamati ya
Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo ya nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC Double Troika) kimeiagiza Serikali ya
Lesotho iwe imetangaza matokeo ya Tume iliyoundwa kuchunguza matatizo ya
kisiasa nchini humo ifikapo Februari Mosi, mwaka huu.
Agizo hilo lililotolewa kwa Waziri Mkuu wa Lesotho, Dk. Pakalitha Mosisili katika kikao cha SADC Double Troika
kilichofanyika mapema wiki hii Gaberone, Botswana, chini ya Mwenyekiti
wake, Luteni Jenerali Seretse Khama Ian Khama ambaye pia ni Rais wa nchi
hiyo.
SADC Double Troika ni kikao maalum cha Wakuu wa Nchi
na Serikali (SADC Summit) na wakuu wa nchi wanaounda Kamati ya Siasa,
Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security
Cooperation) kilichofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa
(GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Pamoja na kutaka Lesotho itangaze matokeo ya tume hiyo, SADC Double Troika
iliitaka nchi hiyo iandae mchakato wa kueleza njia za utekelezaji wa
mageuzi kama yalivyopendekezwa kwenye ripoti ya tume hiyo ifikapo
Agosti, mwaka huu.
“Vilevile, nchi ya Lesotho inatakiwa kuandaa mazingira
wezeshi yatakayotoa nafasi kwa viongozi wa upinzani na baadhi ya maofisa
wa kijeshi wanaoishi uhamishoni ambao walikimbia machafuko, waweze
kurejea nyumbani,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na sekretariati
ya SADC siku moja baada ya kikao hicho kumalizika.
Mkutano huo wa Botswana ulihudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli; Rais
wa Botswana, Luteni Jenerali Khama; Rais wa Afrika Kusini, Bw. Jacob
Zuma; Rais wa Msumbiji, Bw. Filipe Jacinto Nyusi; Waziri Mkuu wa
Swaziland, Dk. Barnabas Dlamini na Waziri wa Mambo wa Nje wa Zimbabwe,
Bw. Simbarashe Mumbengegwi ambaye alimwakilisha Rais Robert Mugabe wa
nchi hiyo.
SADC Double Troika ni mkutano unaohusisha viongozi
wakuu watatu wanaoongoza chombo cha ushirikiano wa siasa, ulinzi na
usalama na wengine watatu kutoka kwenye Mkutano wa wakuu wa nchi
wanachama wa SADC. Hawa wanawakilisha mwenyekiti aliyepo madarakani,
mwenyekiti aliyemaliza muda wake na mwenyekiti ajaye ambaye huwa ni
makamu mwenyekiti.
Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini,
Balozi Radhia Msuya, chini ya muundo wa SADC, kuna mambo makuu mawili;
la kwanza likiwa ni utangamano wa kikanda ambao unasimamiwa na mkutano
wa wakuu wa nchi (SADC Summit) na la pili ni la siasa, ulinzi na usalama
ambalo linasimamiwa na chombo maalum (SADC Organ).
Akifafanua zaidi, Balozi Msuya alisema wajumbe wa mkutano wa SADC Organ
ni Msumbiji (Mwenyekiti); Afrika Kusini (Mwenyekiti aliyemaliza muda
wake) na Tanzania inayotarajia kuchukua uenyekiti wa chombo hiki ifikapo
Agosti, 2016. Botswana, Zimbabwe na Swaziland ndizo zinaunda SADC Summit.
Mapema, kikao hicho, kilipokea taarifa ya msuluhishi
wa SADC kwenye mgogoro wa Lesotho ambaye pia ni Makamu wa Rais wa
Afrika Kusini, Dk. Cyril Ramaphosa ambayo iliainisha mambo kadhaa
yakiwemo ya kikatiba na kiusalama ndani ya nchi hiyo.
Dk. Ramaphosa alitakiwa kuhakikisha kuwa mgogoro huo
uliovihusisha vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi ya Lesotho,
unatatuliwa kwa njia ya mazungumzo kati ya wadau husika ili kuhakikisha
kuwa nchi hiyo inarudi kwenye hali ya amani - kisiasa na kiusalama.
Mgogoro wa Lesotho umehusisha kuuawa kwa aliyekuwa Mkuu wa
Majeshi ya Lesotho, Luteni. Jenerali Maaparankoe Mahao, mnamo Juni 25,
2015. Pia baadhi ya wananchi wanadaiwa kutiwa vizuizini na wengine
kuwekwa ndani.


COMMENTS