POLISI TANZANIA KUANDAA MICHEZO YA MAJESHI YA POLISI KWA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI. Na Jeshi la Polisi. Michezo ya pili ya Majeshi ya P...
POLISI TANZANIA KUANDAA MICHEZO YA MAJESHI YA POLISI KWA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI.
Na Jeshi la Polisi.
Michezo ya pili ya Majeshi ya Polisi kwa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO Games 2018) inatarajia kutimua vumbi jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 6 mpaka 12 mwaka huu katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nchi 14 tayari zimethibitisha kushiriki.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Maandalizi ya Michezo hiyo kinachofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili, Mkuu wa Utawala ndani ya Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Leonard Paul amesema lengo la michezo hiyo kuimarisha ushirikiano na kubadilishana mbinu za kupambana na uhalifu kupitia michezo.
DCP Paul amesema Jeshi la Polisi Tanzania tayari limeanza maandalizi ili kuhakikisha kuwa michezo hiyo inafana na ushindi unabaki hapa nyumbani na ili kufikia lengo hilo wanamichezo hao wanatarajia kuingia kambini hivi karibuni ili wapate muda mrefu wa kujiandaa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Michezo hiyo Naibu Kamishna wa Polisi DCP Daniel Nyambabe alisema wadau mbalimbali wanakaribishwa kufadhili michezo hiyo ambapo alizitaja nchi zinazotarajia kushiriki kuwa ni pamoja na Burundi, Comoro, Djibout, DRC Congo, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Uganda, Rwanda, Sudan, Sudani Kusini, Somalia, Shelisheli na mwenyeji Tanzania.
Mwaka jana michezo hiyo ilifanyika Kampala Uganda na Polisi Tanzania walishika nafasi ya tatu katika ushindi wa jumla na nafasi ya kwanza ilichukuliwa na mwenyeji Uganda na ya pili ilikwenda Kenya.
COMMENTS