KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA Simu: 255-22-2114512, 2116898 E-mail: press@ikulu....
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Aprili, 2018 amefanya mazungumzo na Kamishna wa amani na usalama wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Mhe. Balozi Smail Chergui ambaye amewasilisha ujumbe wa Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo Mhe. Moussa Faki Mahamat.
Mhe. Chergui amesema katika mazungumzo yake na Mhe. Rais Magufuli yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, wamejadili kuhusu masuala yahusuyo amani na usalama barani Afrika hususani ukanda wa maziwa makuu pamoja na masuala ya wakimbizi.
Mhe. Chergui amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushauri wake na mchango wake wa mawazo na uzoefu, wenye lengo la kuimarisha amani na usalama.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Msaidizi wa Rais wa Misri na Waziri Mkuu Mstaafu wa Misri Mhe. Ibrahim Roshdy Mahlab ambaye amewasilisha ujumbe kutoka kwa Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah el-Sisi.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Mahlab amesema katika mazungumzo yake na Mhe. Rais Magufuli wamejadili namna ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Misri, hasa ikizingatiwa kuwa zipo fursa nyingi ambazo nchi hizi mbili marafiki zinapaswa kuzifanyia kazi.
Mhe. Mahlab amebainisha kuwa utekelezaji wa makubaliano yaliyowekwa wakati wa ziara ya Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah el-Sisi hapa nchini umeanza ambapo tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya nchi hizi imeshakutana nchi Misri na kuainisha maeneo yenye fursa na yanayopaswa kufanyiwa kazi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Aprili, 2018
![]() |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Kamishna wa Amani na Usalama wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Balozi Smail Chergui Ikulu jijini Dar es Salaam.
|
COMMENTS