Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipita kwenye gwaride la Kimya lililoandaliwa kwa heshma...
![]() |
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na wananchi wa mpakani Mutukula upande wa Tanzania mara baada ya kuwasili
akitokea Uganda.
|
![]() |
![]() |
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na
viongozi wakuu wa Majeshi ya Uganda mara baada ya kumaliza ziara yake nchini
Uganda.
|
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 11 Novemba, 2017 amemaliza ziara rasmi ya kiserikali ya siku 3 nchini Uganda na kurejea nchini Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli ameagana na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika Mji wa Masaka na baadaye kusindikizwa na Makamu wa Rais wa Uganda Mhe. Edward Kiwanuka Sekandi hadi Mutukula, mpakani mwa Tanzania na Uganda.
Kabla ya kuagana na Mhe. Rais Magufuli, Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ametoa tamko la kulaani uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ambayo imemuagiza mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo kuanzisha uchunguzi dhidi ya mgogoro wa Burundi.
Majaji wa ICC wametoa uamuzi huo juzi tarehe 09 Novemba, 2017 na kumtaka mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo kuchunguza vitendo vya kihalifu dhidi binadamu vilivyotokea nchini Burundi tangu ulipozuka mgogoro nchini humo miaka miwili iliyopita.
Katika tamko hilo Mhe. Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema ICC inaingilia mambo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bila kuwahusisha viongozi wa Jumuiya hiyo jambo ambalo sio sahihi na linarudisha nyuma juhudi za kutafuta amani ya Burundi.
Akizungumzia uamuzi huo Mhe. Rais Magufuli amesema hatua hiyo inarudisha nyuma hatua zilizochukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo iliunda Kamati ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi inayoongozwa na Mhe. Rais Museveni na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa.
Mhe. Rais Magufuli amesema hali ya Burundi sio mbaya kama inavyotangazwa kwa kuwa tayari wakimbizi wengi waliokuwa Tanzania wamerejea Burundi na wengine wanaendelea kurejea, na pia viongozi wanaosuluhisha mgogoro huo wamepanga kukutana tarehe 23 Novemba, 2017 kwa lengo kuendeleza mchakato wa kutatua mgogoro huo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Masaka, Uganda
11 Novemba, 2017
COMMENTS