Na Mwandishi Wetu WAFANYABIASHARA wenye kulipa kodi na kuingizia serikali mapato kwa wakati ndio watakaopata nafasi ya kuwekeza kwe...
Na Mwandishi Wetu
WAFANYABIASHARA wenye kulipa kodi na
kuingizia serikali mapato kwa wakati ndio watakaopata nafasi ya kuwekeza kwenye
jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA-TBIII), imeelezwa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano),
Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye alipofanya ziara ya kutembelea Makao Makuu ya
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na kumalizia TBIII.
Mhandisi Nditiye amesema baada ya kukamilika
kwa jengo hilo baadaye mwakani, wafanyabiashara watakaopewa kupaumbele hususan
waliopo kwenye Jengo la zamani (TBI) na jengo la pili (TBII) ni wale tu
wanaozingatia ulipaji wa kodi na mapato yote ya serikali kwa wakati.
“Tunajua wapo wengi waliojitokeza kuomba
maeneo ya kufanya biashara, lakini wale ambao watahama kutoka majengo yetu haya
mawili la TB I na TBII tunawaambia wazi kabisa kuwa wale waaminifu na waadilifu
wenye kulipa kodi ya pango na mapato mengine ya serikali kwa wakati ndio
wanafikiriwa kwanza, na wale wasiolipa kwa wakati hawatapewa nafasi kabisa ya
kuwekeza kwenye jengo hili,” amesisitiza Mhe. Nditiye.
Hata hivyo, Mhe. Nditiye amesema tayari
ameuagiza uongozi wa TAA kuhakikisha wanapitia mikataba yote ya biashara kwenye
majengo hayo ya abiria na kutengeneza upya ile yenye matatizo ili iweze kuleta
tija kwa taifa, kwani kwa sasa kumekuwa na mikataba ya hovyo.
Amesema TBIII inafursa za biashara ambapo
inaeneo kubwa la kujenga hoteli, migahawa na sehemu za kupumzikia watu, hivyo
kuwataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza.
“Juzi tu nilikutana na Wajerumani nikawaeleza
tunaeneo la uwekezaji hapa TBIII na kule Msalato mnapotarajia kujenga kiwanja
cha kimataifa, na wameonesha nia ya kuja kuwekeza, nia ya serikali na tupo
pamoja katika uwekezaji wa maeneo yetu mbalimbali, ili kujiimarisha katika
uchumi,” amesema Mhandisi Nditiye.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw.
Richard Mayongela amesema kuwa wanatarajia watoa huduma na wafanyabiashara
watakaokidhi vigezo na masharti ya kutoa huduma bora ndio wakaopata nafasi
kwenye jengo hilo la tatu.
“Pia tunatarajia watoa huduma na
wafanyabiashara ni wale wanaokodhi vigezo kwa hiyo yote yanalenga katika
kuhudumia watanzania na kukuza sekta ya usafiri wa anga na kuhudumia vizuri
wale wanaopita hapa,” amesema Bw. Mayongela.
Amesema jengo hilo likikamilika litakuwa na
uwezo wa kuhudumia abiria takribani milioni sita (6) kwa mwaka ambalo ni
ongezeko kubwa ukilinganisha na jengo la sasa la TBII linauwezo wa kuihudumia
kati ya abiria milioni 1.2 hadi 1.5 kwa mwaka.
Hivyo tunaishukuru serikali kwa kutupa
ushirikiano katika kuendeleza viwanja vya ndege, pia kwa upande wa TAA wamekuwa wakifanya
matengenezo madogo madogo kwa kutumia fedha za bajeti ya ndani.
Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa ameitaka TAA kuwaondoa wafanyabiashara
wote wasiolipa kodi na mapato mengine ya serikali kwa wakati, kutokana na
kukwamisha juhudi za serikali za ukusanyaji mapato.
![]() |
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), (mbele katikati), Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye akiongea na Menejimenti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Makao Makuu, kabla ya kuanza kwa ziara ya kutembelea majengo matatu ya abiria ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Oktoba 24 2017.
COMMENTS