Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu . Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) tumepokea taarifa z...
Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) tumepokea taarifa za kukamatwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Chama chetu na Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) Kwa masikitiko makubwa.
Tabia hii ya ubabe na uonevu ya Polisi inaonekana kuota mizizi na kutaka kufanywa kuwa utamaduni na utaratibu wa Jeshi la Polisi kujiamulia kumkamata kiongozi yeyote wa CHADEMA pale atakapoikosoa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli.
Utamaduni huu ni wa kidikteta, kibabe na unaokiuka misingi ya Utawala Bora na haki ya kutoa maoni kwa mujibu wa Katiba.
Moja ya misingi mikuu ya taifa la kidemokrasia ni kuwa na Uhuru wa kujieleza na kutoa maoni au mawazo tofauti na hili ni lazima Serikali ikubali kukosolewa na kusikia upande mwingine una fikra gani juu ya mambo yanayotekelezwa na Serikali.
BAVICHA tumewahi kusema ubabe huu na uonevu huu unaivimbisha nchi, unaitikisa nchi, Rais Magufuli amejivika joho la ubabe na uonevu na kuvunja Katiba ya nchi na kukiuka misingi ya utawala bora.
Tunarudia kumtaka Rais Magufuli kukubali kusikia kutoka kwa watu wasiokuwa wa Chama chake hususani CHADEMA.
Tunalitaka Jeshi la Polisi kufuata misingi ya kuanzishwa kwake, lisimamie uwepo wake ambao ni kulinda raia na Mali zao. Hiki ambacho Jeshi hili linafanya ni kinyume cha sheria ya Jeshi la Polisi nchini (PGO) na hivyo tunamtaka IGP Sirro kuwaelekeza watendaji wake kutimiza wajibu wao na sio kusubiri kuwakamata viongozi wa CHADEMA.
Itafika hatua tutashindwa kuendelea kuvumilia ubabe huu tutalazimika kujitetea kwa mujibu wa misingi ya Tamko la haki za Binadamu
Polisi wenye ndimi mbili ni hatari Kwa Taifa Kwani Jana RPC Dodoma alisema Polisi hawana sababu ya Kumkamata na Leo Polisi Dar es Salaam wanamkamata, Jeshi linapoteza heshima yake ya kuaminika Kwa wananchi. Tunawataka waseme ukweli kwani sheria za Dodoma na Dar ziko tofauti ?. Wanatufundisha kuwa hawaaminiki!
Tunawataka watanzania wote hususani Vijana kusimama upande wa Haki, tusikubali misingi ya Taifa letu kutikiswa.
Hakika tutashinda.
_________________
Julius Mwita
Katibu Mkuu - BAVICHA.
COMMENTS