NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR. KATIBU wa NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu amewataka viongozi na wat...
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
KATIBU wa NEC, Idara
ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu amewataka viongozi na
watumishi wa Chama na Serikali kubuni miradi na fursa zitakazosaidia kukuza kipato
cha wananchi.
Alisema Viongozi Wakuu wa Kitaifa wamekuwa wakisisitiza suala
la ubunifu kwa watumishi wa umma ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa
majukumu ya watumishi hao kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa.
Kauli hiyo ameitoa ofisini kwake Kisiwandui Mjini Unguja, alieleza kwamba ajenda ya maendeleo
ya nchi inamgusa kila mtu hasa watumishi waliopewa dhamana ndio wanaotakiwa
kupanga mikakati ya kiuchumi kwa kuwahasisha wananchi watumie fursa
zilizowazunguka zikiwemo ujasiriamali, kilimo, uvuvi na ufugaji kujipatia kipato cha halali.
“Nchi yetu inapita katika kipindi kigumu cha kutoka katika uchumi
wa Kati kwenda uchumi wa juu unaotegemea viwanda na masoko ya kimataifa ya
ndani ya nchi, yote hayo yanahitaji ushirikiano wa kiutendaji miongoni mwetu.”,
alisema Waride.
Pia alieleza kwamba wananchi wataendelea kuwa na imani na Chama
cha Mapinduzi endapo serikali zote mbili zitaendelea kuwa karibu na wananchi kwa kutatua kwa wakati kero
na matatizo yanayowakabili.
Aidha alisema lengo la CCM ni kuendeleza utamaduni wa kuenzi
demokrasia ndani na nje ya taasisi hiyo, sambamba na kuzishauri serikali
zitekeleze sera za maendeleo kwa wananchi wote bila ubaguzi wa kisiasa na
kidini.
Akizungumzia mipango ya chama hicho kwa sasa kuwa ni
kufanikisha Uchaguzi wa ndani ya taasisi hiyo ambao kwa sasa unafanyika kwa
ngazi za jumuiya na matawi yake ili kupata
viongozi na watendaji watakaotekeleza majukumu ya CCM kwa ufanisi ndani
ya miaka mitano ijayo.
Katibu huyo alisema mpango mwingine ni kusimamia kwa nguvu
zote utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho, sambamba na kuandaa
mazingira bora ya kisiasa yatakayosaidia wananchi kuichagua CCM kwa kura nyingi
katika uchaguzi mkuu wa 2020.
Hata hivyo alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye pia ni
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi zake za kupambana
na vitendo vya ubadhirifu wa rasilimali za Taifa.
COMMENTS