Mkuu wa kitengo cha Kodi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Dennis Masami akitoa mada kuhusu Maana na Umuhimu wa ulip...
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa tahadhari kwa wadaiwa wa kodi ya pango la Ardhi kwa kutoa elimu ya kuhusu dhana ya Kodi hiyo.
Hivi karibuni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa mafunzo mafupi kwa waandishi wa habari kwa nia ya kuhamasisha ulipaji wa kodi ya pango la Ardhi na kubainisha utofauti wake kati ya kodi hiyo na Kodi ya Majengo ambayo hukusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA).
Akizungumza na waandishi wa habari; Mkuu wa Kitengo cha Kodi; Dennis Masami alisema; Dhana ya ulipaji wa kodi ya pango la Ardhi inatokana na Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 katika fungu la 3 kifungu kidogo cha 1 (a) kinachosema: ‘Itambulike kuwa ardhi yote ya Tanzania ni mali ya Umma iliyowekwa chini ya Mheshimiwa Rais kama mdhamini kwa niaba ya wananchi’’
Aliendelea kusema kuwa; Mfumo huu wa umiliki wa ardhi unatambulika kama lease hold na sio free hold, ambapo aina hii ya umiliki ni upangaji katika ardhi, ambao mpangaji anawajibika kufuata masharti ya upangishaji, mojawapo ya masharti hayo ni kulipa pango la kipande cha ardhi. Ambayo Mmiliki ni Rais kwa niaba ya umma na mpangaji ni Mwananchi.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mhe. William Lukuvi ametoa tahadhari kwa wasiolipa Kodi ya Pango la Ardhi akisema; “Wale wote ambao hawajalipa Kodi ya Pango la Ardhi, wote wanao miliki viwanja na mashamba yaliyopimwa, wahusike kulipa kabla ya mwisho wa mwezi wa sita (6). Ifikapo tarehe 30/06 hatua zifuatazo zitachukuliwa dhidi yao; Watashitakiwa Mahakamani, Mali zao zikamatwe na majengo yapigwe mnada kupitia madalali na Miliki zao zifutwe.
Alisema hatua hizo zote zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria, na kutoa tahadhari kuwa kila mmoja achukue hatua ya kulipa kwa hiari kwa Maendeleo ya Taifa.
(Na kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi)
COMMENTS